Dar es Salaam. Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta) umemkabidhi tuzo Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Tamali Vullu, aliyeshinda katika sherehe za Mei Mosi.

Sherehe hizo zilifanyika wiki iliyopita mkoani Njombe, ambapo, pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mgeni rasmi, aliwatunuku hati ya mfanyakazi bora wa mwaka 2025/26 baadhi ya wafanyakazi kutoka vyama vinavyounda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), waandaaji wa sherehe hizo.

Kwa upande wa Jowuta, jumla ya washindi sita walitangazwa, akiwemo Tamali aliyeshinda kipengele cha mfanyakazi bora kutoka Mkoa wa Dar es Salaam.

Hafla ya kukabidhi tuzo hiyo, iliyojumuisha cheti na fedha taslimu, imefanyika leo, Mei 5, 2026, katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na wafanyakazi wenzake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa Jowuta, Seleman Msuya, amesema katika kinyang’anyiro hicho waandishi sita walioteuliwa, wengi wao waliwahi kufanya kazi MCL.

Akizungumzia ushindi wa Tamali, amesema sifa mojawapo iliyomtofautisha ni nidhamu katika utendaji wa kazi, akibainisha kuwa wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu.

Aidha, Msuya amewahimiza wafanyakazi wa Mwananchi kujiunga na chama hicho, ili kuongeza nguvu ya pamoja katika kutetea maslahi yao ndani ya sekta ya habari.

“Njooni Jowuta, siyo sehemu hatari, bali ni mahali salama. Sisi ni wamoja, na chama hiki kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Msuya.

Naye Mwenyekiti wa Jowuta, Musa Juma, amesema utoaji wa tuzo hizo ni mwanzo wa jitihada za kuthamini mchango wa wafanyakazi wa vyombo vya habari, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Kwa upande wake, Tamali ameishukuru Jowuta kwa kutambua mchango wake, akisisitiza kuwa tuzo hiyo si yake binafsi, bali ni ya wafanyakazi wote wa MCL.

“Tuzo hii iwe chachu ya kuongeza bidii kwa wafanyakazi wenzangu ili tuendelee kuleta matokeo chanya katika jamii,” amesema Tamali, ambaye ni Mhariri Msanifu.

Aidha, amewahamasisha waandishi wengine kujiunga na Jowuta ili wanufaike na fursa mbalimbali, ikiwemo mafunzo ya kitaaluma na ulinzi wanapokumbana na changamoto katika kazi zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *