Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza kuimarisha uwezo wa uongozi katika sekta ya afya kupitia awamu ya pili ya Mpango wa Kukuza Uongozi ili kubadilisha na kuimarisha sekta ya afya Afrika (PHLTA), hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.
Mpango huo umewaleta pamoja Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs), Waganga Wakuu wa Wilaya (DMOs) pamoja na maofisa kutoka Idara ya Sera na Mipango ya Wizara ya Afya, mwishoni mwa wiki wakipatiwa mafunzo maalumu ya uongozi ili kukabiliana na changamoto za mifumo ya afya.
Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya afya nchini ikikabiliwa na mabadiliko ya mzigo wa magonjwa, ongezeko la mahitaji ya huduma na changamoto za kiutendaji, hali inayohitaji viongozi wenye uwezo wa kufanya uamuzi wenye tija na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Serikali, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), iliandaa na kuanzisha mpango huo kutokana na azimio la mwaka 2020 la mawaziri wa afya Afrika la kujenga kizazi kipya cha viongozi wa mageuzi katika sekta ya afya.
Tathmini ya mahitaji ya mafunzo iliyofanyika mwaka 2024 kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Kituo cha Maendeleo ya Elimu ya Afya Arusha (CEDHA) pamoja na RMOs, ilibaini kuwa licha ya uwepo wa mafunzo ya kitaalamu, bado hayajatafsiriwa ipasavyo katika uongozi bora wa vitendo.
Kupitia PHLTA, washiriki wanahimizwa kuanza kwa kujiuliza dira ya sekta ya afya wanayoijenga na mustakabali wa Afrika kwa ujumla, huku wakifundishwa mbinu ya fikra za kimfumo zinazowawezesha kuona mfumo mzima badala ya kutatua changamoto kwa mtazamo finyu.
Aidha, mafunzo hayo yanasisitiza umuhimu wa kubadilika kutoka mtazamo usiobadilika kwenda mtazamo unaokua, kwa kuzingatia tafakari, kujifunza endelevu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko.
Washiriki walionesha ushiriki mkubwa wakati wa mafunzo hayo, wakibadilishana uzoefu wa changamoto halisi wanazokutana nazo katika maeneo yao ya kazi, zikiwemo utendaji wa timu, mawasiliano, motisha ya watumishi na vikwazo vya utoaji huduma.
Akizungumza kuhusu mpango huo jana, Mei 2, 2026, Mratibu wa Mifumo ya Afya wa WHO, Dk Thomas Tefoyet, amesema tofauti na nchi nyingine zinazolenga viongozi wa ngazi ya juu, Tanzania imewekeza zaidi kwa viongozi walioko karibu na utoaji huduma.
“Kwa kuimarisha uongozi wa RMOs na DMOs, tunatarajia kuongeza motisha kwa watumishi, kuboresha utendaji na kuinua ubora wa huduma za afya,” amesema.
Kwa upande wake, Profesa Nathanael Sirili wa MUHAS amesema taasisi hiyo inashirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha mpango huo unakuwa endelevu.
Amesema MUHAS inapanga kuandaa mitaala maalumu ya uongozi wa afya inayozingatia mazingira ya Tanzania, pamoja na kuwajengea uwezo washiriki ili wawe wakufunzi watakaosambaza mafunzo hayo nchi nzima.
Mpango wa PHLTA unajikita katika maeneo matatu ya uongozi ambayo ni kujiongoza binafsi, kuongoza timu na kuongoza taasisi. Washiriki huanza kwa kujitambua, kisha kujenga uwezo wa kusimamia timu na hatimaye kuelekea katika mabadiliko ya kimkakati ya taasisi.
Baada ya mafunzo, washiriki wanatarajiwa kuingia katika kipindi cha miezi sita cha utekelezaji, ambapo kila mmoja ataandaa na kutekeleza mradi wa kuboresha huduma za afya katika eneo lake, akipata ushauri na ufuatiliaji wa karibu.
Kupitia mpango huo unaoungwa mkono na WHO, Tanzania inalenga kuwa na viongozi wa afya wenye uwezo wa kubadilika, kujifunza na kuongoza mageuzi yatakayoboresha huduma za afya kwa wananchi.