
Dar es Salaam. Mamlaka zenye jukumu la kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele, likiwamo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zinatajwa kutotekeleza wajibu wake wa udhibiti kikamilifu, huku wananchi wakiendelea kuripoti usumbufu kutoka maeneo ya burudani yaliyopo katikati ya makazi yao.
Mamlaka zingine ni za Serikali za mitaa pamoja na kamati za mazingira katika ngazi za kijiji, mtaa na kata.
Ingawa taasisi hizo na viongozi wake wamechukua hatua mbalimbali, zikiwamo kampeni za uhamasishaji kwa umma na kufunga baadhi ya maeneo yaliyobainika kukiuka sheria, kelele zilizopitiliza bado zinaendelea kuwa tatizo kama inavyobainishwa na uchunguzi uliofanywa na Mwananchi.
Kwa mujibu wa sheria zilizopo, ikiwamo Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2025, pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Viwango vya Kudhibiti Uchafuzi wa Kelele na Mitetemo) za mwaka 2015, kila taasisi inapaswa kutekeleza wajibu wake katika ngazi husika kabla ya mashauri kuwasilishwa NEMC.
Uwepo wa malalamiko kutoka kwa wananchi unaonesha kuwapo upungufu katika utekelezaji wa sheria na uratibu kati ya ngazi hizo, hali inayozua wasiwasi kuhusu utekelezaji kamili wa mfumo wa kisheria.
Ingawa Kifungu cha 147 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kinakataza kelele zinazozidi viwango vinavyoruhusiwa na marekebisho ya mwaka 2025 yaliimarisha mamlaka ya utekelezaji kwa Serikali za mitaa, uchunguzi unaonesha utekelezaji bado si wa kudumu.
Kutokana na hali hiyo, maeneo kama Sinza, Tabata, Ukonga na Kawe mkoani Dar es Salaam na baadhi ya maeneo mjini Morogoro na jijini Arusha yameendelea kuwa vitovu vya usumbufu wa kelele, mara nyingi bila hatua za kisheria kuchukuliwa licha ya wananchi kutoa malalamiko.
Pengo hilo katika utekelezaji linaonesha wasiwasi; licha ya kuwapo kwa sheria na kanuni, uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo bado ni miongoni mwa changamoto kubwa za kimazingira zinazoathiri afya ya umma na ustawi wa jamii katika maeneo mengi nchini.
Katika mitaa mingi, kelele zilizopitiliza zinaendelea kuvuruga maisha ya kila siku, zikichangia ukosefu wa usingizi, msongo wa mawazo na kupungua kwa uwezo wa kusikia.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa tatizo hilo halipungui. Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019, iliyochapishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), inaeleza kuwa, uchafuzi wa kelele unaongezeka kwa kasi katika maeneo ya mijini na unasababisha athari za kiafya kwa mwili na akili.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa, kelele kutoka kwenye usafiri, viwanda na maeneo ya burudani zinazidi kuwa changamoto kubwa ya kimazingira kadiri miji inavyoendelea kukua.
Licha ya hatua za utekelezaji zilizochukuliwa, ikiwamo NEMC kufunga baadhi ya maeneo katika wilaya za Kinondoni na Ubungo mwaka 2025, uzingatiaji wa sheria haujadumu.
Kutokana na hali hiyo, wakazi wengi wanaendelea kuvumilia kelele zilizopitiliza, hasa mwishoni mwa juma ambapo muziki mara nyingi huendelea hadi alfajiri.
Wasiwasi mitaani
Wakizungumza na Mwananchi, viongozi wa Serikali za mitaa wanasema kudhibiti uchafuzi wa kelele katika ngazi ya jamii kunazidi kuwa kazi ngumu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sinza C, Fredrick Kapufi, anasema wakazi wamekuwa wakilalamikia mara kwa mara muziki mkubwa kutoka maeneo ya burudani yaliyo jirani.
“Kama viongozi wa Serikali za mitaa tuliwaita wamiliki wa maeneo hayo na kufanya nao mazungumzo, pamoja na viongozi wa nyumba kumi wanaoishi karibu na majengo hayo,” anasema.
Anasema NEMC iliwahi kuingilia kati kutokana na malalamiko ya wakazi akieleza: “Baadhi ya wakazi walipeleka suala hilo moja kwa moja NEMC, iliyofika eneo husika na kulifunga kwa muda. Baada ya hapo kelele zilipungua kwa kipindi fulani.
“Anasema baadaye kulifanyika vikao vya ufuatiliaji kati ya viongozi wa eneo na wamiliki wa maeneo hayo, walioahidi kufunga mifumo ya kuzuia sauti isitoke nje.
“Walituhakikishia wataweka vifaa vya kisasa vya kupunguza kiwango cha kelele,” anasema Kapufi.
“Tulipowauliza kwa nini wanapiga muziki kwa sauti kubwa sana, baadhi yao walisema wateja wao ndio wanataka hivyo.”
Anasema baadaye viongozi wa nyumba kumi walikagua maeneo hayo ili kujiridhisha kama hatua za kupunguza kelele zilikuwa zimetekelezwa.
Kapufi anasema wakati mwingine utekelezaji wa sheria huwa mgumu kutokana na mtazamo mpana kuhusu ukuaji wa biashara jijini.
“Serikali inaposema Dar es Salaam ni jiji la biashara, inatuletea changamoto sisi viongozi wa ngazi za chini. Baadhi ya biashara zinaendeshwa kwa namna inayowaathiri wakazi wengine,” anasema.
Ingawa maeneo mengi ya burudani yanafanya biashara kihalali na hulipa kodi za halmashauri, Kapufi anasisitiza kuwa ni muhimu pia kuzingatia ustawi wa jamii.
“Biashara ni muhimu, lakini waendeshaji wanapaswa kuhakikisha kelele haziwasumbui watu wanaoishi jirani,” anasema.
Pia, anabainisha kuwa baadhi ya taasisi huanza shughuli bila kujitambulisha ipasavyo kwa mamlaka za eneo.
“Mashirika mengi yanaendesha shughuli katika maeneo yetu bila kujitambulisha hadi pale tunapokwenda kuyatafuta sisi wenyewe,” anasema.
Kiongozi wa eneo la Mtaa wa Kilakala wilayani Temeke, Idrisa Goja anasema usumbufu wa kelele katika eneo lake kwa kiasi kikubwa umedhibitiwa, ingawa bado hutokea mara chache.
“Tulizungumza na wamiliki wa maeneo hayo na kuwashauri wapunguze kiwango cha sauti,” anasema Goja akieleza kwa sasa kampeni za uhamasishaji zimepewa kipaumbele.
Kiongozi mmoja Kata ya Kivule, wilayani Ilala, ambaye hakutaka kutajwa jina anasema muziki mkubwa kutoka kwenye baa zinazofanya kazi hadi usiku wa manane bado ni tatizo kubwa.
“Kisheria, maeneo ya burudani yanapaswa kuwa na mifumo ya kuzuia sauti isitoke nje. Lakini baadhi yao hudai burudani yao inapaswa kusikika nje ili watu wengi zaidi waifurahie,” anasema akieleza kuwa, hali hiyo huwaathiri zaidi watu walio katika mazingira magumu, wakiwamo wagonjwa wanaohitaji utulivu ili wapone.
Katika Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kihonda Maghorofani mkoani Morogoro, viongozi wa Serikali za mitaa wanasema wamekuwa wakipokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi wanaodai kunyimwa haki ya kupumzika kutokana na kelele za usiku.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Gerrad Mawanja anasema walijaribu kufanya mazungumzo na baadhi ya wamiliki wa baa na kumbi za burudani ili wapunguze viwango vya sauti na kufunga mifumo ya kuzuia kelele kusambaa nje ya maeneo yao.
Anasema baadhi yao walikubali na kuahidi kufanya maboresho hayo, lakini baada ya muda walirejea katika tabia ileile ya kupiga muziki kwa sauti kubwa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kihonda Maghorofani, Libent Christopher anasema baadhi ya wafanyabiashara hutetea matumizi ya sauti kubwa wakidai ndiyo njia ya kuvutia wateja.
Hata hivyo, anasema haki ya kufanya biashara haiwezi kuwa sababu ya kuvunja sheria au kuathiri afya na ustawi wa wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo.
Mtazamo wa wadau
Mwanaharakati wa mazingira kutoka Arusha, Deus Mollel anasema tatizo la kelele nchini si la ukosefu wa sheria bali ni kushindwa kuzitekeleza kwa usawa na bila kuathiriwa na masilahi binafsi.
Anasema katika maeneo mengi wananchi wamekuwa wakitoa taarifa mara kwa mara kuhusu kumbi zinazopiga muziki kwa viwango vinavyozidi vile vinavyoruhusiwa, lakini hatua stahiki hazichukuliwi kwa wakati.
