Dar es Salaam. Ni mcheshi na mwenye upendo, hii ndiyo sura ya James Temba (24) iliyoelezwa na waombolezaji, huku Mchungaji wa Jimbo la Kati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frank Kimambo, akieleza kuwa alipata wakati mgumu kuandaa mahubiri kutokana na uzito wa tukio hilo.
Mchungaji huyo amesema aliyaandaa mahubiri kwa mara ya kwanza na kuyachana kutokana na kusikia sauti ya Mungu kwamba ameyaandaa kwa hisia kali.
Awamu ya pili, baada ya kuandaa mahubiri, Mchungaji Kimambo alisema hakuyatumia, hivyo alimuomba Mungu ampe utulivu na ujumbe unaofaa kwa ajili ya mazishi ya Temba.
“Nimepata wakati mgumu kuandaa mahubiri, nilichana na kuandika tena na kuandika tena na kuachana nayo. Nikiongea na Mungu, nilisikia sauti kuwa mahubiri nimeandaa kwa hisia kali sana.
“Ni mara yangu ya kwanza tangu niwe mchungaji kuzika mwili usio na kichwa. Ninachojua, hata katika hili Mungu ataendelea kuwa mfariji,” alisema.
Waombolezaji wakiwa katika misa ya kumwombea marehemu James Temba kwenye Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT) Tabata Kuu Magengeni jijini Dar es Salaam.
Pamoja na hayo, waombolezaji ambao ni majirani, wanafunzi, uongozi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) alichosoma Temba, viongozi wa dini na wanajumuiya, wamemuelezea marehemu alikuwa kijana mcheshi, wakisema kifo chake ni cha maumivu.
Temba, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili IFM, aliuawa kwa kukatwa kichwa na mwili wake kupatikana Aprili 29, 2026 katika Mto Msimbazi, eneo la Kipawa, jijini Dar es Salaam, ukielea.
Wakati misa ya kumuaga ikifanyika katika kanisa la KKKT Tabata Kuu Magengeni leo Jumatano, Mei 6, 2026, na mwili wake kusafirishwa kwenda Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kwa maziko kesho Alhamisi, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imetangaza kuwashikiliwa watuhumiwa wanne kuhusiana na mauaji hayo.
Taarifa ya Polisi imewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Steven Chaka (31), ofisa maabara, mkazi wa Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Mwingine ni Anna Lema (30), mkazi wa Tabata- Chang’ombe, ambaye pia ni mfanyabiashara.
Wengine ni Twalibu Khamis (23) na na Michael John (26), wakazi wa Kigogo Kati.
“Vipo pia baadhi ya vielelezo vinachunguzwa kuhusiana na tukio hilo. Wito wa Jeshi la Polisi kwa wananchi ni kuwa watulivu ili kila aliyehusika, kulingana na ushahidi, aweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” imeeleza taarifa hiyo ya polisi.
Mchungaji na waombolezaji
Akihubiri katika misa ya kumuaga Temba, Mchungaji Kimambo ametoa muongozo kwa waombolezaji, tofauti na nyakati nyingine, akisema mwili huo hautafunguliwa kwenye jeneza wakati wa kuaga.
Waombolezaji wakiwa katika misa ya kumwombea marehemu James Temba kwenye Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT) Tabata Kuu Magengeni jijini Dar es Salaam.
Akiongozwa na kitabu kutoka maandiko matakatifu ya Ufunuo wa Yohana 21:1-8, Mchungaji Kimambo amesema alipitia wakati mgumu kuandaa mahubiri hayo na kusema anachojua hata katika hili Mungu ataendelea kuwa mfarij.
Mchungaji Kimambo amesema katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana kimefafanua kuwa anayeteseka sasa hatateseka milele, na anayetesa sasa hatatesa milele.
Amesema kitabu hicho kinafariji wanaoteseka na kuteswa na wengine, na kinaonya wanaotesa wengine.
“Kifo kinapokuja kinaonekana kama ni mwisho, lakini neno la Mungu linaeleza ni mwanzo mpya kwa wale waliomshika Yesu Kristo, hata kama tunateseka,” amesema.
Akizungumzia maisha ya Temba ndani ya kanisa, Mchungaji Kimambo amesema alikuwa kijana aliyekuwa akiandaliwa kuwa mzee wa kanisa.
Mama mzazi wa James Temba akilia kwenye jeneza lenye mwili wa mwanaye katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Tabata Kuu Magengeni wakati wa misa ya kumuaga.
Amesema Mungu ana njia nyingi za kupumzisha watu wake, akisema mateso aliyokutana nayo Temba wakati wa kukata roho sasa hayapo kwake, hata jeneza likifunguliwa na kukatwa tena, hawezi kusikia kwani yalipita na hana maumivu tena.
