Nchini DRC, chama UDPS cha kwake rais Felix Tshisekedi, kinatarajiwa kufanya maandamano ya amani kuonesha uungaji mkono wao kwa rais wa Marekani Donald Trump pamoja na mpango wa amani wa nchi hiyo unaoratibiwa na Washington.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Awali maandamano hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika Jumapili Mei 2 lakini baadae katibu mkuu wa chama hicho, Augustin Kabuya, alisema yamesogezwa mbele hadi Jumatatu ya wiki hii, maandamano yanayoenda kufanyika siku chache kupita tangu Marekani imuwekee vikwazo rais wa zamani Joseph Kabila kwa madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda.

Aidha vikwazo dhidi ya rais Kabila, vinafuatia vile vilivyowekwa kwa maofisa wa M23 na jeshi la Rwanda, Washington ikiwaonya wanaochochea machafuko mashariki mwa DRC.

Kabuya amesema lengo la maandamano hayo ni kuwasilisha ujumbe wa mshikamano kwa rais wa Marekani kupitia ubalozi wa nchi hiyo mjini Kinshasa, ambapo wataanzia makao makuu ya UDPS kupitia eneo la People’s Palace hadi ubalozi wa Marekani.

Tangu Marekani iingilie kati kusaidia juhudi za kupata amani ya kudumu mashariki mwa nchi hiyo, utawala wa Kinshasa umekuwa karibu na Washington, ambapo umesaini mikataba kadhaa ya ushirikiano wa kiuchuimi na Marekani ikiwemo madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *