Unguja. Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Ramadhani Soraga amesema ili kufanikisha utekelezaji wa mifumo ya kidijitali ni lazima izingatie mahitaji ya sekta husika.

Soraga ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Mei 6, 2026, wakati akizindua mifumo ya kidijitali ukiwamo mfumo wa malipo ya pensheni kwa wazee (PBMS) na mfumo wa ukusanyaji mapato katika vituo vya utalii (ZanExplore), kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Amesema ameridhishwa kuona mifumo hiyo imezingatia mahitaji ya sekta mbalimbali kupitia ushirikishwaji wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Mamlaka ya Serikali Mtandao (EGAZ).

Soraga amezitaka kuepuka kuwa miongoni mwa taasisi zisizokumbatia mageuzi ya kidijitali, akisisitiza kuwa mabadiliko hayo ni muhimu kwa maendeleo ya Serikali na jamii kwa jumla.

Amebainisha kuwa lengo la Serikali kwa sasa ni kuharakisha mageuzi ya kidijitali, mifumo hiyo itasaidia wazee kupata pensheni zao kwa wakati na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya utalii.

“Wakati mwingine taasisi zetu hubuni mifumo mizuri, lakini hukosa kupokewa vizuri kutokana na ukosefu wa uelewa kwa wananchi. Ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kuitangaza ili iweze kutumika ipasavyo,” amesema Soraga.

Aidha, amekiri kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya taasisi, ikiwamo viongozi kuingilia mifumo kwa masilahi binafsi, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuhujumu mifumo hiyo.

“Tutachukua hatua kwa watendaji watakaochezea mifumo kwa makusudi, na ni marufuku kwa wizara kufanya mikataba nje ya mifumo rasmi ya Serikali,” amesisitiza.

Waziri huyo pia ameagiza Mamlaka ya Serikali Mtandao kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma wa kada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuboresha ufanisi wa kazi na kuwawezesha kufanya kazi kulingana na taaluma zao.

Akifafanua kuhusu mifumo hiyo, Mkurugenzi wa EGAZ, Dk Saidi Seif amesema ni matokeo ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya Tehama kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma.

Amesema mfumo wa ukusanyaji mapato katika maeneo ya utalii utarahisisha huduma kwa watalii, kuongeza mapato ya Serikali na kuitangaza Zanzibar kimataifa.

Kwa upande wa mfumo wa PBMS, amesema utahakikisha wazee wanapata pensheni zao kwa wakati, kupunguza ucheleweshaji unaotokana na makosa ya kibinadamu, pamoja na kuimarisha uwazi katika matumizi ya fedha za umma.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kutoa mafunzo ya Tehama kwa watumishi ili kuimarisha usalama wa mifumo hiyo na kuhakikisha teknolojia inakuwa nyenzo muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Katibu mkuu wa wizara hiyo, Fatma Mabrouk amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuunganisha taasisi za umma kwenye mifumo ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma bora na kuongeza uwazi kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *