Dar es Salaam. Rais wa Kenya, Dk William Ruto ameeleza haja kwa Tanzania na Kenya kuaminiana ili kuchochea maendeleo kwa watu wa nchi hizo huku zikiimarisha mtengamano na kupanua biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Pia, amesisitiza kuhusu dhana ya uongozi, kwamba ni zaidi ya yote, ni heshima inayokuja na wajibu, inayowataka kuheshimu maneno yao, kutimiza ahadi wanazozitoa na kuilinda imani ambayo watu wamewapatia.

Ruto amebainisha hayo leo Mei 5, 2026 wakati akilihutubia Bunge la Tanzania jijini Dodoma, akiwa ni Rais wa pili wa Kenya kulihutubia, baada ya Daniel Arap Moi aliyefanya hivyo Novemba 12, 2002.

Rais wa Kenya, Dk William Ruto katika ziara hiyo ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania, amekutana na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan, washuhudia pamoja utiaji saini mikataba minane na baadaye amelihutubia Bunge.

Kiongozi huyo wa Kenya amewasili bungeni saa 5:30 asubuhi na kukagua gwaride rasmi katika viwanja vya Bunge kabla ya kurejea katika jukwaa maalumu lililoandaliwa katika viwanja hivyo, kisha nyimbo za Taifa za Tanzania na Kenya zikapigwa.

Katika hotuba yake iliyodumu kwa takriban saa moja kuanzia saa 6:03 mchana hadi saa 6: 59 mchana, Rais Ruto ameweka msisitizo kwenye suala la kutoaminiana baina ya Kenya na Tanzania ambako kumekuwa kukiathiri shughuli za kiuchumi baina ya mataifa hayo.

Amesema kwa muda mrefu, uhusiano kati ya nchi majirani umekuwa ukichangiwa na ushindani, mashaka na uhasama, hali ambayo imegawanya masoko, kudhoofisha sauti yao na kuzuia maendeleo ya pamoja.

Amebainisha kwamba roho hiyo ilizaa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967 na ingawa ilivunjika mwaka 1977; ilijengwa upya kupitia mazungumzo na uongozi wa busara na hatimaye kufufuliwa tena mwaka 1999.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Samoei Ruto wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa katika viwanja vya Gwaride Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma Mei 5, 2026.

“Leo, Jumuiya imefufuliwa ikiwa imara na imepanuka, lakini msingi wake unabaki uleule: ushirikiano unaokua kati ya mataifa yetu, unaoelezwa si kwa kukosekana kwa changamoto, bali kwa uwezo wetu wa kuzishinda na kusonga mbele pamoja katika kutafuta maendeleo na nguvu ya pamoja,” amesema.

Ruto amesisitiza kwamba kwa kuimarisha mtengamano wa EAC, kupanua biashara na kuwekeza katika miundombinu ya pamoja, watatengeneza ajira, ujasiriamali na heshima kwa kizazi hiki.

Vilevile, amesema wanakabiliana na changamoto za wakati, kuhakikisha kwamba nguvu na uwezo wa vijana unatumika katika maendeleo, utulivu na ustawi wa pamoja.

Amebainisha kwamba Kenya na Tanzania zinategemeana kwa kiwango kikubwa.

“Wakenya si maadui wa Tanzania na Watanzania si maadui wa Kenya; adui wetu sote ni pale ambapo hatuna mali, hatuna nafasi za ajira na hatuna fedha, hiki ndicho kinachotutesa,” amesema.

Amesema biashara ya pande mbili ilifikia takribani dola za Marekani 860 milioni mwaka 2025, na inaelekea kufikia dola 1 bilioni mwaka huu, ishara ya fursa inayokua.

“Ushirikiano katika uwekezaji unasimama kama nguzo kuu ya uhusiano wetu wa pande mbili. Biashara za Kenya zimewekeza zaidi ya dola 1.7 bilioni nchini Tanzania, zikizalisha ajira, kuendeleza uhamishaji wa ujuzi, na kuimarisha uwezo wa ndani katika sekta muhimu zikiwemo viwanda, nishati, usafirishaji, huduma za kifedha na kilimo.

“Wakati huohuo, uwekezaji wa Watanzania nchini Kenya, ambao sasa unakadiriwa kuwa zaidi ya dola 336 milioni, unaendelea kukua kwa kasi; ukichochea ajira, kuimarisha uhusiano wa kampuni, na kukuza ukuaji wa pamoja.

Amesisitiza kwamba uwekezaji mpya wa kimkakati kutoka kwa wawekezaji wa Tanzania nchini Kenya, natarajia thamani hii ya uwekezaji kuongezeka zaidi ya mara mbili kufikia mwisho wa mwaka huu.

Azungumzia ya Rostam

Ruto amesema kuna wakati mfanyabiashara, Rostam Aziz alimtembelea, akamwambia anataka kuwekeza kupitia Taifa Gas huko Mombasa, Kenya lakini alikuwa akizungushwa, hivyo aliamua kuwaambia Wakenya kwamba mwekezaji kutoka Tanzania ni mwenzao kwa kuwa anawaletea fedha.

Tunachukua muda mrefu sana kutafuta wawekezaji, lakini kasumba ambayo imekuwepo ni kwamba mwekezaji lazima awe mweupe (mzungu), lazima awe foreigner (mgeni), lakini mambo sivyo tena.

Mfanyabiashara wa Tanzania, Rostam Aziz akizungumza wakati wa Kongamano la biashara kati ya Kenya na Tanzania lililofanyika  jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais William Ruto

“Tuna kampuni 500 zinazowekeza hapa Tanzania. Nimefungua milango kwa kampuni za Tanzania zije ziwekeze Kenya. Ushirikiano wa kampuni na wajasiriamali hususani katika uchakataji wa mazao ya kilimo zinaendelea kustawi kutokana na sera zinazotabirika,” amesema.

Amesisitiza kwamba hayo yanaashiria kwamba sekta binafsi imekuwa ndiyo mhimili katika utengamano wa kikanda.

Dhana ya uongozi

Ruto amebainisha kwamba uongozi, zaidi ya yote, ni heshima inayokuja na wajibu, inayohitaji waheshimu maneno yao, kutimiza ahadi na kuendeleza imani ambayo wananchi wamewapatia.

Amebainisha kwamba kipimo cha kweli cha uongozi si nafasi wanazoshika, bali ni matokeo wanayoyaleta, na ujasiri wanaouonyesha katika kuyatekeleza.

“Nchini Kenya leo, tunafanya maendeleo ya makusudi katika kupanua huduma za afya, kuimarisha elimu, na kutoa makazi kwa kiwango kikubwa kama sehemu ya dhamira pana ya heshima na ustawi wa pamoja. Juhudi hizi zimehitaji ujasiri; ujasiri wa kufanya uamuzi mgumu kwa ajili ya manufaa ya taifa kwa muda mrefu,” amesema.

Ameongeza kuwa uongozi si kufuata mkumbo wa wengi, bali ni kuongoza kwa msimamo wa imani, hata pale njia inapokuwa ngumu.

“Ni katika ari hii ambayo sasa tunapaswa kuongoza nje ya mipaka yetu, kwa sababu uamuzi tunaofanya kama mataifa yataashiria nguvu tunayojenga kama kanda, na ushawishi tunaoutoa kama bara,” amesema Rais huyo.

Ruto pia amesema ipo haja ya kuoanisha sekta ya mawasiliano ya simu katika nchi za Afrika Mashariki ili kupunguza gharama na kurahisisha mawasiliano ya kibiashara.

Amesema wawekezaji katika sekta ya mawasiliano wanapaswa kushirikiana kuunda mfumo mmoja utakaofanya simu za kuvuka mipaka kuwa sawa na za ndani, hatua ambayo amesema itahusisha nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.

“Tunataka simu kutoka Kenya kwenda Tanzania iwe kama simu ya ndani, na simu kutoka Tanzania kwenda Kenya iwe kama simu ya ndani kwa sababu sisi ni wamoja,” amesema.

Wabunge wachangia

Baada ya kuhitimisha hotuba yake, Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu alitoa nafasi kwa wabunge wachache kuchangia hotuba ya Rais Ruto, jambo ambalo lilishangiliwa na wabunge kwa kugonga meza.

Mzungumzaji wa kwanza alikuwa Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso ambaye amempongeza Rais Ruto huku akisema dunia ya sasa inataka viongozi watakaoleta maendeleo, akisema viongozi wa Tanzania na Kenya ni viongozi wa matokeo.

“Kwa haya uliyoyazungumza Rais Ruto, hakika viongozi hawa (Samia na Ruto) watakumbukwa katika suala zima la maendeleo,” amesema Aweso ambaye pia ni Waziri wa Maji na mapema asubuhi aliwasilisha hotuba yake ya bajeti.

Kwa upande wake, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela amesema jambo kubwa analolitaka Rais Ruto, katika hotuba yake, ni Tanzania na Kenya kuendelea kushirikiana ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Amesema kwamba Watanzania wanawapenda Wakenya na kwamba hawana malalamiko yoyote dhidi yao.

“Kama kweli tunataka maendeleo, tuendelee kupendana kama nyie viongozi wetu (Samia na Ruto) mnavyopendana,” amesema Kilango.

Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Samoei Ruto akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mei 5, 2026 Jijini Dodoma.

Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema jambo kubwa alilolizungumza Rais Ruto kwenye hotuba yake ni kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wazalishe mali wenyewe kwa kutumia rasilimali zao.

“Umezungumza kitu ambacho Mwalimu Nyerere alikizungumza kabla hajafariki, alisisitiza kwamba maendeleo yetu tutajiletea sisi wenyewe, kwa hiyo alisisitiza tutumie rasilimali tulizonazo kujiletea maendeleo,” amesema.

Naye, Mbunge wa Ikundi Magharibi, Elibariki Kingu amesema maneno ya Ruto yanawakumbusha ndoto za Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Jomo Kenyatta wa Kenya, ambazo zinaishi ndani ya viongozi wa mataifa hayo.

“Ukifika Kenya waambie Watanzania tunawachukulia Wakenya kama kaka na dada zetu, mipaka haiwezi kututenganisha. Tunawapongeza sana viongozi wetu kwa kazi kubwa mnayofanya ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema Kingu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *