KIUNGO mshambuliaji wa She Corporate FC ya Ligi Kuu ya Wanawake Uganda, Husna Mpanja amesema mechi mbili zilizosalia kwenye ligi zinawabana na kuwapa presha kubwa kwenye harakati za kuwania ubingwa.

Mpanja amesema kwa sasa timu hiyo ipo kileleni ikiwa na tofauti ya pointi mbili dhidi ya wapinzani wao, hali inayofanya kwa mechi zilizobaki kulazimika kushinda.

“Tupo nafasi ya kwanza, tunamzidi mpinzani pointi mbili. Ni ngumu kwa sababu mechi mbili zilizobaki tunatakiwa kushinda zote ili tuchukue ubingwa,” amesema Mpanja.

HUSN 01

Kiungo huyo Mtanzania ameongeza kama atachukua ubingwa itakuwa mara yake ya kwanza kuubeba tangu aanze kucheza soka.

“Kwanza tukichukua ubingwa itakuwa rekodi kwangu kubeba taji nikiwa nje ya Tanzania, pia itanipa zaidi motisha ya kupambana msimu ujao kwa kuwa huu bado nilikuwa chini ya uangalizi.”

Kabla ya kutua Uganda, aliwahi kukipiga timu za Ruvuma Queens, Tiger Sports Academy, Yanga Princess, Fountain Gate Princess na Geita Queens.

Anafichua safari yake ya kufika Uganda kuwa baada ya kuondoka Tiger Sports Academy alipata nafasi ya kwenda kucheza India katika klabu ya Sethu, lakini mambo hayakwenda kama yalivyotarajiwa.

HUSN 02

“Baada ya kutoka Tiger Sports nilipata timu India inaitwa Sethu, lakini baada ya kutoka Kombe la Dunia la U-17 niliporudi kulikuwa na changamoto kidogo, nikarudi Tanzania na nikakuta usajili umefungwa,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema alitumia nafasi ya dirisha la usajili la Uganda ambalo bado lilikuwa wazi na kujiunga na Makerere University (She Mak), kabla ya kurejea tena Tanzania na kucheza Yanga Princess kisha Fountain ambako ndiko alikoonekana na timu hiyo ya Uganda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *