Mbeya. Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Mkoa wa Mbeya, linatarajia kufanya kikao cha ndani cha siku mbili kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni siku chache baada ya chama hicho Kanda ya Nyasa kuzindua ofisi na kurejea rasmi katika shughuli za kisiasa.

Kikao hicho kinachotarajiwa kuwashirikisha wajumbe takribani 30, kitafanyika Mei Mosi na 2, 2026 na baada ya mijadala ya ndani, wanatarajia kufanya mkutano maalumu wa wanachama kwa ajili ya kuwasilisha maazimio yatakayofikiwa.

Aprili 18, 2026, Chama hicho Kanda ya Nyasa kilizindua ofisi zake na kupandisha bendera, hatua iliyoashiria kurejea kwa shughuli zake za kisiasa baada ya kuruhusiwa na Mahakama Kuu kufuatia kusimamishwa kwa takribani mwaka mmoja kutokana na kesi iliyohusu mgawanyo wa mali za chama.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 29, 2026, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Chonya Elisha amesema kikao hicho kinalenga kujadili masuala muhimu ya chama katika ngazi ya mkoa.

Amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kupokea na kuchambua utekelezaji wa maagizo ya Kamati Kuu ya chama Taifa, kutathmini hali ya kisiasa katika Mkoa wa Mbeya, pamoja na kuandaa mpango kazi wa shughuli za kisiasa.

“Pia, Mei Mosi tutajadili mfumo shirikishi wa jamii katika masuala ya haki na Katiba kwa wananchi. Tunatambua kuwa tumepoteza muda mwingi, hivyo ni muhimu kurejea kwa nguvu mpya,” amesema Elisha.

Ameongeza kuwa kikao hicho kitahusisha wajumbe kutoka majimbo saba pamoja na wilaya zinazounda Mkoa wa Mbeya, zikiwamo Rungwe na Mbeya na kwamba, Mei 2 watakamilisha kwa kufanya mkutano maalumu wa wanachama.

Elisha amesema kipindi ambacho chama hicho kilikuwa kimesimamishwa kimewapa fursa ya kujipanga upya, na kuwaomba wananchi kuwa tayari kukipokea tena chama hicho katika kuendeleza harakati za kisiasa.

“Sisi ni kimbilio la wananchi. Tunawaomba wawe tayari kukipokea chama chao ili kuendelea kutetea na kudai haki zao pamoja na kulijenga Taifa. Tumejipanga kuanzia ngazi za chini hadi Taifa,” amesema.

Kwa upande wake, mmoja wa wafuasi wa chama hicho, Charles Msombe amesema kwa muda mrefu walikosa fursa ya kufanya shughuli za kisiasa, lakini sasa wako tayari kuendelea pale walipoishia.

“Kilichotokea kilikuwa ni changamoto, lakini bado tuko imara. Tunarejea kuendeleza harakati zetu na tunachohitaji ni haki kwa wananchi,” amesema Msombe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *