
TANZANITE Queens imeanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Cameroon, huku Kocha Mkuu, Bakari Shime, akiamini timu hiyo bado ina nafasi kubwa ya kupindua matokeo na kufuzu Kombe la Dunia Wanawake mwaka huu nchini Poland.
Tanzanite ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Cameroon kwa mabao 3-1, mechi iliyopigwa Yaounde, huku marudiano ikipangwa kuchezwa Mei 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza baada ya kuanza mazoezi, Shime alisema licha ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1, bado hawajakata tamaa kwani wana uwezo wa kupindua matokeo nyumbani.
“Malengo yetu kwenye mechi ya kwanza yalikuwa kupata ushindi au sare, lakini hata haya matokeo tuliyopata si mabaya sana. Tuna uwezo wa kubadilisha matokeo na tuna nafasi ya kushinda,†alisema Shime.
Tanzanite Queens ipo katika raundi ya nne ya kufuzu michuano hiyo, ili ifuzu Kombe la Dunia Wanawake inapaswa kushinda mabao 2-0 nyumbani.
Katika mechi zingine za kufuzu, Ghana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uganda mjini Accra, wakati Nigeria ikiifunga Malawi mabao 2-0 huko Ikenne. Ivory Coast na Benin zilitoshana nguvu kwa sare ya 1-1 jijini Abidjan.
Hii ni raundi ya nne ya kufuzu Kombe la Dunia Wanawake ambapo Tanzanite Queens ilianzia raundi ya pili ya michuano hiyo kwa kuvaana na Angola na kupata ushindi wa jumla ya mabao 7-0 baada ya awali kushinda 4-0, kisha kumalizia 3-0, ikakutana na Kenya. Katika mechi ya kwanza ugenini ililala bao 1-0, kisha kupindua meza ikiwa nyumbani ikikshinda bao moja na kusonga mbele kwa penalti 3-1.
Tanzanite itakuwa na kibarua dhidi ya Cameroon, ambayo yenyewe ilitinga hatua hii baada ya kuiondoa Botswana kwa jumla ya mabao 5-1, ikionyesha kuwa sio timu nyepesi.
Washindi wa jumla wa mechi hizo nne watajihakikishia tiketi ya kwenda kushiriki Kombe la Dunia Wanawake nchini Poland, huku Tanzanite Queens ikisaka historia ya kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo makubwa duniani.
Lakini kwa Tanzania sio mara ya kwanza kwani mwaka 2022 timu ya taifa ya wasichana chini ya miaka 17 ilifuzu Kombe la Dunia Wanawake U17 yaliyofanyika India na kuishia robo fainali, huku katika harakati za kufuzu, iliiondosha Cameroon kwa jumla ya mabao 5-1, ikishinda ugenini 4-1, kisha ushindi wa 1-0 nyumbani, mechi iliyopigwa New Amaan Complex, Zanzibar.