KOCHA Mkuu wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi amesema hadi sasa msimu huu timu hiyo iko katika uelekeo mzuri Championship, licha ya ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao wakubwa, ambao kila mmoja anataka kupanda Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalwisi amesema kadri ligi inavyosonga mbele ndivyo ushindani unavyoongezeka kutokana na malengo ya kila timu iliyojiwekea, hasa zile zinazowania kupanda ligi kuu.

“Nimewaambia wachezaji tucheze mechi zetu na kuhakikisha tunashinda bila ya kuangalia wapinzani wetu wengine wanafanya nini, lengo ni kuepuka presha kubwa ambayo mwisho wa safari yetu inaweza kutuangusha pia,” amesema Mwalwisi.

Msimu huu kikosi hicho kiko nafasi ya tatu na pointi 51, nyuma ya Kagera Sugar iliyokusanya pointi 58, ikiwa ya pili, huku vinara Geita Gold yenye 61, imecheza mechi 23 hadi sasa, imeshinda 16, sare tatu na kupoteza nne.

Kocha huyo wa zamani wa Ihefu (sasa Singida Black Stars), licha ya uzoefu mkubwa alionao wa kufundisha timu mbalimbali ikiwemo TMA ya Arusha, ana kazi ya kuipigania Mbeya Kwanza irejee Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2021-2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *