
Dar es Salaam. Wakati makali ya bei za petroli, dizeli na taa yakiendelea kung’ata nchini, Serikali imeweka ruzuku ya Sh259 kwa kila lita moja ya dizeli ili kupunguza makali ya bei yake.
Hilo limefanyika kwa kile kilichoelezwa kuwa, mafuta hayo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii zikiwamo za uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma.
Hata hivyo, wakati petroli na dizeli zikiwa na ongezeko la chini ya Sh500 kwa kila lita, watumiaji wa mafuta ya taa nchini wataumia kutokana na ongezeko la Sh993 kwa kila lita.
Kwa mujibu wa taarifa ya bei kikomo za mafuta zitakazotumika Mei mwaka huu iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Maji (Ewura) jana Jumanne Mei 5, 2026, ongezeko hilo linaendelea kuchagizwa na vita inayoendelea Mashariki ya Kati ikihusisha Iran na Marekani iliyoanza Februari mwaka huu.
Vita hiyo imesababisha mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya uzalishaji, uhifadhi na usafishaji wa mafuta vikiwamo visima vya uzalishaji, maghala ya kuhifadhi na viwanda vya kusafisha mafuta, hivyo kuathiri uwezo wa uzalishaji.
Hali hiyo pia imesababisha upungufu wa mafuta katika soko la dunia na kuchochea ongezeko la bei za bidhaa hiyo kwa kiasi kikubwa.
Pia, kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa duniani, kumeathiri upatikanaji na usambazaji wa mafuta duniani na kuongeza gharama za usafirishaji pamoja na bima za meli za mafuta.
“Hali hii imepelekea kupungua kwa mzunguko wa meli, usafirishaji wa mafuta kupitia njia hiyo umeshuka kwa kiwango kikubwa na kusababisha msongamano wa meli, ucheleweshaji wa mizigo na kuongezeka zaidi kwa bei za mafuta katika soko la dunia,” inaeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Geral Maganga.
Kufuatia hali hiyo, sasa bei ya mafuta ya petroli ndani ya Jiji la Dar es Salaam imeongezeka kwa Sh295 hadi kufikia Sh4,115 kwa rejareja kutoka Sh3,820 iliyokuwapo Aprili mwaka huu.
Mafuta ya dizeli ndani ya Dar es Salaam sasa yatauzwa lita moja kwa Sh4,248 kutoka Sh3,806 iliyokuwapo Aprili mwaka huu ikiwa ni ongezeko la Sh442.
Kwa upande wa mafuta ya taa yatanunuliwa kwa Sh4,677 kutoka Sh3,684 iliyokuwa ikitumika Aprili mwaka huu ikiwa ni ongezeko la Sh993.
Kwa upande wa watumiaji wa petroli inayopitia katika Bandari ya Tanga, wataugulia maumivu kama wenzao kwa kuwa, sasa lita moja itauzwa kwa Sh4,176 kutoka Sh3,881 ikiwa ni ongezeko la Sh295 kwa kila lita.
Wanaotumia mafuta ya dizeli yanayopita katika bandari hiyo sasa watanunua lita moja kwa Sh4,309 kutoka Sh3,867 Aprili mwaka huu ikiwa ni ongezekoo la Sh442 kwa lita.
Wale wa mafuta ya taa nao watalazimika kuongeza Sh993 kwa kila lita baada ya mafuta kufikia Sh 4,738 kutoka Sh3,745 iliyokuwapo Machi mwaka huu.
Wakazi wa Mtwara watatumia Sh4,207 kununua lita moja ya mafuta kutoka Sh3,912 iliyokuwa ikitumika Aprili mwaka huu ikiwa ni ongezeko la Sh295.
Mafuta ya dizeli nayo yamefikia Sh4,341 kutoka Sh3,898 iliyokuwapo Aprili mwaka huu ikiwa ni ongezeko la Sh443 huku mafuta ya taa yakifikia Sh4,770 kwa lita kutoka Sh3,777 iliyokuwapo Aprili mwaka huu ikiwa ni ongezeko la Sh993.
“Kwa kuwa Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka nchi za Mashariki ya Kati, athari za mabadiliko hayo ya kimataifa zimejitokeza moja kwa moja katika soko la ndani. Ongezeko la bei linaakisi mwenendo wa soko la dunia, bei za mafuta na gharama za usafirishaji zimekuwa zikiongezeka kufuatia athari za vita hiyo,” inaeleza taarifa hiyo.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini muda wote na kuendelea kuhakikisha bei zinaendelea kuwa himilivu ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza zikiwamo zile za kiuchumi na kijamii.
Haya yote yanashuhudiwa wakati bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la Kiarabu ziliongezeka kwa asilimia 71,117 na 122 Aprili 2026 kutoka wastani wa Dola 71.76 za Marekani kwa pipa, Dola 85.99 kwa pipa na Dola 85.34 kwa pipa Februari 2026 kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, mtawalia.
Mgogoro huo pia umevuruga usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji inayohudumia karibu asilimia 20 ya biashara ya mafuta duniani na kusababisha ongezeko kubwa la gharama za uagizaji mafuta.
Mei 2026, gharama hizo kwa bidhaa za mafuta zilizopokewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam ziliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 5.4 kwa dizeli na asilimia 7.2 kwa mafuta ya taa.