Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema vijana walioanza ajira karibuni na wale waliojiajiri watapewa kipaumbele katika kupewa nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Serikali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa nyumba 144 za gharama nafuu zilizojengwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) wilayani Temeke jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Mei 3, 2026, Ulega amesema hatua hiyo imetokana na Serikali changamoto ambazo vijana wanazipitia kwenye kupata nyumba za gharama nafuu kuishi.
“Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2020, Tanzania ina upungufu mkubwa wa nyumba. Kwa kuzingatia hilo, tumeamua kuanza kuchukua hatua za makusudi kushughulikia changamoto hiyo.
“Nyumba hizi 144 ni hapa Dar es Salaam. Lakini Rais wenu, Samia Suluhu Hassan, ameidhinisha pia ujenzi wa nyumba za namna hii mkoani Dodoma na katika miji mingine mikubwa ili kupambana na changamoto hii,” amesema Ulega.
Kati ya nyumba hizo 144 zilizozinduliwa, 72 ni nyumba za chumba kimoja, sebule, jiko na choo na 72 nyingine ni nyumba za vyumba viwili ambapo kimoja ni self-contained, sebule, jiko na choo cha pamoja (common toilet).
Ulega amesema mpango huu utaendelea kupanuliwa katika mikoa mingine ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wanapata makazi bora na nafuu kwa awamu na kwa usawa katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji.
Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Mkuranga mkoani Pwani, amesema vijana walioajiriwa na waliojiajiri wanalazimika kukaa mbali na maeneo yao ya kazi kutokana na uhaba wa nyumba, jambo linaloathiri muda wao wa kuchapa kazi.
Amesema kwa kujenga nyumba katika maeneo ya mijini ambako kuna watu na fursa nyingi zaidi, Serikali inaweka mazingira mazuri kwa vijana kutumia muda mwingi zaidi kuchapa kazi badala ya kuhangaika kutafuta nyumba na usafiri.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega akichanganya udongo na saruji wakati wa uzinduzi wa nyumba 144 za gharama nafuu zilizojengwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) wilayani Temeke jijini Dar es Salaam
Waziri huyo amewaambia wananchi waliohudhuria tukio hilo suala la ujenzi wa nyumba za gharama nafuu si la wizara yake pekee bali ni sehemu ya Mipango ya Muda Mrefu ya Serikali kupitia Dira ya 2050.
“Mkiona Waziri wa Ujenzi yuko hapa leo si kwa sababu hili ni suala lake binafsi au wizara yake. Suala la nyumba liko kwenye Dira 2050 na hii ni sehemu ya utekelezaji wake,” amesema.