
Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimesema badala ya wadau kupinga ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, waunganishe nguvu kushinikiza utekelezwaji wa mapendekezo yake.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, ametaka itungwe sheria maalumu ya utekelezwaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo, aliyosema imegusa sehemu kubwa ya mambo yanayolalamikiwa na wananchi.
Chaumma, ilishaweka wazi mapema msimamo wake wa kuiunga mkono tume hiyo iliyoongoza na Jaji Othman Chande, kwa kile ilichosema ilitazama wasifu wa wajumbe na kujiridhisha kuwa wana sifa. Pia, imeunga mkono ripoti iliyotolewa.
Tume hiyo iliyoundwa Novemba 20, 2025, ilifanya kazi yake kwa siku 153 na kukabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23, mwaka huu.
Kuundwa kwa tume hiyo, kulitokana na matukio ya vurugu wakati na baada ya uchaguzi yaliyosababisha mauaji ya watu na uharibifu wa mali za watu binafsi na miundombinu ya umma.
Mwalimu ameyasema hayo leo, Alhamisi Mei 7, 2026 alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyoketi Mei 5, mwaka huu.
“Jaji Chande (ripoti) alisema kuna kilio cha Katiba Mpya, suala la uchaguzi, utekaji na kupotea kwa watu, uchumi na ajira kwa vijana, uwajibikaji hafifu wa viongozi wa umma, ndivyo vilio vya Watanzania,” amesema.
Amesema sababu hizo ndizo zilizowafanya watu wafanye ghasia za Oktoba 29, akisema chama hicho kinaelekeza nguvu zake kuishinikiza Serikali iyafanyie kazi masuala yaliyopendekezwa na tume.
“Kuliko tukianza kupingana na hapo ndipo wakati mwingine tunapaswa kujiuliza huwa tunakosea wapi hasa sisi wapinzani? Tumeidai Katiba Mpya kwa miaka 30, tume mbalimbali ya Jaji Nyalali, Kissanga na Warioba tume zimekuwa zikiundwa sasa hivi tunakosea wapi,” amesema.
Amesema wanadhani moja kati ya sababu ni kutangulizwa kwa dhana kwamba wapinzani kazi yao ni kupinga kila kilichoundwa na Rais.
“Badala yake baada ya muda mfupi tunatumia tume hizo tunazozipinga kama rejea ya mahitaji na madai yetu. Hata hii ya Jaji Chande ni suala la muda tu, hatutamaliza muda mrefu wataitumia kama rejea,” amesema.
Ameisisitiza Serikali kuanza haraka utekelezaji wa mapendekezo ya tume hiyo huku ikiishauri mambo ya kufanya katika utekelezaji huo.
Miongoni mwa mambo aliyotaka yatekelezwe haraka ni Katiba Mpya kwa kuwa ni kipaumbele na kwamba mchakato wake, uwe umekamilika kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2029.
Ametaka mchakato wa uundwaji wa katiba hiyo, unapaswa kuanza sasa kwa kuundwa kwa kundi rejea litakalokubaliana masuala ya kuingia kwenye Katiba mpya kwa kuzingatia mambo yaliyokwamisha mchakato wa mwaka 2014 na kabla.
Ametaka kundi hilo liwe kama mkutano mkuu maalumu wa kitaifa wa Katiba Mpya na lihusishe wadau wote, ili kuwa na mwafaka wa pamoja wa kushughulikia mambo yote yaliyokwamisha mchakato wa awali.
“Kwa mambo ambayo mkutano huo hautakuwa umekubaliana, yapelekwe kwenye kura ya maoni ili Watanzania wakaamue kwa kura,” amesema.
Amesema tayari kuna nyaraka za kuzitumia ikiwemo katiba iliyopendekezwa mwaka 2014 na nyingine zinazoweza kutumika kama rejea.
“Chaumma hatuamini kuendelea tulipoishia kwenye Katiba iliyopendekezwa. Pengine katika kipindi hiki cha miaka 10 tangu pendekezo lililopitishwa, yapo mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii tumejifunza, ambayo yangeweza kuwa sehemu ya Katiba,” amesema.
Mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi na Polisi
Kuhusu mfumo wa haki na demokrasia, Mwalimu amesema Chaumma inapendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya sheria katika kipindi cha mpito kabla ya kupatikana kwa katiba mpya.
Amesema chama hicho kinataka itungwe sheria mpya ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuifanya iwe huru na yenye kuaminika mbele ya wananchi kabla ya kusimamia kura ya maoni ya Katiba.
Aidha, ameitaka Serikali kufanya mabadiliko makubwa katika Sheria ya Jeshi la Polisi hususan vifungu vya 40 hadi 46 ili kupunguza makandokando yanayolalamikiwa na jamii.
Pia, Mwalimu amependekeza mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ili kuimarisha uwazi na demokrasia ya ndani ya vyama, jambo ambalo ripoti ya Jaji Chande ilitaja kama moja ya vichocheo vya hasira za wananchi baada ya kutoridhishwa na uteuzi wa wagombea.
Ajira kwa Vijana
Chaumma, imeshauri Serikali kuwekeza zaidi katika sekta zinazotoa fursa nyingi za ajira kwa vijana na itoe vivutio kwa kampuni zinazozalisha ajira nyingi na kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyowazuia wabunifu.
Kuhusu ugumu wa maisha, Chaumma imetahadharisha uwezekano wa kupanda kwa bei za vyakula kutokana na vita vya Mashariki ya Kati vinavyoathiri upatikanaji wa mbolea.
“Serikali ione umuhimu wa kuwa na bajeti ya dharura kwa ajili ya wakulima na kupunguza tozo kwenye mafuta ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa usafirishaji,” amesisitiza.
Akigusia suala la utekaji na kupotea kwa watu, Mwalimu amesema Chaumma inaitaka tume na mamlaka za uchunguzi kuweka wazi ushahidi dhidi ya wote waliohusika kupanga au kufadhili matukio hayo ili kuepuka dhana ya kuoneana.
Aidha, ametaka kutungwa kwa sheria maalumu ya kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yote ya tume, huku wakitaka viongozi wanaotajwa kwenye ripoti za CAG kuhusika na rushwa wawajibishwe mara moja.
Amesema kamati kuu pia, imeona kuna mambo ripoti ya tume hiyo ilipaswa kwenda mbali zaidi ikiwemo ilipotaja sababu za kutekwa na kupotea kwa watu.
Kwa mtazamo wa chama hicho, kulipaswa kuongezwa sababu za kisiasa kama vyanzo vya matukio ya utekaji na kupotea kwa watu.
“Sisi tunatoa rai kwa tume, kama wana sababu nyingine waseme, lakini pale walikoishia mjadala umekuwa mkubwa, kwamba utekaji ni mapenzi tu, biashara tu na uasi tu, tunadhani zipo na sababu nyingine,” amesema.