Dodoma. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameagiza kusiwe na ukataji wa maji bila sababu za msingi, na wateja wapewe taarifa mapema kabla ya huduma hiyo kukatwa.
Aweso amesema hayo leo Jumanne Mei 5, 2026, wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma.
Hata hivyo, kati ya Sh1.12 trilioni zilizoombwa katika bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2026/27; katika vipaumbele saba, Sh1.04 trilioni zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ni asilimia 93 ya fedha zilizoombwa.
Akizungumzia katakata ya maji, Aweso amesema Watanzania hawataki bla bla ya maneno bali wanataka maji.
Mbali na hilo, Aweso amepiga marufuku ubambikizaji wa ankara za maji na kuagiza wote waliokatiwa maji warudishiwe mara moja na utaratibu upangwe jinsi ya kufanya malipo.
“Huduma ya maji lazima iwe endelevu, siyo leo kuna maji kesho hakuna maji, hakuna kukata maji weekend na hakuna kukata maji sikukuu, mteja kabla hajakatiwa maji apewe taarifa,” amesema Aweso.
Waziri ameagiza pia maunganisho ya maji yafanyike ndani ya siku saba na kwamba, wateja wote waliokatiwa maji na wenye faini wafike kwenye mamlaka za maji wapewe utaratibu wa kurejeshewa maji ili tabasamu lao lidumu.
“Habari ya kubambakizia watu bili za maji, hizo zilipendwa, kutafuta mivujo kwa macho zilipendwa, tumieni mita janja ambazo ni suluhisho, lakini tekelezeni mkakati wa kuharakisha ufungaji wa dira za maji za malipo kabla wa mwaka 2026–2030 ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli,” amesema Waziri Aweso.
Ametaja ufungaji wa dira hizo kwamba utasaidia kuondoa malimbikizo ya madeni, kupunguza malalamiko ya ankara bambikizi na kudhibiti matumizi holela ya maji.
Matumizi, vipaumbele vya bajeti
Aweso amesema bajeti ya maji ya Sh1.12 trilioni kwa mwaka 2026/27 imeongezeka ikilinganishwa na bajeti ya Sh898.2 bilioni ya mwaka 2025/26 huku kazi kubwa ikielekezwa katika mkakati wa kuimarisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi, sambamba na kuboresha huduma za usafi wa mazingira nchini.
Aweso amesema Sh80.7 bilioni ambayo ni asilimia 7 ndizo zitakuwa kwenye matumizi ya kawaida.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza bungeni leo Jumanne Mei 5, 2026 wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake.
Bajeti ya 2026/27 imekwenda sambamba na ongezeko la fedha za maendeleo ambazo zimetoka Sh824 bilioni kwa mwaka 2025/26 hadi kufikia mwishoni mwa Aprili 2026, zaidi ya asilimia 83 ya bajeti hiyo ilikuwa ilishapokewa na kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, vipaumbele vyake ni kuandaa Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji ambao utatoa mwongozo wa muda mrefu wa usimamizi, uendelezaji, matumizi na uwekezaji katika rasilimali za maji nchini.
Aweso amesema sekta ya maji itakuwa na msingi mmoja wa kupanga miradi mikubwa kwa ajili ya matumizi ya maji ya wananchi na sekta za kiuchumi.
“Kipaumbele kingine ni uandaaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, Wizara itaendelea na utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji inayolenga kutumia vyanzo vikuu vya maji ikiwamo maziwa, mito mikubwa, maji chini ya ardhi na mabwawa ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma toshelevu ya maji safi na salama,”amesema Aweso.
Amesema Tanzania haina umaskini wa vyanzo vya maji, kwa kuwa, ina Ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, Ziwa Tanganyika lina asilimia 16 ya maji yote duniani pamoja na mito mingi.
Hata hivyo, amesema wizara itajenga na kukarabati mabwawa 33, kufanya usanifu wa mabwawa mapya 34, kufanya tathmini ya athari za kimazingira kwa mabwawa mawili na kuendelea na uchimbaji wa visima virefu 300 katika maeneo yenye upungufu wa vyanzo vya maji.
Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza uhakika wa maji katika maeneo yenye changamoto ya vyanzo vya kudumu, kupunguza athari za ukame na mabadiliko ya tabianchi katika kuweka msingi wa kutosha wa maji kwa ajili ya wananchi, mifugo na kilimo.
Aweso amesema katika mwaka 2026/27, wizara itakamilisha miradi ya maji 992 vijijini, miradi ya maji 196 mijini, pamoja na miradi ya usafi wa mazingira 26.
Kuhusu miradi ya vijijini amesema watapeleka huduma ya maji katika vijiji 1,575 vilivyobaki katika ya jumla ya vijiji 12,333.
“Kati ya vijiji hivyo, vijiji 10,758 vina huduma ya maji, hivyo bado vijiji 1,575 ambavyo vinaonekana kama doa kwenye shati jeupe, hivyo, wizara itahakikisha vijiji vyote 1,575 vinapata maji kabla ya mwaka 2030,” amesema Aweso.
Hata hivyo, katika bajeti ya mwaka ujao, amesema wizara itapeleka maji katika vijiji 314 ambavyo ni sehemu ya vijiji 1,575 na kuomba wabunge waanzishe kampeni na ligi mbalimbali za kumaliza vijiji hivyo katika maeneo yao.
Amesema wizara itaweka msukumo katika kukamilisha Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji utakaotoa mwongozo wa muda mrefu wa usimamizi, uendelezaji, matumizi na uwekezaji katika rasilimali za maji nchini.
Aweso amesema usalama wa maji ni usalama wa chakula, wa nishati na ni maendeleo ya viwanda, hivyo usalama wa maji ni usalama wa Taifa akieleza kuwa mitambo iliyonunuliwa kwa ajili ya kuchimba maji iko ‘site’ kwa ajili ya kuongeza ufanisi.
Upotevu wa maji
Kuhusu upotevu wa maji amesema wizara itaendelea kuimarisha udhibiti wa upotevu wa maji kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwamo mifumo ya usomaji mita kwa njia ya kielektroniki.
Ameagiza kuwashitaki watu wanaoharibu miundombinu na wezi wa maji ili kuhakikisha miundombinu ya maji inayojengwa inakuwa himilivu akitoa angalizo kuwa, upotevu wa maji mifukoni sasa mwisho.
Katika hotuba yake, Waziri Aweso amesema Serikali imejipanga kuhakikisha tatizo la maji jijini Dar es Salaam halijirudii baada ya Mto Ruvu kukauka kati ya Novemba na Desemba 2025.
Amesema Serikali imefanya uchambuzi na kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kununua pampu za maji kwa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini pamoja na kuchimba visima vya ziada.
Aidha, amesema ujenzi wa Bwawa la Kidunda unaendelea huku mpango wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji ukiwa sehemu ya suluhisho la muda mrefu kwa jiji hilo.
“Niseme kwa ufupi, never ever again. Nawashukuru wana Dar es Salaam kwa uvumilivu wao,” amesema Aweso.
Ameeleza kuwa, kwa sasa Mto Ruvu umejaa maji na Serikali imetoa pampu za Sh8 bilioni kuboresha huduma hiyo. “Nawaelekeza Dawasa (Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam), sitaki kusikia kisingizio cha watu kukosa maji,” amesema.