
Geita. Wananchi mkoani Geita wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho ya wahandisi, makandarasi na watengenezaji wa mitambo ya uchimbaji madini yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho vya Dk Samia Suluhu Hassan, Manispaa ya Geita.
Imeelezwa kuwa maonesho hayo yanalengo la kuwaiongezea uelewa wa matumizi ya teknolojia katika shughuli za kiuchumi.
Maonesho hayo yanayofanyika kwa mara ya tatu mkoani Geita, yalianza Aprili 24, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Mei 3, 2026, yakiwa na lengo la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu matumizi ya vifaa vya kisasa katika uchimbaji visima, madini na kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Aprili 28, 2026, katika viwanja hivyo, Ofisa wa Wizara ya Viwanda na Biashara kutoka Idara ya Maendeleo ya Viwanda, Anet Ngowi amesema maonesho hayo yanalenga kukuza uchumi wa nchi kupitia ushindani wa kibiashara.
Hata hivyo, amesema mwitikio wa wananchi bado ni mdogo kutokana na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya umeme kwa takribani siku tano tangu kuanza kwa maonesho hayo, hali iliyolalamikiwa pia na wafanyabiashara walioshiriki.
“Tunaiomba Tanesco iangalie namna ya kuwasaidia wajasiriamali wetu. Lengo ni kuwainua, siyo kuwakatisha tamaa. Endapo changamoto hizi zitaendelea, washiriki wanaweza kukosa hamasa ya kushiriki maonesho yajayo,” amesema Ngowi.
Ameongeza kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonesho hayo kesho Jumatano, Aprili 29, 2026 na kuwataka wananchi na wajasiriamali kujitokeza kwa wingi.
Kuhusu changamoto ya umeme, imeelezwa kuwa inatokana na baadhi ya makampuni yaliyoshiriki maonesho ya mwaka jana kushindwa kulipia gharama za umeme, hali iliyosababisha kuchelewa kwa huduma hiyo mwaka huu.
Hata hivyo, huduma hiyo imeanza kupatikana leo baada ya juhudi za waandaaji. Mratibu wa maonesho hayo kutoka Kampuni ya MAT Builders and Contractors Limited Global, Menard Mwata, amesema zaidi ya kampuni 40 na wajasiriamali zaidi ya 30 kutoka ndani na nje ya nchi wanashiriki katika maonesho hayo.
Amewataka wananchi, hasa wachimbaji kutumia fursa hiyo kujifunza teknolojia mpya zitakazowawezesha kuongeza tija katika shughuli zao.
“Tunatoa elimu kwa vitendo. Wahandisi wanatoa ushauri wa moja kwa moja kwa wachimbaji na wamiliki wa makampuni. Hii ni nafasi ya kipekee kujifunza bila gharama,” amesema Mwata.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wazazi na vijana kuchangamkia fursa za masomo katika vyuo vya ufundi stadi (VETA), akieleza kuwa ukuaji wa sekta ya madini unahitaji wataalamu wenye ujuzi wa kisasa.
Kwa upande wake, Mhandisi Paul Haruna kutoka Kampuni ya Pawa Mwanza Africa, amesema maonesho hayo yamekuja wakati muafaka, yakitoa fursa kwa jamii kujifunza kazi za kihandisi pamoja na kuwahamasisha vijana wanaotamani kuingia katika taaluma hiyo.