Simba imeichapa Mlandege kwa mabao 3-0 katika Uwanja wa New Amaan ikiifuata Yanga kwenye fainali ya Kombe la Muungano.
Matokeo hayo yanatengeneza mchezo wa mapema wa Dabi ya Kariakoo ambao utapigwa Aprili 29, kisha timu hizo zitamalizana Mei 3, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Mabao ya ushindi kwa Simba yamelazimika kutokea benchi kwa wachezaji wake wawili walioingia dakika ya 60 mshambuliaji Selemani Mwalimu na winga Anicet Oura waliochukuw nafasi za Hassan Kibaila na Mohammed Bajaber.
Mwalimu ndiye aliyetangulia kuipa Simba bao katika dakika ya 63 kwa shuti akimalizia mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki wa Mlandege.
Bao hilo linakuwa la pili kwa Mwalimu kwenye mashindano ya Muungano akitangulia kufunga bao pekee kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Mafunzo.
Oura amepigilia msumari wa pili katika dakika ya 76 kwa shuti kali akimalizia pasi ya Clatous Chama ambaye naye alitokea benchi mwanzoni mwa kipindi cha pili, akichukua nafasi ya Morris Abraham.
Wakati mchezo ukielekea mwishoni Neo Maema ametupia wavuni bao la tatu akimalizia kwa ufundi asisti ya Elie Mpanzu.
Mlandege haikuwa vizuri katika kutengeneza mashambulizi makali ambapo nafasi kubwa kwenye mchezo huo ni ile waliyopata dakika ya 52 wakati mshambuliaji wake Omar Mdachi alipounasa mpira wakati kipa wa Simba, Hussein Abel akitaka kuokoa.
Simba imetengeneza nafasi nyingi za kufunga kwenye mchezo huo, lakini wachezaji wake Neo Maema, Elie Mpanzu wakashindwa kuzitumia.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kulipa kisasi cha mwaka 2025 ilipong’olewa na Mlandege kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Muungano.