Nachingwea. Mkimbiza mwenge wa uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda ametoa mwezi mmoja kwa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa mazingira, Masasi_Nachingwea (Manawasa) kukamilisha kwa mradi wa maji wa Mkumba, nasio kusubiri hadi Agosti ambapo ndio makubaliano ya mkataba.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi leo Alhamisi, Aprili 30, 2026 mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwang’onda amesema kuwa wananchi hao wamekuwa wakipata changamoto ya kwenda umbali mrefu kutafuta maji na kuwataka Manawasa kuhakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja mradi uwe umekamilika.

“Natoa mwezi mmoja kwa Manawasa kuhakikisha kuwa mnakamilisha mradi huu ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma bora ya maji bila kusua sua.”amesema Wang’onda.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Manawasa, Mhandisi Aneth Mwawenya amesema kuwa mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 65 na utanufaisha wakazi 28 elfu napia mradi huo unauwezo wa kuzalisha lita milioni tano kwasiku ambapo kwasasa wanazalisha maji lita milioni mbili kwasiku.

Mhandisi Aneth ameendelea kusema kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu Sh3 bilioni ambpo fedha hizo zimetolewa kutoka Serikali kuu kupitia Wizara ya maji.

“Huu mradi ulianza tangu Agust 13, 2025 na unatarajia kukamilika Agust 12,2026 lakini tutajitahidi kukamilisha mradi huu ndani ya mwezi kama alivyosema kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru  Kitaifa. .”amesema Mhandisi Mwawenya.

Hata hivyo Mhandisi Aneth ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo wa maji  Mkumba kutaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwani kwa sasa maji yanazalishwa lita milioni 2 kwa  siku hivyo itafikia  lita milioni 5 kwa siku katika mji wa Nachingwea.

“Upatikanaji wa maji utaongezeka sana kwasababu sasahivi maji yanapatikana kwa siku lita milioni mbili wakati mradi huu ukishakamilika maji yatakuwa yanapatikana lita milioni tano napia hata kwenye mgawo wa maji utaongezeka kutoka saa nane ya sasa hadi kufikia saa 16.” amesema pia.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda wakati akizindua mradi wa maji katika kijiji cha Mkumba wilayani Nachingwea. Picha na Bahati Mwatesa

Naye Mwananchi kutoka Nachingwea Kuruthum Lunje amesema kumalizika kwa mradi huo utasaidia wananchi hao kuondokana na shida ya maji kwani muda mwingi walikuwa wanakwenda kutafuta maji na kukosa muda wa kufanya shughuli za kijamii

“Tulikuwa tunatembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye visima vya asili,na huko njiani tulikuwa tunakutana na changamoto ya wanyama wakali,kuibiwa kwa baiskeli zetu ambazo tulikuwa tunatumia kubebea maji,mradi huu ukimalizika utakuwa umemaliza changamoto zote za maji hapa Wilayani kwetu.”amesema Lunje.

Naye Mohamed Milanzi amesema kuwa mradi wa maji utakapo kamilika utakuwa umemaliza changamoto ya maji katika eneo lao kwani walikuwa wanatembea umbali wa km 6 kutafuta maji kwenye visima vya asili.

Tulikuwa tunatembea umbali wa km 6 kutafuta maji katika visima vya asili na wakati mwingine tunakutana na wanyama wakali ,wezi ambao walikuwa wanatupora baiskeli zetu ambazo tulikuwa tunatumia kubeba maji,tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwaajili ya wananchi wa Nachingwea.”amesema Milanzi.

Miradi saba yenye thamani ya Sh4 bilioni imetembelewa kuonwa, kuwekwa mawe ya msingi na mbio za mwenge wa uhuru, wilayani Nachingwea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *