Miaka kumi iliyopita, mwezi kama huu wa Mei, niliandika katika safu hii kwamba Mji Mkongwe wa Zanzibar unalia bila ya kupata wa kuutuliza. Wakati huo, nilielezea jinsi mvua za masika zilivyosababisha baadhi ya nyumba zilizokuwa katika hali mbaya kuporomoka na kusababisha vifo vya watu.

Tangu kipindi hicho, kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu mipango kabambe ya kukarabati majengo hayo au kubomoa yaliyochakaa na kujenga mapya yenye kuendana na mwonekano wa kihistoria wa Mji Mkongwe.

Hata hivyo, maneno yamekuwa mengi kuliko vitendo. Kila msimu wa mvua, iwe ni masika au vuli, habari za nyumba kuporomoka zimeendelea kusikika.

Ni kweli kwamba baadhi ya juhudi za ukarabati zimefanyika, lakini kasi yake ni ndogo mno kulinganisha na ukubwa wa tatizo. Hali hii inaongeza hatari ya kupoteza maisha na mali, hasa majengo ya ghorofa yanapoporomoka.

Mji Mkongwe una majengo mengi yaliyojengwa kwa kutumia mawe, udongo, chokaa na boriti, baadhi yao yakiwa na zaidi ya miaka 300. Kwa sasa, mengi yamechakaa na yako katika hatari ya kuporomoka wakati wowote, iwe ni kipindi cha jua au mvua.

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakazi wengi walilazimika kuhama nyumba hizo. Baadhi zimebaki kama magofu, huku zingine zikiwekewa mihimili ya muda (mwega) zaidi ya miaka 20 iliyopita ili kuzuia zisiporomoke. Hata hivyo, hakuna dalili za dhati za ukarabati au ujenzi mpya.

Kupita karibu na majengo hayo ni hatari kwa maisha ya watu na pia huweka katika hatari majengo jirani yanapoporomoka.

Miongoni mwa majengo yaliyopata uharibifu ni yale yaliyokuwa makazi ya masultani wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya 1964, pamoja na sehemu ya jengo la Beit el Ajaib (Nyumba ya Ajabu), lililoporomoka Desemba 2020.

Kulikuwa na taarifa kwamba Oman ilijitolea kusaidia ukarabati wa Beit el Ajaib, jengo lenye thamani kubwa ya kihistoria na kivutio kikubwa cha utalii.`

Jengo hilo lina nakshi za kipekee zinazoakisi tamaduni za Kiarabu, Kiswahili, Kiajemi, Kihindi na hata mtindo wa Baroque wa Ulaya.

Ni moja ya alama muhimu za Zanzibar kimataifa, sambamba na karafuu, upole na ukarimu wa watu wake. Ingawa fedha ziliwahi kutolewa, haijulikani wazi iwapo mpango huo unaendelea au umesimama.

Ilielezwa kuwa ukarabati huo ungechukua takriban miaka mitatu, lakini hadi sasa hakuna dalili za kukamilika kwake katika siku za karibuni. Wakati huo huo, kila msimu wa mvua unaendelea kuleta athari.

Hivi karibuni, jengo la ghorofa mbili lililoko Kokoni karibu na soko kuu liliporomoka, ingawa kwa bahati nzuri hakuna vifo wala madhara kwa binadamu yaliyotokea.

Kila msimu wa mvua unapomalizika na kusababisha maafa, ahadi hutolewa kwamba mipango ya ukarabati ipo njiani. Hata hivyo, haijulikani ni lini hatua madhubuti zitachukuliwa.

Ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar kulinda urithi huu wa kipekee. Mji Mkongwe una vichochoro vya kuvutia na takriban nyumba 1,000 na zaidi ya 70 ni za ibada, ikiwamo misikiti 64.

Baadhi ya nyumba zilizoachwa sasa zimegeuka makazi ya wanyama kama mbwa na paka, maficho ya wahalifu na maeneo ya vitendo viovu.

Zamani, Mji Mkongwe ulikuwa na mandhari ya kuvutia; njiwa waliotapakaa juu ya mapaa, kasuku wenye rangi ang’avu waliokuwa wakiongea na kuwaburudisha wapita njia na hata tausi waliotembea kwa madaha katika bustani za nyumba.

Takwimu za mwishoni mwa miaka ya 1950 zinaonyesha kuwa kulikuwa na kasuku wapatao 200, tausi karibu 100 na zaidi ya njiwa 10,000.

Aidha, maeneo mengi yalijulikana kwa harufu nzuri ya asumini, vikuba na udi. Haya yote yamepotea, sambamba na baadhi ya majengo ya kihistoria.

Leo, majengo haya yako katika hali ya mahututi. Kama mgonjwa anavyohitaji oksijeni, majengo haya yamewekewa mihimili ya muda ili ‘yaendelee kupumua,’ lakini yanahitaji matibabu ya haraka na ya kudumu.

Ni wajibu wa serikali kuweka bajeti maalum kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Mji Mkongwe. Pia, sehemu ya mapato yatokanayo na utalii itumike kuhifadhi urithi huu.

Zaidi ya hapo, ni vyema kuanzishwa Mfuko wa Hifadhi ya Mji Mkongwe, kwa kutenga asilimia 2 hadi 3 ya mapato kutoka bandari, maegesho, leseni za biashara na hoteli za kitalii zilizopo eneo hilo.

Wananchi wa Zanzibar wanapaswa kushirikiana kikamilifu kuhakikisha kuwa urithi huu wa kihistoria haulindwi tu, bali pia unadumishwa kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *