
Dar es Salaam. Uteuzi wa Katibu Mkuu wa chama cha NCCR- Mageuzi, Evaline Munisi, kuwa mbunge na naibu waziri umekigawa chama hicho.
Aprili 2, 2026, Munisi aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mbunge. Mwezi mmoja baadaye, Mei 2, 2026, alimteua kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano).
Uteuzi huo uliibua mijadala ndani na nje ya chama chake, kwamba inawezekanaje akateuliwa na akaendelea na majukumu yake ya katibu mkuu wa chama.
Mei 3, 2026, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Joseph Selasini, alipozungumza na Mwananchi juu ya uteuzi huo alisema hauna dhamira njema, akikitenga chama na nafasi mpya ya Munisi.
“Munisi ni Katibu Mkuu wetu. Ameteuliwa kuingia kwenye Baraza la Mawaziri na atalazimika kusimamia sera za chama kingine, ambacho hatulingani kiitikadi, hivyo hatuwakilishi upinzani,” alisema.
Alisema uteuzi huo hauna maana yoyote kuelekea maridhiano, na kwamba unaweza kuleta mgawanyiko zaidi ndani ya upinzani.
“Kwa upande wetu, huyo si mwanachama wetu kwa vitendo tena. Mwanachama lazima asimame na itikadi na sera za chama chake. Huwezi kutekeleza ilani ya chama kingine na bado ukadai uko kwenye chama chako cha awali,” alisema.
Leo Alhamisi, Mei 7, 2026, chama hicho kimekutana na waandishi wa habari makao makuu yake, Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu, Faustina Sungura, amesema uteuzi huo uliofanywa na Rais Samia kwenye chama chao wameupokea kwa mikono miwili.
“Tumshukuru Rais Samia kwa kuangazia chama na kumteua katibu kkuu wetu, Eveline kuwa mbunge na naibu waziri, na tunamualika aendelee kumualika ndani ya NCCR -Mageuzi ateue wengine watakaofanya nao kazi,” amesema.
Sungura amesema NCCR- Mageuzi wameupokea uteuzi huo na wanaunga mkono, akiwakemea baadhi ya wanachama wanaojitokeza kumshambulia kiongozi huyo baada ya kuteuliwa na Rais Samia.
Amesema baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho wanaojitokeza kumtolea maneno ya kashfa kiongozi huyo walikuwa na masilahi binafsi ambayo walishindwa kuyafanikisha dhidi ya kiongozi huyo, ikiwemo kumtweza utu wake.
“Baadhi ya viongozi ndani ya NCCR wamekuwa wakimshambulia Eveline kuwa si mwanachama, chama kinaunga mkono uteuzi wa Rais. Hao watu walitaka mambo binafsi kumdhalilisha Eveline, kumtweza utu wake, kumtishia kuondoka kwenye chama kwamba atapoteza ubunge wake. Hili ni jambo la kusikitisha,” amesema.
Sungura amesema NCCR Mageuzi itaendelea kumlinda katibu mkuu huyo na haiwezi kutishwa na watu wenye tamaa, akisisitiza chama cha upinzani kupata fursa kuingia serikalini si jambo dogo, kwani watatumia fursa hiyo kusukuma ajenda zao.
“Watovu wote wa nidhamu ndani ya chama hatua kali zitachukuliwa hivi karibuni, watuhumiwa watapelekewa mashtaka yao ili wajibu tujue hatua za kuchukua,” amesema.
Amesema nafasi ya katibu mkuu ndani ya NCCR- Mageuzi ni ya Eveline na majukumu aliyopewa na Rais Samia hayawezi kuathiri utendaji wake ndani ya chama, labda mwenyewe aamue kuachia nafasi hiyo.
“Eveline alijiunga NCCR kwa mapenzi yake, hivyo suala la kukaa milele ndani ya chama hicho hatuwezi kutabiri. Tunachojua kama mwanachama wa NCCR -Mageuzi amepata heshima akiwa ndani ya chama na ataendelea kulinda heshima hii akiwa ndani ya chama,” amesema.
Katika hatua nyingine, Sungura amesema ili chama kichukue nchi kinapaswa kuwa na nguvu ya wanachama na viongozi bora, na ndiyo maana Rais Samia ameona ndani ya chama hicho wapo viongozi bora.
Akizungumzia sera itakayotekelezwa na Evaline wakati akiwa mwanachama wa NCCR -Mageuzi, Sungura amesema utekelezaji wa sera na ilani utakuwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akitumia kauli ya mwanafalsafa Socrates kuwa ‘siwezi kumfundisha mtu yeyote kitu chochote bali nitawafanya wafikiri.’
Kauli ya wachambuzi
Msimamo huo wa NCCR Mageuzi umeibua maoni tofauti kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wakisema kauli ya chama hicho imeonesha ustaarabu wa kisiasa kwa kutambua uteuzi wa mwanachama wao kama fursa ya kitaifa badala ya sababu ya mgawanyiko.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Magabilo Masambu, amesema katika mazingira ya siasa za Tanzania ambako mara nyingi uteuzi wa viongozi wa upinzani huibua migogoro ndani ya vyama, msimamo wao unaonesha chama kinaangalia zaidi maslahi mapana ya Taifa kuliko siasa za ushindani pekee.
“Kauli yao inaashiria mabadiliko ya siasa za maridhiano na ushirikishwaji. Rais Samia kwa muda mrefu ameonekana kuendesha siasa za kujenga madaraja kati ya Serikali na vyama vya upinzani.
“Kwa hiyo, hatua ya NCCR kupongeza uteuzi huo badala ya kuupinga inaweza kusaidia kupunguza siasa za chuki na kuongeza mazingira ya mazungumzo ya kisiasa nchini,” amesema.
Masambu ameeleza kuwa NCCR Mageuzi kinaonesha kujiamini kisiasa. Kumruhusu katibu mkuu wao kuendelea kushika nafasi ndani ya chama huku akiwa serikalini ni ishara kwamba wanaamini uwezo wake wa kutenganisha majukumu ya Serikali na chama.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Paul Loisulie, amesema uteuzi wa Evaline kufanywa na kiongozi mkuu wa nchi si wa kwanza.
Amesema Hamad Rashid aliwahi kuteuliwa na Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa, awamu ya nne, James Mbatia akiwa kiongozi wa NCCR Mageuzi naye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, akisisitiza kuwa uteuzi huo si jambo jipya.
“Hakuna mwongozo kwamba Rais lazima ateue mbunge kutoka wapi au waziri kutoka wapi. Huo ni utashi wake mwenyewe. Suala la NCCR Mageuzi ni mambo yao wenyewe wataamua nini, kwa sababu hakuna wa kwenda kuwapangia jambo la kuamua, lakini tufahamu tu siasa ni ngumu kuliko fizikia, mambo ambayo hayawezekani kwengine kwenye siasa yanawezekana,” amesema.