Dar es Salaam. Tanzania na Rwanda zimeapa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi, huku Rwanda, kwa miaka 29, ikisajili miradi 42 ya uwekezaji nchini yenye thamani ya Dola milioni 325.5 za Marekani (zaidi ya Sh813.7 bilioni).

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, miradi hiyo imesajiliwa kupitia Mamlaka ya Uwekezaji nchini na imezalisha jumla ya ajira 2,225 kwa Watanzania.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumapili Mei 3, 2026, alipozungumza mbele ya waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kikao na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, aliyewasili nchini kwa ziara ya siku moja.

Rais wa Jamhuri ya Rwanda. Paul Kagame wakati akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kikazi, Mei 03, 2026. Kulia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Amesema miradi hiyo ya uwekezaji ni ya kipindi cha mwaka 1997 hadi Machi mwaka huu, huku biashara kati ya mataifa hayo ikifikia Sh644 bilioni kwa mwaka uliopita.

“Licha ya kwamba takwimu hizo zinatia moyo kwenye biashara yetu, tumekubaliana kuendelea kushirikiana ili kukuza uwekezaji, hususan kwa kuondoa vikwazo vya kikodi. Tuzungumze, tuviondoe ili tunufaike na masoko ya kikanda chini ya EAC na Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA),” amesema.

Rais Samia amesema ziara hiyo ya Kagame inaakisi uhusiano wa karibu na wa muda mrefu kati ya mataifa hayo jirani, akieleza kuwa Tanzania na Rwanda si majirani tu, bali ni ndugu na marafiki.

“Tanzania na Rwanda si majirani tu, bali pia ni ndugu na marafiki. Uhusiano wetu una mizizi ya kihistoria hata kabla ya ukoloni, ndiyo maana tamaduni, mila na watu wetu wanafanana kwa karibu,” amesema.

Amesema nchi hizo zinaendelea kushirikiana kupitia majukwaa ya kikanda na kimataifa, ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU), Harakati za Nchi Zisizofungamana na Siasa za Kambi Moja (NAM) na Umoja wa Mataifa (UN).

“Uwekezaji huu unaonesha kuimarika kwa imani kati ya nchi zetu, ingawa bado kuna fursa nyingi zaidi ambazo hazijatumika ipasavyo,” amesema.

Amesema sekta binafsi ya Tanzania nayo imepanua uwekezaji wake nchini Rwanda kupitia kampuni za Bakhresa Group, Magodoro Dodoma, Discount Centre, Jumbo Plastics, Sugar Enterprises, Hagar Enterprises, Buffalo Travelling Tours, Maxcom Africa, Gasabo Brain Mining Company, LCM Delta Company na Matrix Integrated Consult.

Katika sekta ya usafirishaji na usafirishaji wa mizigo, Rais Samia amesema takribani asilimia 70 ya mizigo ya Rwanda hupitia Bandari ya Dar es Salaam, ambayo hushughulikia wastani wa tani milioni 1.6 za mizigo ya nchi hiyo kila mwaka.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Ziara ya Kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mei 03, 2026.

“Kama nchi yenye bandari, tuna wajibu wa kuhakikisha nchi zisizo na bandari zinahudumiwa kwa ufanisi. Tumekubaliana kuboresha zaidi huduma bandarini na kuweka mifumo maalumu ya kurahisisha mizigo ya Rwanda,” amesema.

Katika kikao chao cha uwili, amesema walijadili miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwemo reli ya kisasa (SGR) ya Isaka hadi Kigali, inayotarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi wa biashara.

Katika sekta ya nishati, amesema Tanzania, Rwanda na Burundi zinafaidika na mradi wa umeme wa maporomoko ya Rusumo unaozalisha megawati 80, huku nchi hizo zikikubaliana kuimarisha biashara ya umeme kati ya Tanesco na Rwanda Energy Group (REG).

Amesema ushirikiano katika mawasiliano, hususan upanuzi wa miundombinu ya nyuzi macho, ni eneo jingine litakaloimarishwa ili kuboresha huduma za kidijitali na mawasiliano ya kikanda.

Mengine waliyojadiliana, amesema, ni masuala ya usalama na utulivu.

Kwa upande wake, Rais Kagame ameeleza mazungumzo yao yalikuwa yenye tija na yenye mwelekeo mzuri, yakijenga juu ya msingi imara wa ushirikiano uliopo.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanznia akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kikazi, Mei 03, 2026.

“Ni furaha kuwa hapa. Mazungumzo ya leo yameimarisha uhusiano wetu na kuangazia namna ya kuongeza ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi wetu,” amesema.

Ameitaja Tanzania kama mshirika muhimu wa Rwanda, hasa kupitia Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni lango kuu la nchi hiyo kuingia katika masoko ya kimataifa.

“Tanzania ni mshirika muhimu sana kwa Rwanda. Ushirikiano wetu katika biashara na usafirishaji ni nguzo ya muunganiko wetu na dunia,” amesema.

Aidha, Kagame amesisitiza umuhimu wa umoja wa kikanda kupitia EAC na AU, hasa katika kipindi cha mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani.

Rais Kagame amesema Rwanda inaendelea na maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi, na itawatambua Watanzania walioonyesha ujasiri na ubinadamu wakati wa kipindi hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *