
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York hii leo Guterres amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuzuiwa kwa uhuru wa usafiri katika eneo la Mlango bahari wa Hormuz, jambo linalochelewesha usafirishaji wa mafuta, gesi, mbolea na bidhaa nyingine muhimu, na hivyo kuvuruga masoko ya nishati, usafiri, viwanda na chakula duniani.
Uchumi wa dunia kuporomokoa
Guterres ameeleza kuwa hali hiyo inaweza kushusha ukuaji wa uchumi wa dunia kutoka asilimia 3.4 hadi 3.1 hata katika hali bora, huku mfumuko wa bei ukiongezeka na biashara ya kimataifa kupungua, na katika hali mbaya zaidi kusababisha ongezeko la umaskini kwa watu milioni 32 na njaa kali kwa watu milioni 45 zaidi.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ameonya kuwa kadri hali inavyoendelea, ndivyo gharama kwa ubinadamu zinavyoongezeka, akisisitiza kuwa nchi zinazoendelea zitaathirika zaidi kutokana na madeni makubwa na kupotea kwa ajira.
Amewataka wahusika wote kurejesha mara moja uhuru wa usafiri kama ilivyoainishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio 2817, kufungua mlango huo muhimu na kuhakikisha usalama wa meli ili kuruhusu uchumi wa dunia kuimarika tena, huku akihimiza pia kuepuka vitendo vinavyoweza kudhoofisha usitishaji mapigano na kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kudumu ya amani.
Hali ikoje katika upande wa nishati?
Mvutano unaoendelea wa usafirishaji katika mlango baharí wa Hormuz unaendelea kuzidisha mshtuko wa nishati duniani.
Kwa mujibu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa ajili ya Ulaya UNECE, bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imefikia takribani dola 118, na kuongeza hofu ya upungufu wa mafuta, gesi na rasilimali nyingine muhimu.
Dario Liguti ambaye ni Mkurugenzi wa Nishati Endelevu wa UNECE ameiambia idhaa ya kiingereza ya Umoja wa Mataiafa kuwa mataifa ya Asia ya Kusini na Kusini Mashariki ndiyo yaliyoathirika kwanza na mgogoro huu mkubwa wa nishati, lakini athari zake zinaendelea kuenea, huku hata madereva barani Ulaya wakikabiliwa na gharama kubwa za mafuta.
Shirika hilo linaeleza kuwa uchumi wa dunia bado unategemea kwa kiasi kikubwa nishati ya mafuta ya kisukuku, huku misukosuko ya kisiasa na kikanda ikiathiri upatikanaji wake.
Hata hivyo, linaonya kuwa gesi asilia (methane) ambayo mara nyingi huchomwa bila kutumika katika visima na mitambo ya kusafisha mafuta, inaweza kuhifadhiwa na kutumika ili kupunguza utegemezi huo.
Umoja wa Mataifa pia unasisitiza umuhimu wa kuharakisha mpito wa nishati safi, ikiwemo kuwekeza zaidi katika nishati jadidifu na umeme, hatua ambayo si tu itasaidia kulinda mazingira bali pia kuimarisha usalama wa nishati duniani.
Njaa yazidi kuwa mbaya Lebanon
Nchini Lebanon mapigano yanayoendelea kati ya wapiganaji wa Hezbollah na Israeli yanaendelea kusababisha hofu, athari za kiuchumi zimeathiri maisha, gharama zinazoongezeka na usumbufu wa usambazaji unazidisha uhaba wa chakula.
Wataalamu wa uhakika wa chakula wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa robo ya idadi ya watu wanakabiliwa na njaa Kali.
Tahadhari mpya kutoka kwenye tathimini imetolewa kupitia uchambuzi wa mfumo wa kubaini uhakika wa chakula (IPC) iliyotolewa tarehe 29 Aprili 2026 ilionya kwamba hali inazidi kuwa mbaya. Karibu watu milioni 1.2 wanaweza kukabiliwa na viwango vya juu vya uhaba mkubwa wa chakula kati ya sasa na mwezi Agosti, hili ni ongezeko kubwa kutoka 874,000 walioathiriwa mwishoni mwa mwaka 2025 na mwanzoni mwa mwaka 2026.
Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP lilisema kuwa “Nyuma ya kila idadi kuna familia zinazojitahidi kukidhi mahitaji yao ya chakula mara kwa mara,” huku ukiendelea kuongeza usaidizi kwa washirika.