Dodoma. Serikali imekemea tabia ya baadhi ya watumishi kutokujali na kuthamini rasilimali za umma, pamoja na kutofuata maadili katika maeneo wanayofanyia kazi, wakitakiwa kubadilika, vinginevyo asiwepo wa kumlaumu mwingine.

Onyo hilo limetolewa jana Mei 2, 2026 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, Xavier Daudi, akizungumza na Baraza la Wafanyakazi na Mkutano Mkuu wa mwaka wa watumishi katika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (NBS), ambapo alizuia mpango wa kuhamisha mtumishi aliyeharibu na kumpeleka mahali pengine.

Amesema limeibuka wimbi la matumizi yasiyofaa kwa watumishi wa umma, ambapo wanajali zaidi vifaa vyao vya kazi binafsi kuliko vya ofisini, huku suala la muda kazini haliangaliwi wala kujali.

Naibu Katibu Mkuu huyo ametolea mfano wa magari ya umma kwamba yakiharibika kidogo huachwa na kutelekezwa, yanaozea hapo, wakati gari la mtu binafsi lisingeachwa; na kingine, kwa makusudi wanaondoka na kuacha taa zinawaka ofisini, ingawa majumbani kwao wanazima.

“Jambo lingine ambalo limekuwa ni kero ni hili la mavazi, watu wanavaa kama ilivyo kwa watu wa mitaani wakati tuna waraka unaotuelekeza jinsi ya kuvaa, na utamkuta mtumishi anafika ofisini muda anaotaka na kuondoka muda anaotaka, hatutimizi wajibu wetu, lazima tubanane,” amesema Daudi.

Amesema suala la kubembelezana kwa mtu anayeharibu halafu akahamishiwa pengine kupeleka uozo isiwe tabia ya Serikali, badala yake mhusika ashughulikiwe mahali alipo iwe fundisho.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk Amina Msengwa

Kwa upande wa watakwimu, amewaomba kufanya kazi kwa weledi ili wazalishe takwimu sahihi zenye manufaa kwa nchi, huku wakitambua wapo wasomi wengi wangetamani kufanya kazi serikalini lakini hawajapata fursa hizo.

“Siku hizo unaweza kutangaza nafasi moja ya utumishi wakaja kwenye usaili watu 50,000, sasa tuangalie fursa hizo kwetu. Inaumiza jambo dogo ambalo mtumishi wa chini angeweza kulitatua lakini ninasubiri viongozi wa ngazi ya juu, ni aibu. Toeni takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesisitiza.

Hata hivyo, ameipongeza NBS kuwakutanisha watumishi kwa pamoja katika mkutano wa kujadili masuala muhimu, akisema vikao vya pamoja ndiyo afya ya utumishi, na kusisitiza taasisi zote za Serikali kuiga mfano huo.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Amina Msengwa, amesema kazi iliyopo mbele yao ni kuhakikisha wazalishaji wote wa takwimu wanaendana na hali halisi ya sayansi na teknolojia kulingana na wakati.

Dk Msengwa amesema wanaendelea kutoa mafunzo ya kimaadili pamoja na mbinu za matumizi ya teknolojia ili kuwezesha kila mmoja asikabiliwe na ugumu wa utendaji wa kazi kwenye ulingo wa sayansi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *