Njombe. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuwaongoza Watanzania katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu, zitakazofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa leo Jumatano, Aprili 29, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Mtaka amesema mkoa huo umejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mapokezi ya mgeni huyo pamoja na wageni wengine, kwa kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa katika maeneo yote ili sherehe hizo zifanyike kwa amani na utulivu.
Mtaka amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika uwanja mpya wa mkoa uliopo katika eneo la Halmashauri ya Mji wa Njombe, ambao umeandaliwa mahsusi kwa ajili ya tukio hilo.
“Tunayo heshima kubwa kuwataarifu Watanzania kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,” amesema Mtaka.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, katika ofisi za Mkoa wa Njombe.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: ‘Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.’
Kwa mujibu wa Mtaka, Mkoa wa Njombe umejipanga kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa viwango vya juu ili kuendana na hadhi ya tukio hilo la kitaifa litakaloongozwa na kiongozi mkuu wa nchi.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema jukumu la shirikisho hilo ni kuwahamasisha wafanyakazi kuongeza bidii kazini ili kukuza uzalishaji, hali itakayowapa uhalali wa kudai haki zao.
Amesema katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano kati ya wafanyakazi na serikali umeimarika, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mishahara ya watumishi wa umma imeongezwa, jambo ambalo halikuwa la kawaida hapo awali.
“Hata hivyo, kwa mwaka huu, nini kitajiri tutasubiri kusikia kutoka kwa Rais. Tunatarajia majibu na mwelekeo zaidi yatatolewa Mei Mosi,” amesema Nyamhokya.