Songwe. Serikali imesaini mkataba wa mradi wa kimkakati wa uchimbaji na uvunaji wa gesi ya helium kwa kushirikiana na Kampuni ya Helium One Global Limited kupitia Kampuni ya ubia ya Songwe Helium Limited, hatua inayofungua njia ya kuanza uzalishaji wa rasilimali hiyo adimu duniani.
Mradi huo unatarajiwa kuanza uzalishaji Novemba 2027 na kuifanya Tanzania kuingia katika soko la kimataifa la helium lenye thamani kubwa huku ushindani ukiwa mdogo.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ilifanyika Mei 2, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa wananchi pamoja na viongozi wa dini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema Tanzania imeanza safari mpya ya kihistoria ya uzalishaji wa helium.
Amesema mradi wa gesi ya helium wa Southern Rukwa ni wa kimkakati na utaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa rasilimali hiyo duniani.
Amefafanua kuwa kwa sasa uzalishaji wa helium duniani unatawaliwa na nchi chache, hususan Marekani na Qatar, ambazo kwa pamoja huchangia zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wote. Nchi nyingine zinazozalisha kwa kiwango kidogo ni pamoja na Urusi, Algeria, Canada, China na Poland.
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa (wapili kushoto) akiwa ameshikana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Helium One Global Limited, Lorna Blaisse na kuonyesha mkataba waliosaini kuanza uchimbaji wa gesi ya Helium wilayani Momba mkoani Songwe. picha na Denis Sinkonde
Dk Kiruswa ameongeza kuwa mahitaji ya helium duniani yamefikia zaidi ya futi za ujazo bilioni sita kwa mwaka na yanatarajiwa kuongezeka zaidi ifikapo mwaka 2030 kutokana na matumizi yake katika sekta za teknolojia na afya.
Aidha, amesema Serikali itamiliki asilimia 17 ya hisa katika kampuni ya ubia ya Songwe Helium Limited ili kuhakikisha Taifa linanufaika moja kwa moja na rasilimali hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Wizara ya Madini, Sifuni Mchome alisema utaratibu wa Serikali kumiliki hisa huru zisizohafifishwa thamani unaipa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika miradi ya madini.
Ameongeza kuwa kupitia mfumo huo, Serikali itanufaika kwa gawio, mrabaha, kodi na tozo mbalimbali, huku ikihakikisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa masilahi ya wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Helium One Global Limited, Lorna Blaisse amesema mradi huo uko tayari kuanza uzalishaji wa kibiashara kufuatia mafanikio ya utafiti uliofanyika.
Amebainisha kuwa mafanikio ya Kisima cha Itambula West-1 mwaka 2024 yalithibitisha uwepo wa helium kwa kiwango kinachoweza kuendelezwa kibiashara.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame amesema mradi huo unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo kwa kuongeza ajira, kuboresha miundombinu na kuinua kipato cha wananchi.