ALIYEWAHI Kocha wa zamani wa Ruangwa Queens, Mwinyi Zahera amesema ili timu hiyo isalie Ligi Kuu msimu ujao, inapaswa kufanya mambo mawili.
Kabla ya kuachana na timu hiyo, mkongomani huyo aliwahi kuzifundisha timu za Ligi Kuu Bara ikiwemo Yanga msimu 2018/19, Polisi Tanzania (2022/23), Coastal Union (2023) na Namungo (2023/24).
Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera amesema Ruangwa inapaswa kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha inashinda angalau mechi tano kati ya saba zilizosalia.
Ameongeza, kwa kuwa Mkoa wa Lindi una timu moja ya Wanawake anashauri viongozi wa wilaya kuisapoti ili kuipa nguvu msimu ujao.
“Hii timu raundi ya kwanza tulikuwa tunajifunza, tulifungwa mechi saba kwa kudhulumiwa sana tulidondosha pointi 21, ni nyingi mno, angalau tungepata pointi hata 10,” amesema Zahera na kuongeza;
“Sasa ili ibaki, inapaswa kwanza kuwa na mipango ya namna gani wanashinda mechi zilizosalia, pia kutafuta kocha wa kuokoa kwa sababu hadi sasa hawana kocha mwenye uwezo.”
Zahera aliifundisha Ruangwa Queens hadi mzunguko wa kwanza ulipomalizika timu hiyo ilipomaliza mkiani mwa msimamo wa ligi.
Katika mechi saba zilizosalia, Ruangwa itaikaribisha Geita Queens, (Mei 14), v Simba Queens (Mei 19) ugenini, v Tausi FC nyumbani, v JKT Queens ugenini, v Alliance Girls nyumbani, v Ceasiaa Queens nyumbani na kumalizia ugenini dhidi ya Fountain Gate Princess.