Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imetenga Sh80 milioni kwa ajili ya kukabiliana na athari za makorongo pamoja na kufanya ukarabati wa madarasa yaliyoathirika na mvua katika shule za msingi Malambamawili na Bwawani zilizopo kata ya Msigani.
Hatua hiyo imechukuliwa jana Jumatatu, Mei 4, 2026, siku hiyo ambayo Gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii lilichapisha ripoti maalumu iliyohusu ujenzi wa shule maeneo hatarishi wageuka janga.
Hali hiyo imetokana na hofu iliyojitokeza miongoni mwa wazazi, walimu na wanafunzi kutokana na kuongezeka kwa nyufa na mmomonyoko wa ardhi katika baadhi ya shule za manispaa hiyo, hali inayohusishwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Katika ziara ya kukagua hali halisi ya shule hizo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Albert Msando, akiongozana na Diwani wa Msigani, Zaidi Muliro, walishuhudia uharibifu katika baadhi ya majengo pamoja na udongo unaozidi kusombwa na maji ya mvua.
Wanafunzi wakipita jirani na darasa ambalo kingo moja ya ukuta imeanguka kutokana na mvua katika shule ya Msingi Malamba Mawili iliyopo Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Mei 5, 2026 kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Dk Aron Kagurumjuli amesema fedha hizo zitatumika kurekebisha miundombinu iliyoharibika.
Hatua hizo zinakuja wakati ambao wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na mvua zinazosababisha kuongezeka kwa makorongo, hasa katika shule zilizopo maeneo ya miinuko na jirani na mto.
Wananfunzi wakifanya usafi kwenye moja ya korongo lililopo katika shule ya msingi Malamba Mawili iliyopo wilaya ya ubungo jijini Dar es Salaam.
“Tumetenga bajeti maalumu ya kushughulikia makorongo na kurekebisha madarasa yaliyoathirika ili kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo katika mazingira salama,” amesema Dk Kagurumjuli.
Amesema marekebisho hayo yatafanyika baada ya mvua kuisha kwa sababu hawezei kurekebisha makorongo
Muliro ambaye ni diwani amesema wametembelea shule mbili na kujionea hali halisi akiwa na mkuu wa wilaya hivyo Halmashauri ingeeleza kila kitu.
“Tumetembelea shule mbili ya Malambamawili na Bwawani jana na kujionea uhalisia lakini uongozi wa Wilaya unaweza kuongea kila kitu kuhusu hatua zilizochukuliwa,”amesema Muliro.