Arusha. Serikali imesema haitarajii kupokea malalamiko ya watumishi wa umma waliokosa kupandishwa vyeo licha ya kukidhi vigezo, ikieleza kuwa hali hiyo inasababishwa na uzembe wa baadhi ya wasimamizi katika taasisi za umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Maofisa Utawala na Rasilimaliwatu wanapaswa kuwajibika kikamilifu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi wote wanaostahili.

Akizungumza leo Mei 6, 2026 jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM Tanzania), Kikwete amesema Serikali haitavumilia uzembe unaosababisha watumishi wenye sifa kukosa haki zao.

“Aidha, kwa wale ambao wamejiendeleza watabadilishiwa kada kulingana na miongozo iliyowekwa. Ofisi ninayoiongoza haitarajii kupokea malalamiko ya watumishi walioachwa ilhali wanazo sifa kutokana na kutowajibika kwa baadhi yenu,” amesema.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26, Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kupandisha vyeo watumishi 219,042, na kwamba zoezi hilo linatarajiwa kufanyika Mei mwaka huu kwa watumishi wote waliokidhi vigezo na waliotengewa bajeti.

Kuhusu Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2025, Kikwete amesema unalenga kutoa fursa kwa vijana kupata uzoefu wa kazi kwa njia ya uwazi na haki, kulingana na nafasi zilizopo katika taasisi za umma.

Amesisitiza kuwa wataalamu wa rasilimaliwatu wanapaswa kuzingatia mwongozo huo na kujitathmini ili kuwa chachu ya mageuzi ya kiutendaji, kuboresha huduma na kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima.

Aidha, amewataka wataalamu hao kusimamia sera, sheria na taratibu kwa haki na kwa wakati, pamoja na kuepuka matumizi ya lugha zisizofaa kwa watumishi na wananchi, ili kuimarisha imani kwa Serikali.

“Ni muhimu pia kujenga mazingira rafiki ya kazi yenye usalama wa kisaikolojia kwa watumishi ili waweze kutoa mawazo yao bila hofu, hatua itakayosaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuimarisha afya ya akili,” amesema.

Kikwete amesema mageuzi ya utumishi wa umma yanategemea kwa kiasi kikubwa mchango wa wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu, akiwataja kama wadau muhimu katika kufanikisha malengo ya taasisi na ustawi wa wananchi.

Amesema kada hiyo ina wajibu wa kuhakikisha taasisi zinakuwa na watumishi wenye uwezo, maadili na uzalendo, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia na ubunifu katika utoaji wa huduma.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Rais wa Jumuiya ya Mameneja Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Afrika (APS-HRMnet), Xavier Daudi, amesema mkutano huo umehusisha washiriki 1,350 na kujadili mada mbalimbali kuhusu usimamizi wa rasilimaliwatu katika mazingira ya mabadiliko ya haraka.

Amesema miongoni mwa maazimio ya mkutano uliopita ni kuanzishwa kwa Bodi ya Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala, pamoja na kuhuisha muundo wa maendeleo ya kada hiyo na mitaala ya mafunzo.

Daudi amesema maandalizi ya mapendekezo hayo yanaendelea, huku wadau wakitarajiwa kushirikishwa kabla ya kuwasilishwa kwa mamlaka husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *