Dar es Salaam. Serikali ya Mtaa wa Vikawe Shule imewaombea hifadhi waathirika wa vurugu za Lupaso, Kibaha mkoani Pwani kwenye nyumba ambazo hazijakamilika kujengwa jirani na eneo hilo, baada ya makazi yao kubomolewa katika vurugu zilizotokea alfajiri ya Mei 6, 2026.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limesema linamshikilia mmiliki wa eneo husika (hakutajwa jina), kwa mahojiano.

Vurugu hizo zilizosababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali zilichochewa na mgogoro wa ardhi katika eneo hilo na kusababisha kuibuka mapigano baina ya wakazi na kikundi cha watu waliotambulika kama mabaunsa wa anayetajwa ni mwenye eneo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Shaban Ally Shaban, familia 10 zimekosa makazi baada ya nyumba 20 kubomolewa na mabaunsa, kati yake nyumba 10 zikiwa na watu waliokuwa wanaishi ndani yake, huku nyingine 10 wahusika wakiwa hawajahamia.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

“Hadi vurugu zinadhibitiwa, nyumba 20 zilikuwa zimebomolewa, wananchi wangu wamejeruhiwa, watano walikuwa na hali mbaya na vifo nilivyovishuhudia ni vya mabaunsa watatu. Miili ilipelekwa kuhifadhiwa na majeruhi kutibiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Tumbi,” amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura katika hospitali hiyo, Sialely Moshi jana Mei 6, 2026 aliiambia Mwananchi kwamba wamepokea maiti tatu na majeruhi 15 wa tukio hilo, wote wakiwa wanaume.

Mwananchi imeshuhudia askari wa kutuliza ghasia wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi wakiendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo, huku waathirika wakiendelea kukusanya mabaki ya mali zao na kuhamishia sehemu nyingine.

Maisha mapya

Waathirika hao ni kama hawana matumaini tena, wengi wanaonekana kukata tamaa. Kina mama na watoto faraja pekee wanayoiona ni kulia, hawaelewi kesho yao itakuwaje.

Wakizungumza na Mwananchi leo Mei 7, 2026 wameeleza namna usiku wa kwanza walipolala kwenye mapagale ambako wamepewa hifadhi, ulivyokuwa mgumu kwao.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

“Hatujui hata imefikaje asubuhi leo, tumekuwa na siku ngumu tangu jana, mume wangu amejeruhiwa yupo hospitali, hatuna pa kuishi, watoto hawajala, sikuwahi kuwaza pamoja na umasiki tuliokuwa nao kwamba ipo siku tutafikia kwenye hali hii,” amesema Neema Elisha huku akibubujikwa machozi.

Mkazi mwingine, Upendo Mlale amesema kula yao imekuwa ya taabu, hawana pesa wala kitu chochote.

“Jana kuna mama anakaanga maandazi ndiye alituletea, tukala na kunywa na maji usiku, leo hatujui nani atatupa msaada.

“Watoto wameshindwa kwenda shule, wapo wengine ni wa madarasa ya mitihani, kwa hali hii tunafanyaje,” amesema.

Kwa upande wake Innocent Macha, amesema wamepata hifadhi kwenye mapagale ya watu, akieleza namna wanavyopitia kipindi kigumu, hawana pesa, hawana makazi na hata kula yao na watoto ni shida.

“Tunaomba Serikali itusaidie, tunapitia kipindi kigumu, hatujui kesho yetu itakuwaje. Wasamaria wema wa huku Vikawe ndiyo wanatusaidia chakula, ni maisha ambayo hatukuwahi kutegemea tutayaishi,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vikawe, Shaban Ally Shaban ameiambia Mwananchi kwamba wamelazimika kuwaomba watu ambao nyumba zao hazijakamilika (mapagale) zilizo jirani na Lupaso wasaidie kwa muda kuwahifadhi waathirika.

Amesema kama uongozi wa mtaa ndio wanahangaikia kufanya jitihada kuwasaidia waathirika.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

“Hatuna taarifa kutoka Serikali Kuu kwa maana ya wilayani kwamba watawasaidia wananchi hawa, uongozi wa mtaa ndiyo tumefanya jitihada ya kuongea na wadau wetu kuwaomba kila mmoja alichojaliwa kuwasaidia waathirika.

“Vilevile katika hifadhi, tumeomba wale wenye nyumba lakini bado hawajahamia na wale waliojenga lakini hazijakamilika ujenzi watusaidie kuwahifadhi waathirika kwa muda, wamekubali hivyo wamepata hifadhi kwa muda,” amesema.

Kuhusu ulinzi kwenye eneo la Lupaso kulikotokea vurugu, amesema Jeshi la Polisi limeimarisha japo serikali ya mtaa na wananchi wa Lupaso wapo njiapanda, hawana chochote wanachokifahamu juu ya hatima ya mgogoro huo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge leo Mei 7, 2026 alipoulizwa iwapo kuwa jitihada ambazo mkoa unafanya kuwasaidia waathirika, amesema tayari alishatoa taarifa.

“Lile eneo haijajulikana mmiliki ni nani, nilishatoa press (taarifa kwa vyombo vya habari) nikasema vyombo vya ulinzi vinaendelea kufanyia uchunguzi tukio hilo, subiri utafahamishwa,” amesema.

Waziri wa Ardhi, Leonard Akwilapo alipotafutwa amesema hajausikia mgogoro huo na kutaka atafutwe katibu mkuu wake, ambaye hata hivyo hakupatikana kwenye simu.

Kuhusu mgogoro

Akizungumzia mgogoro huo, Mwenyekiti wa mtaa huo amesema hata yeye hajui mwanzo wa tatizo hilo, kwa kuwa yeye alifika Vikawe mwaka 2010 kabla hata hajachaguliwa kuwa mwenyekiti na kukuta wananchi wanaishi bila migogoro, hadi mwaka jana ulipoibuka, baada ya mtu aliyemtaja kwa jina (limehifadhiwa), kudai eneo hilo ni lake na waliouziwa walitapeliwa.

“Mkuu wa Wilaya ya Kibaha (Nickson John maarufu Niki wa Pili) alikuja kuusuluhisha ili kuleta maridhiano. Wananchi ambao wamejenga kwenye eneo hilo kwa muda mrefu hawakuwa na tatizo, walishakubali kuwa mwanzo walipouziwa walitapeliwa, hivyo kuridhia kulipa tena kwa mwenye eneo kwa mikataba,” amesema mwenyekiti wa mtaa.

Amesema Mkuu wa Wilaya aliwaondolea hofu kuwa jambo hilo halina shaka, kabla ya Mei 2, 2026 kusikia mwenye eneo amekataa maridhiano.

Mei 5 wananchi waliomba kuonana na Mkuu wa Wilaya na jana Mei 6, 2026 walikuwa wakutane naye, lakini alfajiri ya kuamkia siku ya kwenda kuonana na DC ndipo vurugu zikatokea.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha alipotafutwa, simu yake haikupokelewa, ingawa asubuhi baada ya vurugu hizo wananchi wa Lupaso wanasema alifika kuwapa pole.

Mwananchi ilipomtafuta siku hiyo aliomba apigiwe baada ya dakika 10 kwa kuwa alikuwa kikaoni, lakini alipopigiwa baadaye simu yake haikupokelewa.

Akizungumzia hatua za maridhiano zilizofikiwa kati ya wananchi na mwenye eneo mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa mtaa amesema anachokifahamu walikubaliana kwamba kwa kuwa wananchi waliuziwa kwa kutapeliwa, basi eneo hilo lipimwe na waliokwisha kujenga wamlipe mwenye eneo Sh3,000 kwa kila mita ya mraba.

Amesema pande zote ziliridhia mbele ya mkuu wa wilaya na kupeleka wapima wakapima, huku wananchi wakisubiri control number ili wafanye malipo.

“Kila kitu kilikwenda vizuri na huyo mmiliki alikubali kulipwa mbele ya mkuu wa wilaya, lakini Mei 2, 2026 baada ya eneo kupimwa na kujua ukubwa wake alikwenda tena kwa DC na kusema ametengua maridhiano,” amesema.

Amesema mkuu wa wilaya aliwaita na alichokiamua ni kumtaka mwenye eneo kwenda mahakamani, lakini kabla hajafanya hivyo ndipo kundi hilo la mabaunsa likavamia na kusababisha vurugu hizo.

Mwenyekiti huyo pia amemtaja mtu mmoja kwa jina kuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa kwenye kundi la mabaunsa katika vurugu hizo, ambaye awali alitambulishwa kwao kama mwakilishi wa familia ya mmiliki katika michakato ya maridhiano.

Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na  kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

“Nilimuona kwenye vurugu, namba zake nilikuwa nazo na nimempa RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani),” amesema mwenyekiti wa mtaa, ingawa Mwananchi pia ilijaribu kumtafuta mwakilishi huyo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema mmiliki wa eneo hilo ambaye hakumtaja jina anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano.

Amesema majeruhi wanaendelea na matibabu, na mmoja kati yao amehamishiwa Mloganzila kwa matibabu zaidi.

Vurugu zilivyotokea

Mwenyekiti wa mtaa amesema majira ya saa 10 alfajiri ya kuamkia Mei 6, 2026 alipigiwa simu na kuambiwa kuna watu wasiojulikana wamevamia eneo hilo wanavunja nyumba.

Amesema alimpigia simu OCD na Polisi Pata sanjari na Polisi Jamii ili kwenda kutoa msaada.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

Amesema wakati wanafika eneo la tukio walikutana na watu kama 300 waliofika Lupaso kwa usafiri wa mabasi madogo sita aina ya Toyota Coaster, ambao walikuwa na mapanga na nyundo wakivunja nyumba za wananchi.

“Wakati huo wananchi pia walikuwa wanapiga filimbi kuitana, ndipo zikatokea vurugu kubwa zilizosababisha vifo vya wale mabaunsa watatu, wananchi wakajeruhiwa na ukatokea uharibifu wa mali kadhaa zikiwemo nyumba,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *