
KLABU ya Simba ishindwe yenyewe sasa baada ya beki wa kati waliokuwa wakimuhitaji katika dirisha dogo la Januari 2026, Mkongomani Ndongani Samba Gilbani, kutaka kuondoka mwishoni mwa msimu kwenye timu anayocheza ya Asante Kotoko ya Ghana.
Beki huyo alikuwa akihusishwa na Simba katika dirisha dogo la Januari 2026, ingawa licha ya kufikia makubaliano na yeye mwenyewe, lakini ilishindwa kukubaliana na waajiri wake, Asante Kotoko na dili hilo kushindwa kukamilika kama ilivyopangwa.
Taarifa kutoka Ghana, zinaeleza mchezaji huyo ameonyesha nia ya kuondoka mwishoni mwa msimu huu, baada ya dili lake la awali la kujiunga na Simba kuota mbawa, huku ikidaiwa malengo yake yalikuwa ni kucheza Ligi Kuu Bara tangu Januari 2026.
Beki huyo ambaye ni muhimili mkubwa Asante Kotoko, inadaiwa amewekewa mkataba mpya kwa ajili ya kuendelea kubakia ndani ya timu hiyo, ingawa malengo yake ni kutaka kuondoka ili akatafute changamoto sehemu nyinyine.
Licha ya Simba kuonyesha nia ya kumuhitaji, ila taarifa kutoka Ghana zinadai zipo timu mbalimbali pia zinazomuhitaji, ambapo kwa Tanzania nyingine inayomuhitaji ni TRA United na moja kutoka Ufaransa, ambayo hata hivyo, haijawekwa wazi.
Beki huyo aliyezaliwa Februari 2, 2000, akiwa na miaka 26, amekuwa lulu sokoni kutokana na uhodari wake wa kujua kusoma mchezo, ambapo alijiunga na Asante Kotoko ya Ghana tangu Julai 11, 2024, baada ya kuachana na Rahimo FC ya Burkina Faso. Mkataba wake na Asante Kotoko unamalizika mwisho wa msimu huu.