Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imemhukumu adhabu ya kunyongwa mpaka kufa mfanyabiashara Abdallah Miraji Mussa, maarufu kama Mr Blue, kwa kosa la kumuua mpenzi wake kisha kumkataka viungo vya mwili na kwenda kuvitupa maeneo tofautofauti.
Mr Bluu alishtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya mpenzi wake Ezenia Kamana, Agosti 19, 2024, eneo la Chang’ombe Maghorofani, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Alipohojiwa na polisi mara ya pili, maelezo ya ungamo kwa Mlinzi wa Amani (Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo) Mr Blue alikiri kumuua mpenzi, lakini mahakamani alikana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ezenia, kumuua wala kutoa maelezo ya kukiri kosa hilo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa jana Jumatano, Aprili 29, 2026 na Jaji Awamu Mbagwa aliyesikiliza kesi hiyo, imemtia hatiani kwa kosa hilo na kumhukumu adhabu ya kunyongwa mpaka kufa, kwa kuzingatia ushahidi wa kimazingira.
“Mshtakiwa, kosa ulilotiwa nalo hatiani lina adhabu moja tu, kunyongwa mpaka kufa. Kwa mantiki hiyo ninakupa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa vifungu namba 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu,” amesema Jaji Mbagwa.
Pia, Jaji Mbagwa ameamuru gari ambalo mauaji yalifanyika humo litaifishwe na kuwa mali ya Serikali, kwa mujibu wa kifungu cha 351(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ni kifaa kilichosaidia kutekeleza mauaji hayo.
Abdallah Miraji Mussa maarufu Mr Blue mwenye jezi ya rangi ya Bluu, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mpenzi wake Ezenia Kamana kiaha akaukatakata mwili wake vipande vidogovidogo akavifunga viungo kwenye mifuko minane na kwenda kuvitupa maeneo tofautitofauti
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Mr Blue na Ezenia walikuwa wapenzi kwa miaka minne na Mr Blue alikuwa akimtembelea mpenzi wake huyo nyumbani kwake Tandika Maghorofani.
Siku ya tukio Agosti 19, 2024, Ezenia aliondoka kwenda kununua viti vya plastiki kwa ajili ya mgahawa wake na kwamba aliondoka na mpenzi wake Mr Blue kwenye gari yake.
Hata hivyo, walitofautiana katika kauli baada ya Ezenia kumuomba Mr Blue Sh100,000 na kutokana na kukasirishwa na maneno ya mpenzi wake huyo, Mr Blue alichukua kisu kilichokuwa ndani ya gari akamchoma mpaka akafariki dunia.
Kisha aliondoka na mwili wa mpenzi wake huyo akaenda nao nyumbani kwake Sinza, ambako aliukatakata akautenganisha viungo akavifunga katika mifuko ya salfeti na kwenda kuvitupa maeneo mbalimbali.
Baada ya Ezenia kuchelewa kurudi na mama na ndugu zake wakampigia simu bila mafanikio, kaka wa Ezenia, Livingstone Stanley Kamana alimpigia simu Mr Blue kumuulizia kama alikuwa na Ezenia, lakini Mr Blue akasema kuwa walikuwa hawajaonana.
Kesho yake Agosti 20, 2024 Mr Blue alikwenda nyumbani kwa kwa mpenzi wake akaeleza kuwa, jana yake kweli alimchukua Ezenia, lakini alishuka Mwembeyanga baada ya kutofautiana.
Hivyo wote yeye Mr Blue na kaka wa Ezenia; Livingstone walikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Chang’ombe walikofanyiwa mahojiano, lakini wakati wa mahojiano hayo Mr Blue alikuwa na wasiwasi, hivyo akawekwa chini ya ulinzi wakati upelelezi unaendelea.
Agosti 22, Mkuu wa upelelezi Wilaya (OC-CID) Kawe, Mrakibu wa Polisi, Joram Magova alipokea taarifa kupatikana viungo vya binadamu eneo la Kunduchi ambako walikwenda wakakuta mifuko minne ya salfeti ikiwa na viungo mbalimbali vya binadamu.
Magova alivichukua viungo hivyo na kuvipeleka Hospitali ya Mwananyamala kisha alituma taatifa hizo kwenye kundi la WhatsApp la maofisa wa Polisi.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Temeke, Kim aliwasiliana na Magova, akaenda na ndugu wa Ezenia katika Hospitali ya Mwanyamala ambako walikutana na Magova na watoa taarifa hao walivitambua baadhi ya viungo hivyo kuwa ni vya ndugu yao kutokana na baadhi ya alama.
Mr Blue alipohojiwa mara ya pili alikiri kumuua mpenzi wake huyo; Ezenia na polisi walifanya upekuzi chumbani kwake wakapata kisu na panga vilivyotumika kutekeleza mauaji hayo.
Mtuhumiwa alikwenda kuwaonesha polisi mahali alikomuulia, alikomkatia viungo na alikokwenda kutupa viungo hivyo, yaani Kunduchi karibu na Hotel ya Silver Sand, Tegeta Block D na Ununio.
Agosti 24, mtuhumiwa huyo aliandikwa maelezo mbele ya kaka yake Mussa Miraji Mussa na kukili alimuua Ezenia na pia akakiri mbele ya Mlinzi wa Amani.
Matokeo ya uchunguzi wa vinasaba uliofanywa na Mkemia wa Serikali yalionesha kuwa mpangilio wa vinasaba kutoka katika sampuli za mwili wa marehemu ulioana na mpangilio wa vinasaba kutoka sampuli za mtoto wa marehemu na za kutoka katika panga na kisu vilivyotumika katika mauaji hayo.
Utetezi wa mstakiwa
Katika utetezi wake Mr Blue alidai kuwa, alimjua Ezenia tangu mwaka 2023 na alikuwa mteja wake wa mikoba ya wanawake, lakini akakana kuwa na uhusiano wala kumuua.
Alidai kuwa maelezo yake ya onyo aliyoyatoa polisi akikiri kumuua Ezenia aliyatoa baada ya kuteswa huku akikana kuandika maelezo ya ungamo (maelezo ya kukiri kosa) kwa Mlinzi wa Amani (Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo) wala kupelekwa kwake.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Mbagwa amesema kuwa, ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kumshuhudia mshtakiwa akimuua Ezenia isipokuwa ushahidi wa kimazingira tu, ambao kisheria unakubalika katika kumtia mshtakiwa hatiani.
Akichambua ushahidi huo wa kimazingira, Jaji Mbagwa amesema kuwa kwanza ni ushahidi kuwa mshtakiwa ndiye mtu wa mwisho kuonekana na Ezenia, ambao hakuukanusha wala hakueleza mazingira ya kifo chake.
Mbili, Jaji Mbagwa amesema kuwa matendo ya mshtakiwa ambayo yanaleta walakini na kwamba yanakinzana na mtu asiye na hatia.
Akichambua matendo hayo Jaji Mbagwa amesema kuwa, kwanza ni mshtakiwa, awali kukana kukutana na Ezenia, siku ya tukio, Agosti 19,2024, lakini baadaye kesho yake alikiri kumchukua kwenye gari lake na kwamba baadaye alimshusha Mwembeyanga baada ya kuhitilafiana.
Lakini, pia Jaji Mbagwa amesema mshtakiwa huyo alikiri na akawaongoza askari kupata viungo vya mwili wa marehemu katika maeneo mbalimbali kama ilivyoelezwa na mashahidi mbalimbali.
Jaji Mbagwa amesema uhusika wa mshtakiwa unakolezwa na shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka, Miraji Omari Miraji, ambayeni ni mtoto wa kaka wa mshtakiwa.
Amesema kuwa shahidi huyo alieleza kuwa mshtakiwa alimtuma kwenda kumnunulia mifuko ya salfeti, ushahidi ambao ukizingatiwa na ushahidi mwingine wa viungo vya marehemu kupatikana kwenye mifuko ya salfeti unathibitisha uhusika wa mshtakiwa na mshtakiwa hakuweza kutikisa ushahidi wake huu.
“Upande wa mashtaka walileta ushahidi wa ungamo (kukiri kutenda kosa mbele ya Mlinzi wa Amani). Ingawa mshtakiwa alikana lakini (ungamo hilo) nimetafakari madai ya mshtakiwa nikaona ni mambo ya kufikirika na ni uwongo,” amesema Jaji Mbagwa.
Amefafanua kuwa, wakati shahidi wa 23 wa upande wa mashtaka anatoa ushahidi wake (kuhusu ungamo la mshtakiwa) Wakili Majaliwa Mohamed Majaliwa, aliyemtetea mahtakiwa, aliupinga kwa vigezo vya kisheria tu kuwa hauoneshi (maelezo hayo) muda wa kuandikwa wala saini ya mshtakiwa.
Jaji Mbagwa amesema kuwa wakili Majaliwa hakusema kama mshtakiwa anakana kutoa maelezo hayo, Mahakama ingeendesha kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi (kujiridhisha kama mshtakiwa alitoa au hakutoa) maelezo hayo ya ungamo.
Hivyo, Jaji Mbagwa amesema kuwa madai yake (mshtakiwa) kuwa hakuandika maelezo hayo kuyaleta wakati upande wa mashtaka ulishafunga ushahidi wake, hayawezi kuzingatiwa.
“Baada ya kuzingatia ushahidi wote japo ni wa kimazingira, unathibitisha kuwa mshtakiwa alimuua marehemu Ezenia Kamana,” amesema Jaji Kamana na kusisitiza:
“Kwa mantiki hiyo ninakuona mshtakiwa Abdallah Miraji Mussa una hatia na ninakutia hatiani kwa kosa la kumuua Ezenia Kamana kinyume na kifungu cha 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.”