“Tatizo kubwa si sheria. Sheria ipo na inaelekeza wazi nini kifanyike. Changamoto ni pale wanaopaswa kusimamia sheria wanaposhindwa kuwajibika au wanaposhawishika kwa namna mbalimbali. Hapo ndipo wananchi wanabaki wakiteseka huku biashara zinazokiuka sheria zikiendelea kama kawaida,” anasema Mollel.
Mwanaharakati wa haki za jamii, Leah Kimaro anasema kukosekana kwa mifumo madhubuti ya kufuatilia malalamiko ya wananchi kunatoa mwanya wa vitendo vya rushwa na upendeleo kuendelea bila kugundulika.
Anasema wananchi wengi wamepoteza imani ya kuripoti ukiukwaji wa sheria kwa sababu mara nyingi hawapati mrejesho wa hatua zilizochukuliwa baada ya kutoa taarifa.
“Watu wanapolalamika kwa miezi au miaka bila kuona mabadiliko yoyote, huanza kuamini kuwa kuna watu wanaolindwa. Serikali inahitaji mfumo wa wazi unaoruhusu wananchi kufuatilia hatua zinazochukuliwa baada ya malalamiko yao kupokewa,” anasema Kimaro.
DJ Nazz kutoka Arusha anasema wamiliki wengi wa baa wana dhana potofu kuwa kadri muziki unavyokuwa mkubwa, ndivyo wanavyovutia wateja wengi na kupata faida kubwa.
“Watu wanaamini kadri muziki unavyokuwa mkubwa ndivyo burudani inavyokuwa nzuri, lakini ukweli ni kwamba unaweza kutoa burudani nzuri bila kuumiza wananchi,” anasema.
Anasema muziki unaweza kudhibitiwa kwa kutumia teknolojia za kisasa zenye uwezo wa kuelekeza sauti na mitetemo ndani ya jengo husika tu bila kuruhusu sauti hiyo kusambaa nje.
Suluhisho za kitaalamu
Mtaalamu wa uandaaji majukwaa na matukio, James Henry anasema tatizo hilo linahitaji suluhisho la kitaalamu na uratibu wa pamoja.
“Hata maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matamasha mara nyingi yako karibu na makazi ya watu,” anasema akibainisha kuwa mengi hayana mifumo madhubuti ya kuzuia sauti.
Anasema teknolojia kama spika zinazoelekeza sauti upande maalumu, paneli za kufyonza sauti na vifaa vya kidijitali vya kudhibiti kiwango cha sauti, vinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa kelele, lakini mara nyingi havitumiki kutokana na gharama au ukosefu wa utaalamu.
Mratibu wa matukio, Christopher Emmanuel anasema kuna haja ya kuboresha mipango na mafunzo.
“Waandaaji wachache sana hutoka nje ya eneo la tukio wakati wa majaribio ili kutathmini umbali ambao sauti inafika,” anasema.
Ushirikiano kitaasisi
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Novemba 2025, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa NEMC, Hamad Taimuru alisema changamoto za kudhibiti kelele zinachangiwa na udhaifu wa uratibu kati ya taasisi mbalimbali.
“Kama taasisi zote zingeshirikiana kwa karibu, suala hili lisingeachiwa NEMC pekee,” anasema.
Vilevile anasema maeneo mengi ya burudani hayana vifaa vya kupimia kiwango cha sauti akieleza: “Baa nyingi na maeneo ya burudani hayana vifaa vya kupima kiwango cha sauti.”
Taimuru anasema NEMC inaendelea kufanya kampeni za uhamasishaji na kushirikisha umma.
“Tunashirikiana mara kwa mara na waandishi wa habari pamoja na wananchi kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na uzingatiaji wa kanuni za kelele,” anasema.
Anasisitiza kuwa udhibiti wenye ufanisi unahitaji ushiriki wa kila upande.
“Kudhibiti uchafuzi wa kelele kunahitaji ushirikiano wa waandaaji, wasimamizi wa sheria na jamii,” anasema.
NEMC pia imezitaka mamlaka zote zenye dhamana kuimarisha uratibu na kuongeza juhudi za pamoja katika utekelezaji wa sheria, ikionya kuwa uchafuzi wa kelele unaendelea kuwaweka wananchi katika hatari kubwa za kiafya nchini.
Kwa mujibu wa NEMC, kuna mwongozo na hatua mbalimbali zilizowekwa kwa lengo la kuboresha udhibiti wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo.
Usikose sehemu ya mwisho ya habari hii ikionesha mbinu ambazo zikitumika ipasavyo zitamaliza tatizo hili.