KUMEKUWA na wimbi la waamuzi Zanzibar kushambuliwa na mashabiki wakati wa mechi, huku Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL) ikitaja sababu kuu inayochangia hali hiyo.
Akitoa ufafanuzi, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim Ali amesema wanajitahidi kuimarisha ulinzi lakini uwanja ambao wanachezea sio rafiki kwani hauna uzio ndio maana wanashindwa kuwadhibiti mashabiki wanapoingia sehemu ya kuchezea na kufanya vurugu.
“Changamoto ya uwanja kutokuwa na uzio hii inatuwia vigumu kuimarisha ulinzi kwani wanaolinda ni wachache na mashabiki ni wengi, hivyo ingekuwa na uzio yasingejitokeza mambo ya aina hiyo,” amesema kiongozi huyo.
Mtendaji huyo amesema ikitokea shabiki wa timu yoyote kumpiga mwamuzi, wanachukua sheria kwa mujibu wa kanuni za mashindano zinavyosema.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 3 ya mashindano 2024-2025, kumzuia mwamuzi kufanya kazi yake ni kosa na adhabu yake ni kumfungia aliyetenda kosa hilo awe shabiki, kiongozi au mtu yeyote kufika uwanjani kwa muda maalumu na kutozwa faini isiyopungua Sh500,000 na kuendelea.
Mtendaji huyo amesema ikiwa shabiki atatambulika, adhabu hiyo inakwenda moja kwa moja kwake na asipotambulika klabu ndiyo itakayobeba adhabu hiyo.
“Tumeshafanya utekelezaji wa hilo kwa kuwafungia mashabiki, viongozi na waamuzi wanaotenda makosa, ndiyo maana pamoja na uwanja kutokuwa na uzio matukio hayo yanatokea kwa uchache kwa kuwa tunafanya utekelezaji,” amesema.
Matukio ya aina hiyo yamewahi kujitokeza katika hatua ya mtoano wa kupanda Ligi Kuu (ZPL), mchezo uliozikutanisha Polisi na Kundemba, Mei 12, 2025 kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.
Mchezo huo ulimalizika kwa Polisi kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kupanda Ligi Kuu, lakini kulikuwa na hekaheka huku ngumi zikipigwa ambapo mashabiki wa Kundemba walihisi kuonewa na kutaka kumpiga mwamuzi jambo ambalo lilisababisha kutolewa uwanjani akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
Tukio lingine la aina hiyo lilitokea katika mchezo wa ZPL kati ya Muembe Makumbi na Kipanga, baada ya mwamuzi kumaliza mechi dakika ya 90, walitokea mashabiki wenye hasira kali kumvamia na kumpiga mwamuzi huyo sababu ikiwa ni kutoridhishwa na matokeo wakidai Kipanga wamebebwa.
Pia tukio kama hilo lilitokea kwenye mechi ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup) na mashabiki wa KVZ walianzisha vurugu wakati timu hiyo ilipocheza na Uhamiaji kwa kutaka kumpiga mwamuzi wa kati. KVZ ilitozwa faini ya Sh3 milioni.
Bodi ya Ligi imewahi kuipiga faini ya Sh1 milioni timu ya Negro inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa kosa la mashabiki wake kumpiga mwamuzi Ramadhan Kesi kwenye mechi kati ya timu hiyo dhidi ya Raskazone.
Timu ya Mwembe Makumbi ilifungiwa kutoingiza mashabiki wake katika michezo minne mfululizo na kutozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la kufanya vurugu wakati wa mechi na kulipa gharama za uharibifu wa miundombinu ya uwanja, fujo hizo zilitokea walipocheza na KVZ.
Kamati ya Uendeshaji ilimfungia Kocha Msaidizi wa KVZ, Hassan Makame Ameir kwa kutokaa benchi la ufundi kwa miezi mitatu na faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumsukuma mwamuzi msaidizi wakati wa vurugu.
Halikadhalika, Bodi ya Ligi iliwatoza faini Muembe Makumbi ya Sh500,000 kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuimba nyimbo zisizokuwa na maadili dhidi ya mwamuzi.
Pia, bodi hiyo iliitoza faini ya Sh1 milioni Black Sailors inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza Unguja kwa kosa la mashabiki wa timu hiyo kufanya vurugu.