ACHANA na matokeo ya ushindi walioupata Mbeya City juzi dhidi ya Tanzania Prisons, kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amesema bado anayo kazi ngumu katika kuisuka safu yake ya ulinzi ili kutoruhusu mabao.

Kwa mara ya kwanza timu hiyo ilionja ushindi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya baada ya kusubiri kwa muda mrefu katika mechi za Ligi Kuu Bara kufuatia kipigo cha mabao 2-1 ilichotoa kwa ndugu zao, Prisons na kupanda nafasi ya 13 kwa pointi 21 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Timu hiyo inatarajia kushuka tena uwanjani Mei 9 mwaka huu kuivaa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, huku ikihitaji pointi tatu zaingine ili kuzidi kupanda nafasi za juu na kufufua matumaini ya kubaki salama Ligi Kuu.

Katika michezo 21 iliyocheza Mbeya City msimu huu, ni mechi mbili tu zilizoisha bila kuruhusu mabao, huku 19 ikiruhusu wavu wake kuguswa hali inayompa machungu Mayanga kuitafutia mwarobaini safu ya ulinzi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga aliyeiongoza timu hiyo michezo miwili akishinda mmoja sawa na sare, alisema wastani wa kuruhusu mabao kila mchezo si hali nzuri na anaisukia mkakati kuhakikisha inakuwa imara.

Alisema kwa michezo tisa iliyobaki ni vita kali kwake kuhakikisha timu haishuki daraja, akieleza kuwa anachotaka ni vitendo uwanjani badala ya maneno akiomba sapoti kwa wadau na mashabiki ili kufikia malengo.

“Bado kazi si nyepesi licha ya kufunga mabao lakini tumekuwa tunaruhusu pia kufungwa, lazima nilifanyie kazi kwa kuimarisha beki yangu, kwa sasa hatutaki maneno ni vitendo uwanjani,”  alisema kocha huyo.

Mbeya City ambayo imerejea msimu huu Ligi Kuu, katika michezo tisa iliyobakiza, itakuwa nyumbani minne dhidi ya Coastal Union, Mtibwa Sugar, Simba na TRA United, huku ikienda ugenini kucheza dhidi ya JKT Tanzania, Namungo, Dodoma Jiji, Singida Black Stars na Pamba Jiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *