Njombe. Historia mpya imeandikwa katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu baada ya kuanzishwa kwa kipengele maalum kinachotambua mchango wa wafanyakazi wa nyumbani.

Hatua hiyo imechukuliwa kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhi, Hoteli, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), ikiwa ni jitihada za kuthamini kundi hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifanya kazi bila kutambuliwa ipasavyo.

Maadhimisho hayo yaliyoratibiwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), pia yalihusisha utoaji wa vyeti na zawadi kwa wafanyakazi bora kutoka sekta mbalimbali, hatua inayolenga kuhamasisha uwajibikaji, bidii na uadilifu kazini.

Katika tukio hilo la kihistoria lililofanyika kitaifa mkoani Njombe, Neema Mollel alitangazwa mshindi wa kwanza katika kipengele hicho kipya na kukabidhiwa cheti maalum pamoja na zawadi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake na uaminifu kazini.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Neema amesema mafanikio yake yametokana na kujituma, kufuata sheria za kazi na kumsikiliza mwajiri wake.

Amesema kwa zaidi ya miaka sita aliyofanya kazi za nyumbani, amekuwa akipata haki zake za msingi ikiwemo likizo, bima ya afya na hifadhi ya jamii, hali iliyompa motisha na kuona kazi hiyo ina hadhi sawa na kazi nyingine.

“Naipongeza Serikali, ILO, TUCTA na CHODAWU kwa kuhakikisha nasi tunatambulika kama wafanyakazi wengine. Hii ni hatua kubwa kwa sekta yetu,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa Serikali kuridhia Mkataba wa ILO Namba 189 ili kuimarisha ulinzi wa haki za wafanyakazi wa nyumbani na kuboresha mazingira yao ya kazi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi wa nyumbani akiwemo Desderia Saimon kutoka Morogoro, wamesema licha ya hatua hiyo, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa mikataba rasmi na baadhi ya waajiri kutofuata sheria za kazi.

“Kuridhiwa kwa Mkataba wa ILO 189 kutasaidia kuweka mfumo imara wa kulinda haki zetu,” amesema Desderia.

Kwa upande wake, Husna Nkusa alisema kutambuliwa kwao katika maadhimisho hayo kumeongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii na uaminifu zaidi.

Naye Paulina Zozime amesisitiza umuhimu wa kuongezwa kwa elimu kwa waajiri kuhusu haki na wajibu wao ili kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Rehema Ludanga, amesema hatua ya kulitambua kundi hilo imelenga kuwapa thamani na heshima wanayostahili kama wafanyakazi wengine.

Amesema ushindi wa Neema Mollel unaashiria mwanzo wa safari mpya ya kuwainua wafanyakazi wa nyumbani na kuhakikisha wanapata haki na ulinzi unaostahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *