
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) la Iran amelaani vikali hatua ya vikosi vya utawala haramu wa Israel kuzuia kwa nguvu meli za Msafara wa Global Sumud zilizokuwa zikipeleka misaada ya kibinadamu Gaza.
Jeshi la Israel pia limewakamata wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina waliokuwa katika meli hizo. Brigedia Jenerali Esmail Qa’ani amesema kitendo hicho ni mfano dhahiri wa ugaidi wa kimataifa.
Ametoa kauli hiyo katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumamosi, kufuatia vikosi vya Israel kushambulia msafara wa misaada katika maji ya kimataifa karibu na pwani ya Ugiriki.
Jenerali Qa’ani amesema juhudi za wanaharakati hao za kuondoa mzingiro uliowekwa na utawala wa Israel dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza, na kujaribu kuwaokoa watoto na wanawake wa Kipalestina kutoka katika makucha ya Wazayuni, zinaonyesha kilele cha mapambano ya kimataifa dhidi ya wale wanaotenda ukatili dhidi ya maisha ya watu wasio na hatia.
Aidha, amesisitiza kuwa “vitendo vya fedheha vinavyofanywa na Wazayuni vitaimarisha tu azma ya wapenda uhuru kote ulimwenguni kuvunja mzingiro dhidi ya wakazi wanaodhulumiwa wa Gaza.”
Mwishoni mwa Jumatano, vikosi vya Israel vilizuia meli 22 kati ya meli 58 za misaada zilizokuwa zikisafiri katika maji ya kimataifa kuelekea Ukanda wa Gaza uliozingirwa.
Inaripotiwa kuwa angalau wanaharakati 211, akiwemo diwani kutoka jiji la Paris, walipelekwa Israel. Maafisa wa Israel, hata hivyo, wamedai kuwa idadi ya waliokamatwa ni 175.
Meli hizo ni sehemu ya msafara wa pili wa Global Sumud ambao katika miezi ya karibuni umekuwa ukijaribu kuvunja mzingiro wa Israel kwa kusafirisha misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza. Msafara huo uliondoka katika bandari ya Barcelona, Hispania, tarehe 12 Aprili.
Meli hizo zilikamatwa karibu na rasi ya Peloponnese nchini Ugiriki, mamia ya maili kutoka Gaza.
Katika taarifa yake, msafara wa Sumud umesema wanaharakati 31 walijeruhiwa wakati wa shambulio la vikosi vya Israel.