Mwanza. Zaidi ya watu 500 wamebainika kuwa na ugonjwa wa homa ya ini mkoani Mwanza huku Serikali ikitangaza hatua za haraka kukabili ugonjwa huo.
Akitoa taarifa kwa Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Zijue Namba Zako’ Mei 4, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema ugonjwa huo ni tatizo kubwa mkoani humo na Kanda ya Ziwa ingawa wananchi wengi hawana elimu ya kutosha.
“Mpaka Aprili 2026, watu 523 wamebainika wana maambukizi ya homa ya ini B… idadi hiyo ni kubwa sana na wameshaanza dawa kwa sababu matibabu yake yanapatikana, na watu 78 wana homa ya ini C,” amesema Mtanda.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure, Dk Bahati Msaki akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Zijue Namba Zako inayolenga kuhamasisha wananchi kujua viashiria muhimu vya afya zao iliyozinduliwa kitaifa katika hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza.
Kwa mujibu wa wataalamu, homa ya ini B na C ni magonjwa yanayoathiri ini lakini yanatofautiana kwa namna ya maambukizi na kinga.
Homa ya ini B huenea kupitia damu, ngono zembe na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua, huku ikiwa na chanjo inayoweza kuzuia maambukizi.
Kwa upande wa homa ya ini C, huenea zaidi kupitia damu hasa matumizi ya sindano au vifaa visivyo salama, na hadi sasa haina chanjo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeeleza kuwa itaongeza nguvu katika kampeni za uelimishaji, upimaji na chanjo ili kudhibiti ugonjwa huo ambao umeendelea kuwa tishio katika jamii.
Akizindua kampeni hiyo, Mchengerwa amesema bado ugonjwa wa homa ya ini haujapewa uzito unaostahili licha ya kuwa hatari.
“Ukweli ni kwamba ugonjwa huu bado hatujauzungumza kwa kina, lakini ni ugonjwa hatari sana ambao mategemeo yangu kwa Katibu Mkuu (Seif Shekalaghe) na timu yako mtajipanga vizuri namna mtakavyokwenda kuuzungumza.
“Nendeni mkatafute fedha kupitia wadau wa maendeleo ili Watanzania tukawapime ugonjwa wa ini… wale tutakaowakuta hawajaathirika tuweze kuwapatia chanjo. Tujipange, natambua eneo hili linahitaji fedha nyingi,” ameagiza.
Amesema wizara itaangalia namna ya kuanza kutenga fedha za awali hata kama hazijawekwa kwenye bajeti ya 2026/27, akisisitiza kuwa Serikali pekee haiwezi kumudu gharama zote bila ushirikiano wa wadau wa maendeleo.
Baadhi ya wataalamu wa afya na wananchi waliofika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kushuhudia uzinduzi wa kampeni ya Zijue Namba Zako, iliyozinduliwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
Kampeni ya ‘Zijue Namba Zako’
Mchengerwa amesema kampeni hiyo inalenga kujenga uelewa mpana kwa jamii na kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu afya zao.
“Kampeni hii si kampeni ya kupima tu. Ni kampeni ya kuamsha dhamira… wajue hali zao, wachukue hatua mapema na wawe sehemu ya kulinda afya zao wenyewe… kinga ni bora kuliko tiba,” amesema.
Amesema kupitia kampeni hiyo, Serikali inalenga kujenga utamaduni mpya ambapo wananchi watakuwa wanapima afya zao kabla ya kuugua.
“Kupitia kampeni hii, tunataka kujenga utamaduni mpya wa afya… mwananchi hapimi afya kwa sababu ameanguka, bali kwa sababu anataka kuendelea kusimama… kujua namba zako ni hatua ya kwanza ya kujilinda,” ameeleza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema kupitia kampeni hiyo, wananchi wanahimizwa kufahamu viashiria muhimu vya afya zao ikiwemo shinikizo la damu, sukari, uzito, mzunguko wa kiuno, mafuta kwenye damu na mapigo ya moyo.
“Hizo ni namba gani? Kwanza ni shinikizo la damu chini ya 120 kwa 80, sukari ya damu chini ya 5.6, uzito 18.5 mpaka 24.9, mzunguko wa kiuno chini ya sentimita 94 kwa mwanaume na 80 kwa mwanamke,” amesema.
Na kuongeza, “Watu wengi watashangaa hii imefanyiwa tafiti kubwa sana… ukiwa na kiuno mwanamke zaidi ya 80 una hatari ya kupata magonjwa ya moyo na yasiyoambukiza.”
Amesema pia wananchi wanapaswa kufahamu viwango vya mafuta kwenye damu na mapigo ya moyo ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
“Maana nyingine ya ‘jua namba yako’ ni kujua mafuta yako ndani ya damu ambayo yanatakiwa kuwa 5.0 na jua mapigo ya moyo 60 mpaka 100,” amesema.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Zijue Namba Zako inayolenga kuhamasisha wananchi kujua viashiria muhimu vya afya zao iliyozinduliwa kitaifa katika Hospitali ya Sekou Toure mkoani Mwanza.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ndilo lililosukuma kuanzishwa kwa kampeni hiyo, akibainisha kuwa watu wengi wanaishi na magonjwa bila kujijua.
“Kidunia, mwaka 2020/21 wananchi waliokuwa wameugua magonjwa yasiyoambukiza walikuwa milioni 5.1, lakini kwa mwaka jana wamefika milioni 6.9… lakini wengi walikuwa hawafahamu… hawajijui kabisa.
“Ndani ya nchi yetu asilimia 41 ya vifo vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza, kwa hiyo ukiwa na watu 10, watu wanne wanakufa kwa sababu ya magonjwa haya… lakini duniani katika watu 100, watu 74 wanakufa kwa magonjwa haya,” amesema.
Ameonya kuwa magonjwa hayo sasa yanaathiri zaidi vijana walio katika umri wa kufanya kazi kuanzia miaka 18 hadi 45.
“Ugonjwa wa kiharusi sasa hivi umeongezeka kwa kiwango kikubwa sana… sisi kwetu wanapatikana watu wa miaka 18 mpaka 45,” amesema.
Ujenzi wa jengo la ghorofa tisa Sekou Toure
Akitoa taarifa kwa Waziri, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Bahati Msaki amesema jengo hilo litajumuisha huduma za dharura, wagonjwa wa nje na uangalizi maalum.
Amesema Serikali kwa kuanzia imetenga Sh5 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya mradi huo, huku sehemu ya fedha ikiwa tayari imeshatolewa katika miaka ya nyuma.
Ili kuanza kwa ujenzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameomba kibali cha ujenzi kwa wizara hiyo huku Waziri Mchengerwa akiagiza mchakato wa ujenzi huo kukamilika haraka ili hospitali hiyo iweze kutoa huduma zote za kibingwa ndani ya mkoa huo.