
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abbas Araqchi, amefika katika mji wa Islamabad, Pakistan na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu nchini humo.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran, ambaye ameanza ziara ya nchi tatu za kieneo amefanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Pakistan akiwemo Mkuu wa Jeshi la Pakistan jijini Islamabad.
Baada ya ziara yake nchini Pakistan, Araqchi ataelekea Oman na kisha baada ya hapo atatemebelea Russia.
Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, hakuna mkutano uliopangwa kati ya maafisa wa Iran na Marekani katika safari ya Araqchi nchini Pakistan, kwani mashauriano yanajikita kwenye juhudi za kudumisha amani ya kikanda.
Hapo awali, Shirika la Habari la Tasnim lilikanusha taarifa iliyokuwa imeripotiwa na CNN, iliyodai kwamba mwanadiplomasia mkuu wa Iran angefanya mazungumzo na maafisa wa Marekani wakati wa ziara yake.
Shirika hilo limebaini kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atafanya mazungumzo na upande wa Pakistan kuhusu msimamo na tathmini ya Iran juu ya namna ya kukomesha kikamilifu vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mnamo Februari 28, Marekani na utawala wa Israel walianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran, ambayo yalipelekea kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na makamanda waandamizi wa kijeshi, wasomi na raia wa kawaida wakiwemo watoto wa shule.
Vikosi vya Ulinzi vya Iran vilijibu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kwa muda wa wiki kadhaa, yakilenga maeneo ya kijeshi ya Marekani na Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na eneo la Ghuba ya Uajemi, na kusababisha hasara kubwa katika zaidi ya awamu 100 za mashambulizi ya kujibu ndani ya siku 40.
Machi 8, kupitia upatanishi wa Pakistan, usitishaji mapigano wa wiki mbili ulifikiwa, na kufungua njia kwa mazungumzo ya Islamabad. Katika mazungumzo hayo, Iran iliwasilisha mapendekezo ya hoja kumi, yakiwemo kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo na kufutwa kwa vikwazo.
Jamhuri ya Kiislamu imekataa kurejea kwenye mchakato wowote wa mazungumzo iwapo Marekani haijaondoa mzingiro wa baharini inaowekea meli na bandari za Iran, ambao ni kinyume cha sheria.
Iran pia imesisitiza kwamba mradi mzingiro huo bado unaendelea, haina nia ya kufungua tena Lango-Bahari la Hormuz, njia muhimu ya kimkakati ambayo imeifunga kwa usafiri wote wa baharini kama hatua ya kujibu mashinikizo hayo.