Arusha. Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimesema kitatumia mkutano wake mkuu wa mwaka huu kujadili kwa kina wajibu na mchango wa wanasheria katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, ikiwa ni sehemu ya wadau muhimu katika maendeleo ya nchi.

Kuanzia leo, Jumatatu, Aprili 27, 2026, mawakili 500 wameanza semina na mijadala ya kitaaluma itakayohitimishwa na mkutano mkuu Alhamisi.

Akizungumza jijini Arusha leo, Meneja wa Programu wa TLS, Kefar Mbogela, amesema wiki ya mkutano mkuu imeanza ikiambatana na semina mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo mawakili pamoja na kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu.

Kwa mujibu wa Mbogela, kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuangazia nafasi ya mwanasheria katika kuelekea Dira ya Taifa 2050, ambapo TLS inalenga kutazama kwa upana namna wanasheria wanavyoweza kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Tunaenda kutazama kwa ukubwa wake namna gani wanasheria tunaweza kuchangia ili kufikia dira hiyo, kama sehemu ya wadau kwenye mnyororo wa haki,” amesema.

“Hii ni wiki ya TLS, tuko Arusha kwa ajili ya mkutano mkuu. Tumeanza na semina mbalimbali zitakazoendelea hadi Jumatano, ambapo mawakili wanapata nafasi ya kujiongezea maarifa na kubadilishana uzoefu,” amesema Mbogela.

Amesema mkutano mkuu utafanyika Alhamisi, ukitarajiwa kufunguliwa na Jaji Mkuu, George Masaju, na utaambatana na shughuli nyingine, zikiwemo vikao vya kikanda vya mawakili.

Ameongeza kuwa, mbali na mawakili, semina hizo pia zimewashirikisha wadau kutoka kada nyingine kutokana na umuhimu wa mada zinazojadiliwa kuwa na manufaa mapana zaidi kwa jamii.

Miongoni mwa mada zinazowasilishwa ni pamoja na maadili ya uwakili, ubobezi wa kisheria, namna ya kusawazisha maisha ya kazi na binafsi, afya ya akili pamoja na mbinu za uwekezaji kwa mawakili ili kuwaongezea ufanisi wa maisha nje ya taaluma yao.

“Kwa mfano, leo tunajadili kuhusu maadili kwa mawakili, zingine zitahusu ubobezi wa kisheria na masuala ya uwekezaji,” amesema.

Amesema mawakili 500 wanashiriki katika shughuli hizo, ambazo pia zinahusisha utoaji wa elimu ya msaada wa kisheria kupitia matawi 21 ya TLS nchini, ikiwa ni sehemu ya mchango wa chama hicho katika maendeleo ya jamii.

Mmoja wa washiriki, Wakili Triza Mponzi, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwaongezea uelewa na kuwajengea uwezo mawakili, hasa katika kuwahudumia wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Semina hizi zinatuendeleza na kutukutanisha na wabobezi wa masuala ya kisheria, na pia zitatusaidia kutujenga sisi na kusaidia wananchi pale wanapohitaji msaada wa kisheria,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *