
Tandahimba. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, wamemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mariam Mwanzalima kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu matumizi ya Sh107 milioni zilizotengwa kwa ajili ya ziara na mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Hoja hiyo imeibuka baada ya fedha hizo kutoonekana katika taarifa ya mapato na matumizi iliyowasilishwa mbele ya Baraza la Madiwani, jambo lililosababisha sintofahamu miongoni mwa wajumbe.
Suala hilo lilijadiliwa katika kikao cha baraza kilichofanyika Aprili 29, 2026, wakati wajumbe wakichambua taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha.
Baadhi ya madiwani waliochangia mjadala huo walieleza kushangazwa na kutokuwepo kwa taarifa za matumizi ya fedha hizo, wakitaka maelezo ya wazi kuhusu zilipo na namna zilivyotumika.
Diwani wa Mkoreha, Saidi Melenje amesema ni jambo la kushangaza kuona suala la kiutendaji lenye kumbukumbu kushindwa kufafanuliwa.
Amehoji iwapo fedha hizo hazipo au zinakusudiwa kutumika kwingine bila taarifa rasmi.
Amesema hali hiyo inaibua hofu ya kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu katika halmashauri hiyo, jambo linaloweza kusababisha upotevu wa fedha za umma bila maelezo sahihi.
Diwani wa Mkwiti, Shaibu Nnalu amesema licha ya madiwani kufanya ziara Zanzibar Novemba mwaka jana, bado kulitengwa fedha nyingine katika bajeti ya mwaka 2025/26, lakini matumizi yake hayajaelezwa.
Mbunge wa Tandahimba, Ahmad Katani amesema madiwani wamekuwa wakifuatilia suala hilo hata nje ya vikao rasmi na wana kumbukumbu sahihi za uamuzi uliopitishwa.
Amesisitiza kuwa mabadiliko yoyote ya matumizi ya fedha, yanapaswa kuwashirikisha madiwani mapema.
Awali, akijibu hoja hizo, Mwanzalima ambaye ni mkurugenzi aliomba muda kupitia upya taarifa husika ili aweze kutoa majibu ya kina kuhusu kiasi kilichotumika na kilichobaki.
Hata hivyo, Diwani wa Lukokoda, Abbas Membe hakuridhishwa na majibu hayo, akieleza kuwa suala hilo liko wazi na halihitaji uchunguzi wa ziada kwa sababu wahusika wanajulikana.
Katika majibu yake ya baadaye, Mwanzalima alikiri kuwepo kwa changamoto katika usimamizi wa taarifa za matumizi ya fedha, akieleza huenda kulikuwa na uzembe wa kiutendaji uliosababisha kuchanganywa kwa matumizi bila taarifa kwa madiwani.
Amewahakikishia madiwani kuwa suala hilo litashughulikiwa kabla ya mwaka wa fedha kuisha.
Pamoja na majibu hayo, madiwani wamesisitiza umuhimu wa uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji taarifa, ili kuepusha sintofahamu na kulinda imani ya wananchi kwa viongozi wao.