Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza Jeshi la Polisi kote nchini kuziachia pikipiki wanazozishikilia ambazo hazina makosa makubwa ili wahusika waendelee kuzitumia kwa ajili ya kutafuta faini wanazodaiwa.

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesisitiza pikipiki zote ambazo zimekamatwa kwa kuhusishwa na makosa makubwa ikiwemo ubakaji, unyang’anyi, kubeba madawa na matumizi ya silaha kwamba zisitolewe hadi uchunguzi utakapokamilika.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 30, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani.

Katika swali lake la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Cherehani kumekuwa na changamoto kubwa kwa wananchi kukamatiwa pikipiki zao kwa makosa ambayo ni madogo hasa vijana wanaotoka vijijini ambapo amesema vituo vya Polisi nchini pikipiki zimelundikwa na nyingi zinachakaa lakini akaomba bunge kupitia upya faini kwa vyombo hivyo.

Waziri Mkuu amekiri kuwepo kwa mlundikano wa pikipiki kwa vituo vingi ambako baadhi zimekamatwa kwa makosa madogo yasiyotakiwa kuendelea kuzishikilia lakini kwa sababu zisizoeleweka zinaendelea kushikiliwa.

“Mheshimiwa Spika, ni kweli baadhi ya maeneo kumekuwepo na mlundikano wa pikipiki ambazo zimekamatwa kwa makosa mbalimbali, zipo ambazo zimekamatwa kwa makosa makubwa mfano wa kuvunja, wizi wa kutumia silaha au kubeba uhalifu, ubakaji na uuwaji,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema zilizokamatwa kwa makosa makubwa zitaendelea kuwekwa maeneo hayo kwa ajili ya kukamilisha ushahidi lakini kwenye makosa madogo wahusika wapewe vyombo vyao ili waendelee kuvitumia kutafuta hizo faini.

“Naagiza mahali popote ambapo vyombo hivyo vimekamatwa kama havijafanya makosa makubwa niliyoyataja hapo juu, wahusika waruhusiwe kuchukua pikipiki na bajaji zao ili waendelee kutafuta fedha wakalipe hizo faini,” amesema Dk Mwigulu.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, hakuna sababu ya kuendelea kushikilia chombo cha mtu wakati Watanzania siku hizi wanavyo vitambulisho vya Nida lakini vyombo wanavyovitumia vimesajiliwa hivyo hawawezi kukimbia madeni.

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesisitiza wahusika wasitumie agizo lake kama kivuli cha kujificha badala yake waendelee kuchukua hatua kwa ajili ya usalama wao na vyombo wanavyovitumia ili kuepuka usumbufu.

Akijibu swali la Mbunge wa Ngara (CCM), Dotto Bahemu kuhusu Polisi kuchelewa kufanya uchunguzi na hivyo kuwanyima haki zao watuhumiwa, Waziri Mkuu amesema Tume ya Haki Jinai ilishatoa mwongozo ikiwemo kutomshtaki mtu kama upelelezi haujakamilika na inapotakiwa upelelezi unapaswa kukamilika ndani ya siku 90.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *