Ziara za wiki hii za Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Kenya, William Ruto nchini Tanzania zinaakisi mwelekeo mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika nyanja za diplomasia na uchumi.

Nasema hivyo kwa sababu katika wakati huu ambao mataifa yanashindana kiuchumi huku yakitafuta washirika wa kuaminika, mikutano ya viongozi wa ngazi ya juu imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga uelewano, kuimarisha uhusiano na kufungua fursa mpya za maendeleo.

Nadiriki kusema, kwa Tanzania, ziara hizi zina umuhimu wa kipekee kwa sababu zinaongeza uzito wake kama kitovu cha diplomasia katika Afrika Mashariki.

Kwa sababu kwa muda mrefu sasa Tanzania imejijengea sifa ya kuwa nchi inayotanguliza amani, utulivu na mazungumzo ya kirafiki katika kushughulikia masuala ya kikanda.

Hivyo, kupokea viongozi hawa wawili ndani ya muda mfupi ni ishara ya imani kubwa waliyonayo majirani zake. Hali hii inaimarisha nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambako ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii ni msingi wa maendeleo ya pamoja.

Kwa upande wa uchumi, wachambuzi wa masuala ya uchumi nchini wanasema ziara hizi zinafungua milango mipya ya biashara na uwekezaji.

Hata tukizingatia kuwa Kenya ni moja ya washirika wakubwa wa kibiashara wa Tanzania, huku Rwanda ikiwa ni soko muhimu linalotegemea huduma za usafirishaji kupitia Tanzania.

Hivyo, kupitia mazungumzo ya viongozi hawa, kuna uwezekano wa kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru, kurahisisha taratibu za forodha na kuboresha mazingira ya biashara kwa ujumla. Hatua hizi zitachochea ukuaji wa biashara ya mipakani na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda.

Umuhimu wa Bandari ya Dar es Salaam hauwezi kupuuzwa katika muktadha huu. Bandari hii ni lango kuu la biashara kwa nchi kadhaa zisizo na bandari, ikiwamo Rwanda. Kuboresha ufanisi wake kupitia uwekezaji katika miundombinu na teknolojia, kutasaidia kupunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mizigo.

Hivyo, ziara hizi zinaweza kuchochea makubaliano ya kuongeza ushirikiano katika matumizi ya bandari na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha usafirishaji katika ukanda.

Hali kama hiyo ipo pia katika sekta ya miundombinu, ziara hizi zinaweza kuwa chachu ya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya pamoja. Miradi hiyo ni pamoja na huu wa Reli ya kisasa (SGR), barabara kuu na miradi ya nishati ni baadhi ya maeneo yanayoweza kunufaika. Kuunganisha mifumo ya usafiri kati ya Tanzania, Rwanda na Kenya kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, kupunguza gharama za biashara na kuongeza ushindani wa kiuchumi. Aidha, ushirikiano huu unaweza kusaidia kuvutia wawekezaji wa kimataifa wanaotafuta masoko yenye mtandao mzuri wa miundombinu.

Diplomasia ya uchumi ni eneo lingine linalonufaika na ziara hizi. Tanzania ina nafasi ya kutumia mikutano hii kujitangaza kama kitovu cha uwekezaji katika ukanda.

Nasema hivyo kwa sababu Sekta za viwanda, kilimo, madini, utalii na huduma zinaweza kuvutia wawekezaji kutoka Kenya na Rwanda pamoja na mataifa mengine kuja nchini.

Kwa maana nyingine, naweza kusema uwepo wa mazingira ya kisiasa tulivu na sera zinazoboreshwa za kiuchumi, ni vivutio muhimu vinavyoweza kuongeza mtiririko wa mitaji na teknolojia.

Hata hivyo, pamoja na fursa hizi, bado kuna changamoto zinazopaswa kushughulikiwa. Urasimu, tofauti za sera za kitaifa na ucheleweshaji wa utekelezaji wa makubaliano ni baadhi ya vikwazo vinavyoweza kudhoofisha jitihada hizi.

Ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kuwa makubaliano yanayofikiwa yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi ili kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Zaidi ya hayo, ziara hizi zina mchango katika kuimarisha uhusiano wa kijamii na kitamaduni kati ya mataifa haya. Ushirikiano katika elimu, utalii na utamaduni unaweza kuimarishwa zaidi kupitia makubaliano ya kubadilishana uzoefu na rasilimali watu. Hii itasaidia kujenga mshikamano wa kikanda unaoenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa ujumla, ziara za Rais Kagame na Rais Ruto nchini zinaashiria fursa kubwa ya kuimarisha diplomasia na kuchochea ukuaji wa uchumi. Tanzania ikiwa itatumia vyema fursa hizi, inaweza kujiimarisha zaidi kama kitovu cha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda katika Afrika Mashariki.

Hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa diplomasia hii inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Hii inajumuisha kuongeza ajira, kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuboresha huduma za kijamii.

Mwandishi wa uchambuzi huu ni Mhariri wa habari za Siasa sambamba na Jarida lake ndni ya Gazeti la Mwananchi anapatikana kwa simu 0713235309

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *