Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Riziki Shemdoe, amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kote nchini kuanza mara moja maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na uwepo wa wanafunzi wa darasa la tano na sita watakaohitimu kwa wakati mmoja, hali itakayosababisha ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoingia sekondari.

Akizungumza leo Jumatano, Mei 6, 2026 jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa elimu wa Mkoa wa Dodoma, Shemdoe amesema maandalizi ya mapema yatasaidia kuepusha changamoto za msongamano na uhaba wa nafasi kwa wanafunzi.

“Sote tunafahamu kuwa mwaka 2028 tutakuwa na wanafunzi wengi wanaoingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja. Hii inahitaji maandalizi ya dhati kuanzia sasa ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa nafasi ya kuendelea na masomo,” amesema Shemdoe.

Amezitaka mamlaka husika kuwekeza katika ujenzi wa shule mpya, kuongeza vyumba vya madarasa pamoja na miundombinu ya vyoo ili kukidhi mahitaji yatakayojitokeza.

Shemdoe ameonya kuwa upungufu wa miundombinu unaweza kusababisha utoro na kuathiri juhudi za Serikali katika kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu.

Mbali na hilo, Shemdoe amekemea tabia ya baadhi ya shule kuwazuia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kufanya mitihani ya kitaifa kwa kisingizio cha kushusha kiwango cha ufaulu.

Amesema hatua hiyo ni kinyume na misingi ya elimu jumuishi na haki za mtoto, akiwataka walimu kuwasaidia wanafunzi hao ili waweze kufanya vizuri.

“Walimu waache mara moja tabia hiyo. Wajibu wao ni kuwasaidia wanafunzi wote bila ubaguzi,” alisisitiza.

Amebainisha kuwa mitihani yote ya kitaifa, ikiwemo ya darasa la nne, la saba, kidato cha pili, cha nne na cha sita, inapaswa kufanywa na wanafunzi wote bila ubaguzi.

Shemdoe ametoa tahadhari kuhusu matumizi ya adhabu kali kwa wanafunzi, akisisitiza kuwa adhabu zinapaswa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Elimu na Tamisemi.

“Sipingi adhabu, lakini lazima zilingane na kosa, umri wa mtoto na miongozo iliyopo,” alisema.

Pia, amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kupata chakula cha mchana shuleni, akibainisha kuwa njaa ni kikwazo kikubwa kwa ujifunzaji.

Amezihimiza shule zenye mashamba kuzalisha chakula kwa ajili ya wanafunzi ili kuongeza umakini darasani na kuboresha matokeo ya kitaaluma.

Katika hatua nyingine, Shemdoe ameupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kupanda kutoka nafasi ya 10 mwaka 2024 hadi nafasi ya pili kitaifa mwaka 2025 katika matokeo ya mitihani ya taifa.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Kiduma Mageni amesema mkoa huo una shule za msingi 968 na sekondari 303, lakini bado unakabiliwa na upungufu wa walimu na miundombinu.

Mageni amesema shule za msingi zina wanafunzi 590,958 huku walimu wakiwa 8,423, hivyo kuna upungufu wa walimu 4,399. Sekondari zina wanafunzi 140,322 na walimu 5,175, ikiwa na upungufu wa walimu 1,267.

Ameongeza kuwa kuna upungufu wa madarasa kwa asilimia 42 katika shule za msingi na asilimia 12 sekondari, huku madawati yakipungua kwa asilimia 38 msingi na asilimia 1.85 sekondari.

Pia, amesema kuna upungufu wa vyoo kwa asilimia 27, maabara asilimia 60 na viti pamoja na meza asilimia 18.

Hata hivyo, amesema juhudi zinaendelea kufanywa na halmashauri mbalimbali kuboresha miundombinu na kuongeza walimu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mkoa huo umeanzisha mfumo wa utoaji tuzo kwa shule, wilaya na halmashauri zinazofanya vizuri kielimu.

Amesema hatua hiyo imeongeza ushindani chanya na uwajibikaji, hali iliyochangia mkoa huo kushika nafasi ya pili kitaifa mwaka 2025.

“Utoaji wa tuzo umeleta ari mpya ya ushindani na uwajibikaji katika sekta ya elimu,” alisema Senyamule.

Ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi iliibuka kinara kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *