
Dar es Salaam. Serikali imeamua kuanza upya mchakato wa kuandaa Mpango wa Uendelezaji wa Eneo la Sinza baada ya wananchi kulalamikia kutoshirikishwa vya kutosha katika hatua za awali na kuibua maswali kuhusu umiliki wa ardhi na hatima ya mali zao.
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatano Julai mosi, 2026 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo ukiashiria mabadiliko katika utekelezaji wa moja ya miradi mikubwa ya uendelezaji wa makazi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Sinza wilayani Ubungo, Dk Akwilapo amesema mikutano yote ya awali haitakuwa msingi wa mchakato mpya, huku akisisitiza kuwa wananchi wote watapatiwa nafasi ya kushiriki katika kuandaa mpango huo.
“Mapendekezo yote yaliyowasilishwa yatazingatiwa, lakini mikutano ya awali haitakuwa sehemu ya mchakato huu. Tunaanza upya ili kila mwananchi apate nafasi ya kutoa maoni yake,” amesema.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakazi wengi kueleza kutoridhishwa na namna rasimu ya Mpango wa Uendelezaji wa Sinza wa mwaka 2026–2046 ilivyoandaliwa, wakidai walipewa taarifa baada ya uamuzi kufanyika.
Mkazi wa Sinza A, Sufiani Rajabu amesema changamoto kubwa ya mchakato wa awali ilikuwa kutoshirikishwa kwa wananchi wanaomiliki ardhi katika eneo hilo.
“Sisi ndio wamiliki wa ardhi hii. Tunaposema hatukushirikishwa ni kwa sababu kweli hatukushirikishwa. Tunataka maendeleo, lakini yashirikishe wananchi tangu mwanzo,” amesema.
Amesema wananchi wengi hawakupinga maendeleo, bali walipinga namna uamuzi uliohusu mchakato mzima.
Mkazi mwingine wa Sinza C, Jumanne Ramadhani ameibua wasiwasi kuhusu hatima ya umiliki wa ardhi endapo utekelezaji wa mpango huo utahusisha kuunganishwa kwa viwanja.
“Ikiwa viwanja kadhaa vitaunganishwa kuwa eneo moja, umiliki wake utakuwa wa namna gani? Haya ni baadhi ya maswali ambayo hayakupata majibu ya kuridhisha,” amesema.
Mwanasheria na mjumbe wa Kamati ya Wamiliki wa Ardhi na Mali Sinza, Ramadhani Chaurembo amesema rasimu ya mpango huo iliandaliwa kwa Kiingereza, jambo lililowafanya wananchi wengi washindwe kuielewa.
“Kuandaa nyaraka kwa Kiingereza pekee kuliondoa fursa ya wananchi wengi kushiriki kikamilifu. Mchakato unaohusu wananchi unapaswa kutumia lugha wanayoielewa,” amesema.
Pia, amesema baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo vilitafsiriwa kana kwamba wamiliki wa ardhi wangeweza kulazimishwa kuuza mali zao, hali iliyozua hofu miongoni mwa wananchi.
Akijibu hoja hizo, Dk Akwilapo amekiri kuwa kulikuwa na upungufu katika ushirikishwaji wa wananchi, lakini amewataka wakazi wa Sinza kujitokeza kwa wingi kila panapoitishwa mikutano.
“Mara nyingi mikutano huitishwa lakini wanaohudhuria ni wachache. Ni muhimu kila mmoja ashiriki kwa sababu maamuzi haya yanahusu maisha yenu ya baadaye,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa uendelezaji wa Sinza ni muhimu ikiwa Dar es Salaam inataka kuwa jiji la kisasa lenye makazi yaliyopangwa vizuri na miundombinu bora.
Amesema wataalamu na wananchi wataendelea kushirikiana kuamua sura ya baadaye ya eneo hilo, huku akifafanua kuwa utekelezaji wa mradi hautafanyika kwa wakati mmoja katika kata nzima kwa kuwa maoni ya wananchi yanahitaji kwanza kupatanishwa.
Dk Akwilapo amesema mpango utakaoboreshwa utazingatia sheria na miongozo ya mipango miji, huku ukilenga kuboresha makazi, miundombinu na huduma za kijamii.
Amesema pia utekelezaji wake utasaidia kutatua changamoto za muda mrefu za miundombinu katika eneo la Sinza, ikiwamo ukosefu wa mfumo wa maji taka.
“Sinza ya zamani lazima ipangwe upya. Baadhi ya maeneo yameendelea, mengine bado, lakini hatuwezi kuendelea kusubiri milele,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema miundombinu duni imezuia maeneo mengi ya Sinza kufikia thamani yake halisi licha ya kuwa katika eneo lenye fursa kubwa za uwekezaji.
Amesema pamoja na kuboreshwa kwa barabara katika miaka ya karibuni, maeneo mengi bado hayana mifumo ya majitaka na huduma za majisafi zinakabiliwa na changamoto za nafasi ya kupitisha miundombinu.
“Hakuna mpango wa kuwaondoa wakazi wa Sinza na kuwaleta wengine. Wamiliki wa sasa wataendelea kuwa wamiliki wa mali zao,” amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo amesema mgogoro uliojitokeza unatokana zaidi na udhaifu wa mawasiliano katika hatua za awali za mashauriano.
Amesema maoni yatakayokusanywa katika mchakato mpya yanapaswa kuzingatiwa katika mpango wa mwisho, akisisitiza kuwa haki za wananchi zitalindwa kwa mujibu wa sheria.
Awali, Mei 28, 2026, Dk Akwilapo aliliambia Bunge kuwa Serikali imeanza kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya uendelezaji wa maeneo ya Sinza na Msasani chini ya Mpango wa Urekebishaji wa Ardhi (Land Re-adjustment Programme).
Alisema mpango wa Sinza unalenga kuongeza thamani ya uwekezaji kupitia matumizi mchanganyiko ya ardhi na kuruhusu ujenzi wa majengo ya ghorofa mbili hadi 20 kulingana na uwezo wa eneo husika.