“James hajapotea, hata kama hicho kichwa hakitapatikana, ninachojua maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, na amesema atafanya maskani pamoja nasi.
“Mungu ana njia nyingi za kuwafuta watu machozi, hivyo muacheni Mungu atawafuta machozi yeye mwenyewe. Ni ngumu sana kushinda katika maumivu haya, lakini Yesu mwenyewe atatusaidia,” amesema.
Mchungaji Kimambo amesema Mungu katika maandiko yake ametoa onyo kali kwa wasioamini, wauaji na waabudu sanamu, kwani makao yao ni ziwa liwakalo moto, akihimiza watu kuepuka kumwaga damu kwani si jambo zuri katika Taifa lolote.
Amesema dhambi ya kuua imekemewa na Mungu na watu wanapaswa kupendana, kwani chuki ni sawa na mauaji.
“Si kazi ya Mkristo kulipa kisasi; kisasi ni kazi ya Mungu mwenyewe. Kuondoa uhai wa mtu ni jukumu la Mungu. Kama mtu ameingilia kazi ya Mungu, ni kumuombea Tanzania tusirudie tena mauaji kama haya,” amesema mchungaji huyo.
Dakika 10 za maisha ya Temba
Dakika tisa, (saa 7:23 hadi 7:32), zilitosha kueleza maisha ya Temba tangu alipozaliwa 2002 hadi umauti ulipomfika, huku ukimya ulitawala kwa waombolezaji kanisani hapo.
Jackson Temba, amemuelezea ndugu yake kuwa mwenye upendo na ucheshi, akisema alizaliwa akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu wa mzee Temba.
Mwili wa mwanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba aliyeuawa kwa kukatwa kichwa ukiwasili nyumbani kwao Tabata Mbuyuni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuagwa.
Jackson amemtaja ndugu yake huyo kama zawadi ya familia, akibatizwa mwaka 2003 mkoani Kilimanjaro na mwaka 2015 alipata kipaimara mkoani humo.
Amesema Temba alianza elimu ya msingi katika Shule ya Harvard East Africa School jijini Dar es Salaam, na mwaka 2019 alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Wavulana Kibaha, na baadaye kuchaguliwa kujiunga na mafunzo ya Kujenga Taifa (JKT) mkoani Tanga.
Baada ya mafunzo hayo, aliendelea na masomo ya kidato cha tano na sita mkoani Mbeya mwaka 2022 na baadaye kujiunga na IFM.
Katika matukio ya kanisa, Jackson amesema Temba alifanya mitihani ya Biblia na kuwahi kukabidhiwa jukumu la kuwa mzee wa kanisa, akijiuliza kwa nini kifo cha kikatili kimemkuta ndugu yao.
Salamu mbalimbali kwa Temba
Makundi mbalimbali yalijitokeza kutoa salamu za rambirambi, kumueleza Temba namna alivyoishi na watu duniani kwenye huduma mbalimbali.
Mwakilishi wa IFM amesema Temba alikuwa mwanafunzi wao ambaye angesoma kwa miaka mitatu, lakini lengo hilo halikufanikiwa.
“Temba alikuwa mwana jumuiya yetu, tuna uchungu tumepoteza mwanafamilia wetu,” amesema mwakilishi huyo wa IFM.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Serikali ya wanafunzi IFM ametoa pole, akitaka familia iendelee kuombewa ili Mungu ampokee Temba.
Nao Umoja wa Wanawake Machimbo wamesema mauaji ya Temba wameyapokea kwa uchungu usioelezeka.
Salamu za pole pia zilitolewa na kwaya kuu Machimbo wakisema wameumizwa na msiba huo na wanamshukuru Mungu kwa yote.
Kwa upande wa vijana, mwakilishi wa VWAO eneo la Machimbo amesema Temba alikuwa anategemewa ndani ya kanisa na alikuwa anaandaliwa kuvaa viatu vya kuongoza vijana wenzake kutokana na uwezo wake.
Diwani wa Liwiti, amesema msiba huo umestua hadi Serikali, akihimiza jamii kuishi kwa upendo.
Pia, Jumuiya ya Samaria imesema imeumizwa na msiba wa Temba kwani mara zote ndiye aliyekuwa akihubiri ndani ya jumuiya na mara ya mwisho alihusika kufanya usafi kanisani.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, amewataka wakazi wa Dar es Salaam kupunguza maneno juu ya tukio hilo kuhusu sababu ya kutokea kwake.
“Tupunguze maneno eti kifo kimetokana na nini. Maneno haya yanaendelea kusababisha maumivu kwa familia,” amesema.