
Geita. Bebki ya Exim Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuboresha ustawi wa jamii kwa kuimarisha huduma za afya katika Hospitali ya Manispaa ya Geita kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) unaojulikana kama Exim Cares.
Hatua hiyo inalenga kuziba mapungufu yaliyokuwapo katika huduma za afya ya uzazi na dharura, hususan kwa wajawazito na watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda au wenye changamoto za kiafya.
Akizungumza Mei 6, 2026 katika hafla ya makabidhiano ya msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameipongeza benki hiyo kwa mchango wake, akisema umefika wakati muafaka wa kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Amesema licha ya tawi la benki hiyo mkoani humo kuwa jipya na bado halijaanza kuingiza faida, taasisi hiyo imeonesha uwajibikaji mkubwa kwa jamii kwa kuweka kipaumbele katika sekta ya afya.
“Mchango huu unaenda kusaidia moja kwa moja watoto wachanga, hasa njiti na wale wenye changamoto za kiafya, hivyo kuboresha huduma zinazotolewa hospitalini hapa,” amesema Komba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Stanley Kafu, amesema msaada huo umetokana na tathmini ya mahitaji halisi ya jamii, akibainisha kuwa benki hiyo inalenga kugusa maeneo yenye athari ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi.
“Kupitia Exim Cares, tunalenga kutoa suluhisho la changamoto halisi za jamii. Hapa Geita tumebaini upungufu katika huduma za afya ya uzazi na watoto, hivyo tumeona ni muhimu kuingilia kati ili kuboresha hali hiyo,” amesema Kafu.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Geita, Dk Thomas Mauru, amesema msaada huo utaongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma bora na kwa wakati, hasa kwa watoto wanaohitaji uangalizi maalum.
“Msaada huu unakuja wakati muafaka na utaongeza ufanisi wa huduma zetu, hivyo kuboresha afya ya jamii kwa ujumla,” amesema Dk Mauru.
Mbali na sekta ya afya, mpango wa Exim Cares unahusisha pia uwekezaji katika elimu, mazingira, ubunifu na uwezeshaji wa kiuchumi, ukilenga kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
Baada ya shughuli hiyo, benki hiyo inatarajiwa kuzindua rasmi tawi lake jipya mkoani Geita, tukio litakaloongozwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha huduma za kifedha na kuchochea ukuaji wa biashara katika eneo hilo.