Kahama. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, imeanza uchunguzi wa madai ya kuwepo kwa kikundi cha watu wanaotoza ushuru kwa wafanyabiashara wa samaki katika Soko la Namanga, Manispaa ya Kahama, kinyume na utaratibu.

Uchunguzi huo umeagizwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kikundi kinachojulikana kama Umoja wa Wauza Samaki Kahama (Uwasaka), kinachodaiwa kutoza ushuru kwa kutoa stakabadhi za mkono, kinyume na mfumo rasmi wa kodi na tozo za serikali.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo leo Aprili 25, 2026, Nkinda amesema hali hiyo haikubaliki na ameielekeza Takukuru kufanya uchunguzi wa haraka kubaini uhalali wa kikundi hicho pamoja na kuwepo kwa ukosefu wa uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

“Naiagiza Takukuru pamoja na wataalamu husika kufuatilia tuhuma hizi haraka na kuniletea uhalisia pamoja na ushauri wa namna ya kumaliza mgogoro huu,” amesema Nkinda.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda, akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Namanga katika Manispaa ya Kahama kwenye mkutano wa kusikiliza na kutatua kero zao. Picha na Amina Mbwambo.

Aidha, ameagiza ukusanyaji wa takwimu sahihi za mapato yanayokusanywa sokoni hapo ili kusaidia kufanya maamuzi ya haki na yenye tija.

Baadhi ya wafanyabiashara wa samaki, akiwemo Irene Mugwa, wamesema wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa ushuru usio rasmi.

Mugwa amesema licha ya kuwa na mtaji wa Sh500,000, analazimika kulipa hadi Sh390,000 kwa mwezi kwa kikundi hicho.

“Mtaji wangu ni laki tano, lakini kwa mwezi nalipa ushuru laki tatu na tisini. Bado sijamlipa mfanyakazi, sasa nabaki na nini? Ukijaribu kuhoji unasimamishwa kufanya biashara,” amesema.

Amehoji uhalali wa kikundi hicho, akisisitiza kuwa soko ni la kila mfanyabiashara anayefuata sheria za nchi.

Mfanyabiashara mwingine, Jonas Mosses, ameomba Serikali kuchunguza mfumo wa ukusanyaji wa ushuru ili kuhakikisha unakuwa wa haki, uwazi na unaozingatia uwezo wa wafanyabiashara wadogo.

Amesema licha ya makusanyo ya kila siku, hawapati taarifa ya mapato na matumizi ya fedha hizo wala kunufaika nazo.

“Sisi hatufuatiliwi kwa chochote. Mapato wanayachukua wao wenyewe, na mwisho wa mwaka wanagawana. Hakuna uwazi wala mrejesho kwa wafanyabiashara,” amesema.

Ameongeza kuwa kuna zaidi ya watu 40 wanaohusika na ukusanyaji, huku wafanyabiashara halisi wakiwa wachache.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Namanga, Juma Jumeju, amesema mfumo wa ukusanyaji mapato kupitia kikundi cha Uwasaka ulianzishwa ili kuleta utaratibu na kuondoa changamoto za awali za ukosefu wa utulivu sokoni.

“Katika kipindi ambacho soko halikuwa na utulivu, tuliingia ubia na wafanyabiashara wa samaki kuunda kikundi kilichosajiliwa kisheria ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato. Sasa kinachoendelea kinashangaza,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *