
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli limewakamata watuhumiwa 40 wanaodaiwa kujihusisha na wizi wa miundombinu ya reli, hususani katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kufuatia operesheni iliyofanyika katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Alhamisi, April 30, 2026 Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli Tanzania, Matride Kuyeto amesema operesheni hiyo ilifanyika kuanzia Machi 18 hadi Aprili 18, 2026, ikiwa na lengo la kudhibiti na kusaka wahusika wa uhalifu unaolenga miundombinu ya reli.
“Katika msako huo, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vifaa mbalimbali vinavyodaiwa kuibwa kutoka kwenye mradi wa SGR,” amesema Kamanda Kuyeto.
Amesema vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na nondo 431, mabomba 458 ya chuma ya madaraja, waya za uzio bando tano zenye urefu wa mita 60 kila moja, mabati 23, stendi tatu zilizotengenezwa kwa kutumia mabomba ya mradi wa SGR.
Vifaa vingine ni sahani za chuma tano na mafuta ya dizeli lita 40 na vyombo vilivyotumika kusafirisha vifaa hivyo, vikiwemo magari matatu na pikipiki sita.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema Aprili 6, 2026, mkoani Morogoro, mtuhumiwa mmoja alikamatwa kwa kosa la kughushi tiketi za usafiri wa treni ya SGR.
Amesema hatua za kisheria zinaendelea dhidi ya watuhumiwa wote waliokamatwa ili wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kikosi hicho kimewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kulinda miundombinu ya reli na miradi mingine ya kimkakati nchini.
“Tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote wanaojihusisha na uhalifu huu pamoja na wale wanaohujumu miradi ya maendeleo,” amesema.
Mbali na jukumu la kulinda usalama, amesema kikosi hicho pia kinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo na kufuata sheria wanapotumia huduma za treni.
Kuhusu usalama wa mali za abiria, Kamanda Kuyeto amesema ndani ya treni zote kuna askari wanaosimamia usalama wa abiria na amewataka wananchi kutoa taarifa mara moja endapo watabaini viashiria vya uhalifu.
“Tunawahakikishia wananchi kuwa safari za treni ni salama na tunawahimiza kutoa ushirikiano kwa askari waliopo ndani ya treni ili kuhakikisha usalama unaendelea kuimarika,” amesema.