MABOSI wa Simba wanaendelea na mchakato wa kuangalia maeneo ya kuboresha kwa ajili ya msimu ujao, ambapo mojawapo linaloangaliwa zaidi ni la beki wa kulia, analocheza nyota wa timu hiyo, Shomari Kapombe.

Kapombe aliyejiunga na Simba, Julai 1, 2017, akitokea Azam amekuwa muhimili wa kikosi hicho ambapo kwa sasa mabosi wa timu hiyo wanataka kumtafutia mbadala wake baada ya kutoridhishwa na kiwango cha David Kameta ‘Duchu’.

Licha ya Duchu kushindwa kuonyesha ushindani, kwa sasa mabosi wanaangalia uwezekano wa kumpata beki wa kulia wa Azam, Nathaniel Chilambo ambaye mkataba unamalizika mwisho wa msimu huu.

Chilambo aliyejiunga na Azam FC, Julai 6, 2022, akitokea Ruvu Shooting, inaelezwa anaweza kuondoka mwisho wa msimu pindi mkataba utakapoisha, baada ya kukosa pia nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Nyota huyo anayemudu pia kucheza beki wa kushoto, amekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kwa sababu ya ushindani uliopo na nyota wenzake pia kikosini, huku mshindani wake mkubwa akiwa ni nahodha, Lusajo Mwaikenda.

Kutokana na hilo, uongozi wa Simba umeanza mchakato wa kuinasa saini yake bure msimu ujao, ambapo inaelezwa makubaliano ya awali yamefikiwa kati ya pande zote mbili, hivyo kinachosubiriwa ni mkataba wake tu ufikie tamati mwisho wa msimu.

Hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa, ikiwa Chilambo atasajiliwa atakuwa ni mbadala sahihi wa David Kameta ‘Duchu’, ambaye tangu amesajiliwa Julai 10, 2023, akitokea Mtibwa Sugar, ameshindwa kuonyesha ushindani.

Chanzo hicho kilisema Chilambo ni mbadala sahihi wa Kapombe tofauti na Duchu, ingawa malengo yao ni kuipata saini ya beki wa kulia wa Singida Black Stars, raia wa Ivory Coast, Ande Koffi Cirille, anayemaliza mkataba wake mwisho wa msimu.

Cirille aliyejiunga na Singida Julai 1, 2024, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, mkataba wake wa miaka miwili aliousaini unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu, jambo linaloifanya Simba kuanza harakati za kumpata.

Chanzo kutoka ndani ya Singida kimeliambia Mwanaspoti kuwa nyota huyo aliyewahi kuchezea FC LYS Sassandra ya kwao Ivory Coast, amewekewa mkataba mpya ili kuendelea kubaki, ingawa ameomba kufanya uamuzi huo hadi mwishoni mwa msimu.

Chaguo la kwanza la Simba kwa mrithi wa Kapombe ni kuipata saini ya Cirille mwishoni mwa msimu huu, ingawa atakayekuja kusaidiana naye mwingine ni Nathaniel Chilambo atakayechukua nafasi ya Duchu, anayeweza kuondoka msimu huu utakapoisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *