
Dodoma. Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imesema michezo ya kubahatisha inalenga burudani na starehe pekee, ikionya kuwa si ajira wala njia sahihi ya kujipatia kipato.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, James Mbalwe, wakati wa semina kwa kamati ya ulinzi ya Mkoa wa Dodoma.
Mbalwe amesema michezo hiyo ni halali kwa mujibu wa sheria na ina mchango mkubwa kwa serikali, ikibainisha kuwa mwaka 2020/21 ilichangia Sh131.9 bilioni na kuongezeka hadi Sh260.2 bilioni mwaka 2024/25.
Hata hivyo, amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ikiwemo uwepo wa waendeshaji wasio waaminifu wanaoendesha michezo bila vibali, jambo linalochangia taswira hasi kwa jamii.
“Bodi huwa inafanya ukaguzi wa mara kwa mara na pale itakapobainika ukiukwaji wa sheria, hatua kali za kisheria huchukuliwa,” amesema Mbalwe.
Ameongeza kuwa pamoja na kuchangia mapato ya serikali, sekta hiyo imeajiri takribani watu 30,000 wanaoendesha maisha yao kupitia shughuli halali za michezo ya kubahatisha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Bodi hiyo, Daniel Olesumayan, amesema michezo ya kubahatisha ipo katika aina mbili ya kibiashara na ile ya matangazo kwa ajili ya kuvutia wateja.
Amesisitiza kuwa michezo hiyo si tatizo endapo itatumika kwa lengo la burudani na kwa kiwango kinachofaa, akionya kuwa inakuwa hatari inapochukuliwa kama ajira.
“Michezo hii si mibaya kama mtu anacheza kwa kujifurahisha na si kwa matarajio ya kupata kipato,” amesema Olesumayan.
Amebainisha kuwa waendeshaji wote wanapaswa kuwa na leseni halali, huku akisisitiza kuwa ni marufuku kuwahusisha watoto chini ya miaka 18 katika michezo hiyo na kwamba hatua kali huchukuliwa dhidi ya wanaokiuka taratibu.
Aidha, amesema michezo hiyo hairuhusiwi kufanyika karibu na nyumba za ibada, shule, vyombo vya usalama na maeneo yasiyofikika kirahisi kwa ukaguzi.
Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama wa Mkoa wa Dodoma wameeleza wasiwasi wao kuhusu athari za michezo hiyo, ikiwemo uraibu, uvivu na mmomonyoko wa maadili kwa vijana.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Sophia Kizigo, amesema vijana wengi wameathirika na michezo hiyo na kushindwa kujishughulisha na kazi za uzalishaji, hususan katika msimu wa kilimo.
“Vijana wengi hawataki kufanya kazi, wanategemea mikeka yao itiki. Hii imeathiri hata shughuli za kilimo vijijini,” amesema Kizigo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema pamoja na uhalali wake, michezo hiyo imechangia kuvunjika kwa ndoa kutokana na baadhi ya watu kutowajibika.
“Tuna kesi nyingi za ndoa kuvunjika kutokana na michezo hii. Elimu zaidi inahitajika na ikiwezekana kuwe na mipaka ya kucheza,” amesema Shekimweri.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Khatibu Kazungu, ameitaka GBT kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma ili kupunguza athari za uraibu, hususan kwa vijana.
“Elimu itolewe kwa vijana kucheza kwa kiasi ili kuokoa familia zilizoathirika na utegemezi wa michezo ya kubahatisha,” amesema Dk Kazungu.