Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kupata mtoto wa kwanza kupitia huduma ya upandikizaji mimba (In Vitro Fertilization – IVF), mafanikio yanayoashiria hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa nchini na kutoa matumaini kwa wanandoa wenye changamoto ya uzazi.
Kwa mara ya kwanza, Muhimbili ilianza upandikizaji wa vijusi kwenye tumbo la mama Mei mwaka 2025. Imesema hadi sasa jumla ya kinamama 22 wapo katika hatua mbalimbali za upandikizaji.
Akizungumza leo Jumatano, Mei 6, 2026, wakati akipokea ugeni kutoka Ofisi ya Rais, Tamisemi, Idara Maalum Zanzibar, Mkurugenzi wa MNH, Dk Delila Kimambo amesema mtoto huyo alizaliwa baada ya huduma hiyo kuanza kutolewa rasmi mwaka 2025 katika hospitali hiyo.
Ameeleza kuwa mama na mtoto wanaendelea vizuri kiafya.
“Tunayo furaha kubwa kufanikisha hili. Kuna familia nyingi zilikuwa na uhitaji wa kupata watoto lakini zilishindwa kwa njia ya kawaida. Sasa huduma hii inapatikana hapa hapa nchini,” amesema Dk Kimambo.
Mkuu wa msafara kutoka Ofisi ya Rais, OR Tamisemi Idara Maalum Zanzibar, Mikidadi Mbago Mzee kushoto akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Delila Kimambo
Amebainisha kuwa hadi sasa wanawake 22 wamefanyiwa upandikizaji mimba katika hospitali hiyo, huku mtoto huyo akiwa wa kwanza kuzaliwa kupitia teknolojia hiyo. Amewataka wananchi kujitokeza kupata huduma hiyo badala ya kusafiri nje ya nchi.
Jumla ya wenza 2,000 walijitokeza kuhitaji usaidizi wa kupata watoto katika kitengo cha upandikizaji mimba hospitalini hapo, na kwa mujibu wa wataalamu, 120 walibainika kuwa na vigezo vya kupandikizwa hadi kufikia Machi 2025.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, IVF ni mchakato wa kitabibu unaohusisha uchukuaji wa mayai ya mwanamke na mbegu za mwanaume, ambazo hukutanishwa maabara ili kutengeneza kiinitete.
Baadaye, kiinitete hupandikizwa kwenye mfuko wa uzazi wa mwanamke ili kukuza ujauzito. Njia hii hutumika kwa wanandoa wenye matatizo ya uzazi yanayoshindikana kutatuliwa kwa njia za kawaida.
Historia ya huduma ya IVF Muhimbili
Huduma ya upandikizaji mimba Muhimbili ilianza rasmi mwaka 2024 kwa vipimo mbalimbali kabla ya kuanza upandikizaji Mei mwaka jana, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma za ubingwa bobezi nchini.
Mbali na IVF, Dk Kimambo amesema Muhimbili inaendelea kuimarisha huduma nyingine za kibingwa, ikiwemo upandikizaji figo. Amesema hadi sasa wagonjwa 124 wamepatiwa huduma hiyo kwa mafanikio, huku wagonjwa watano wakitarajiwa kufanyiwa upasuaji huo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya matundu madogo.
“Teknolojia imeboreshwa, sasa tunavuna figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia tundu dogo, jambo linalopunguza maumivu na muda wa kupona,” amesema.
Ameeleza kuwa hospitali hiyo, yenye zaidi ya miaka 120 tangu kuanzishwa mwaka 1905, imeendelea kubadilika kwa kiwango kikubwa na sasa ina vitanda 1,436 na kliniki zaidi ya 141.
Kwa upande wa huduma za kila siku, amesema hospitali inapokea wastani wa wagonjwa 4,420 kwa siku, huku zaidi ya wagonjwa 2,000 wakiwa wa nje. Pia huduma za radiolojia zinahudumia takribani wagonjwa 300 kwa siku, na wagonjwa 120 hupatiwa huduma ya kusafisha damu (dialysis).
Katika kitengo cha dharura, amesema hospitali inapokea takribani wagonjwa 120 kwa siku, ambapo asilimia 20 ni watoto, na kusisitiza kuwa Muhimbili ni miongoni mwa hospitali chache zenye uwezo wa kutoa huduma maalumu za dharura kwa watoto.
Dk Kimambo ameongeza kuwa uwepo wa maabara yenye vifaa vya kisasa umewezesha kufanyika kwa vipimo vyote muhimu ndani ya hospitali hiyo, hatua inayochangia kupunguza rufaa zisizo za lazima.
Amesema juhudi hizo zimepelekea kupungua kwa rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi, ambapo mwaka jana wagonjwa 108 pekee walipatiwa rufaa ikilinganishwa na maelfu ya miaka ya nyuma.
Aidha, amesema hospitali hiyo inapokea wagonjwa wa rufaa kutoka Zanzibar, ambapo wastani wa wagonjwa 249 hupokelewa kwa ajili ya matibabu ya kibingwa, hususan magonjwa ya masikio, pua na koo (ENT) pamoja na magonjwa mengine.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara kutoka Ofisi ya Rais, Tamisemi, Idara Maalum Zanzibar, Mikidadi Mbago Mzee amesema wamevutiwa na maendeleo ya Muhimbili na wamefika kujifunza namna huduma za hospitali za rufaa zinavyotolewa ili kuanzisha hospitali maalumu kwa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Tumekuja kujifunza kuhusu huduma za VIP, maabara na uendeshaji wa hospitali za rufaa. Muhimbili imepiga hatua kubwa sana na ni mfano wa kuigwa,” amesema.
Amesisitiza kuwa Zanzibar inalenga kujenga hospitali ya rufaa yenye viwango vya juu kwa kuiga uzoefu wa Muhimbili, ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.