
Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Biashara, Dar es Salaam, imekataa ombi lililowasilishwa na benki za kimataifa za Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited na Standard Chartered Bank Malaysia Berhad, lililokuwa likiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya rufaa dhidi ya uamuzi wa awali wa mahakama hiyo kuhusu usajili wa hukumu ya kigeni.
Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Pan African Power Solutions (PAP) na VIP Engineering and Marketing Limited.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Musa Pomo Mei 5, 2026, katika shauri la maombi ya kibiashara namba 1361/2026, ambalo lilitokana na mgogoro wa awali wa kesi namba 67 na 75 za mwaka 2017.
Katika shauri hilo, benki hizo ziliiomba Mahakama Kuu iruhusu kuongezwa muda wa kuwasilisha notisi ya rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ulioahirisha kusajili hukumu yake ya Mahakama ya Nje, baada ya muda uliowekwa kisheria kupita.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ilitupilia mbali ombi la benki hizo ikisema kuwa hazikutoa sababu za msingi za kuongezewa muda.
Historia ya mgogoro
Kulingana na kumbukumbu za mahakama, mgogoro huu unatokana na hukumu ya kigeni iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza Novemba 2016 dhidi ya mjibu maombi wa kwanza kuhusu makubaliano ya mkopo kati ya pande husika.
Baada ya hukumu hiyo, benki hizo ziliwasilisha maombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Biashara, zikitaka hukumu hiyo isajiliwe nchini ili iweze kutekelezwa.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake wa upande mmoja uliotolewa na Jaji Barke Sehel Februari 9, 2017, ilisajili hukumu hiyo na kuwa hukumu ya mahakama hiyo.
Hata hivyo, IPTL, PAP na VIP walifungua shauri la maombi wakiiomba mahakama hiyo kuufuta usajili wa hukumu hiyo.
Pamoja na sababu nyingine, walidai utekelezaji wa hukumu hiyo ungekiuka sera ya umma ya Tanzania kwa kudhoofisha mashauri yanayoendelea ndani ya nchi, likiwemo shauri la madai namba 229 la 2013 linalopinga uhalali wa uhamisho na ubadilishaji wa mkataba wa mkopo.
Pia, walidai kuwa usajili wa hukumu hiyo haukufuata taratibu sahihi na ulipuuzia mashauri sambamba yanayoendelea Tanzania.
Wajibu maombi ambao ni benki hizo kupitia wakili wao, Gaspar Nyika, walipinga hoja za waombaji wakidai utekelezaji wake haukukiuka sera ya umma na kwamba masharti yote ya kisheria ya usajili yalitimizwa.
Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Butamo Phillip Agosti 26, 2017, iliufuta usajili huo ikisema shauri namba 229/2017 ambalo bado lilikuwa linaendelea mahakamani nchini lilitangulia shauri la Uingereza.
Pia, mahakama ilisema usajili wa hukumu hiyo haukuzingatia shauri hilo lililokuwa linaendelea nchini, jambo lililofanya utekelezaji kuwa usiofaa kwa kuwa ungeweza kuleta hatari ya mgongano wa maamuzi ya kimahakama.
Safari ya rufaa
Baada ya uamuzi huo, benki hizo ziliwasilisha notisi ya rufaa na baadaye kufungua rufaa ya madai namba 386/2022 katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Hata hivyo, rufaa hiyo ilikumbwa na changamoto za kiutaratibu wakati wa usikilizwaji wa rufaa. Wajibu rufaa waliwasilisha pingamizi la awali wakipinga uhalali wa rufaa hiyo wakidai kuwa kulikuwa na kasoro katika utaratibu wa kuwasilisha nyaraka muhimu.
Januari 9, 2026, Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na pingamizi hilo na kuifuta rufaa hiyo kwa kukosa uhalali wa kisheria.
Kufuatia hatua hiyo, benki hizo ziliamua kurejea Mahakama Kuu kuomba muda wa ziada ili ziweze kuwasilisha notisi mpya ya rufaa.
Hata hivyo, muda wa kisheria ulikuwa tayari umepita, hivyo waliwasilisha maombi ya kuongezewa muda chini ya kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa.
Hoja za waombaji
Kupitia mawakili wao, waombaji walidai kuchelewa kwao hakukutokana na uzembe, bali kulisababishwa na mchakato wa kisheria uliokuwa unaendelea katika rufaa ya awali.
Walidai kuwa walikuwa wamefanya juhudi zote kwa wakati na kwamba rufaa yao ilifutwa kwa misingi ya kiutaratibu tu, si kwa msingi wa hoja za kimaudhui.
Pia, walidai baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa walichukua muda mfupi kupata ushauri wa kisheria na kuandaa maombi mapya, jambo ambalo walidai ni la kawaida katika mchakato wa kisheria.
Wakirejea baadhi ya kesi za awali za Mahakama ya Rufaa, mawakili wa benki hizo walisisitiza kuwa Mahakama ina mamlaka ya kuongeza muda kwa kuwa kuna sababu za msingi, hasa pale ambapo hakuna ucheleweshaji wa makusudi.
Wajibu maombi
Kwa upande wao, wajibu maombi walipinga ombi hilo wakidai kuwa benki hizo zilichelewa bila sababu za msingi na kwamba uzembe wao katika kufuata taratibu za kisheria hauwezi kusamehewa.
Walidai kuwa kushindwa kuwasilisha nyaraka muhimu kwa wakati kulisababisha kufutwa kwa rufaa ya awali, hivyo hali hiyo haipaswi kugeuzwa kuwa sababu ya kuomba msamaha wa muda.
Aidha, walieleza kuwa waombaji hawakutoa maelezo ya kina kuhusu kipindi chote cha kuchelewa na pia walishindwa kuambatanisha nyaraka muhimu, ikiwa ni pamoja na uamuzi wanaotaka kukata rufaa dhidi yake.
Uamuzi wa Mahakama
Katika uamuzi wake, Jaji Pomo amebainisha kuwa sheria inahitaji mwombaji wa aina hiyo ya maombi kutoa sababu za msingi na za kuridhisha zinazoonyesha kwa nini alichelewa na kwa nini Mahakama inapaswa kutumia busara yake kumpa muda wa ziada.
Mahakama ilisisitiza kuwa kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa ndicho kinachoongoza maombi ya aina hiyo na kwamba masharti yake lazima yazingatiwe kikamilifu.
Jaji Pomo amesema ingawa Mahakama ina mamlaka ya kuongeza muda, mamlaka hayo hayapaswi kutumika kiholela bali kwa kuzingatia uhalali wa sababu zilizotolewa.
Katika uchambuzi wake, Mahakama pia ilibaini kuwa waombaji walishindwa kueleza kwa kina kila hatua ya kuchelewa kwao na hawakutoa ushahidi wa kutosha unaoonyesha walikuwa makini katika kufuatilia haki zao ndani ya muda uliowekwa.
Mahakama pia ilikataa hoja kwamba kuchelewa kulikuwa kiufundi tu ikisema hata ucheleweshaji wa kiufundi lazima uelezwe kwa uwazi na kuungwa mkono na ushahidi wa kutosha.
Baada ya kuzingatia hoja zote za pande zote mbili, Mahakama Kuu iliamua kutupilia mbali ombi la benki hizo ikisema hazikutoa sababu za msingi za kuongezewa muda.
Mahakama pia haikutoa amri ya gharama kwa upande wowote, lakini ilisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria kwa umakini, hasa katika masuala ya rufaa za kimataifa na usajili wa hukumu za kigeni.